TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Tuesday, June 21, 2011

Dk Mkumbo:Tuchukue hatua, taifa limo katika mtikisiko wa elimu


Dk Kitila Mkumbo

TAKWIMU zinaonyesha kutoka mwaka 2008 hadi 2010, zaidi ya nusu ya wahitimu wa kidato cha nne wamekuwa wakifanya vibaya kwa kupata madaraja ya nne na sifuri.

Kama haitoshi, masomo ya sayansi na hesabu yameendelea kuwasumbua wanafunzi wengi, jambo linaloweka rehani jitihada za serikali na wadau kuongeza wataalamu wa fani hizo ambao ni muhimu katika maendeleo ya nchi.

Dk Kitila Mkumbo, Mkuu wa Idara ya Saikolojia ya Elimu na Masomo ya Mitalaa ya Shule Kuu ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anazungumzia sababu zinazoitikisa sekta ya elimu nchini kama alivyohojiwa na mwandishi wetu Gedius Lwiza.

Swali: Nini maoni yako kuhusu jitihada zinazoendelea kuhakisha elimu inayotolewa nchini inakuwa bora?
Jibu: kwa hali ilivyo sasa, elimu bora ni ndoto na hali ni mbaya kadiri siku zinavyosonga mbele.Tutegemee miujiza gani katika harakati za kupata elimu bora ikiwa wahusika kila wanapoambiwa, wanalichukulia kama suala kawaida? Kwa hali hii ni dhahiri kuwa taifa linaelekea kubaya.

Swali: Umesema hali ni mbaya, lakini hivi mnawashirikisha viongozi mnapofanya tafiti na kubaini changamoto katika shule hasa zile za umma?
Jibu: Tunawafahamisha, lakini hali ya kusikitisha ni kwamba, wahusika wamejikita katika siasa zaidi na ndio maana wanashindwa kuzisaidia shule za umma.Hali ni mbaya katika shule za kata, ni kwa sababu hii, viongozi hawataki kuwapeleka watoto wao katika shule hizi. Wengine wanawapeleka watoto nje ya nchi.

Swali: Kama hali iko hivi, nini mustakbali wa elimu yetu?
Jibu: Ukweli ni kwamba kwa sasa nchi iko kwenye mtikisiko mkubwa wa elimu, kutokana na kitendo cha serikali kuamua kudharau mtihani wa kidato cha pili ambao ulikuwa muhimu.

Ukitoa marufuku ya mtihani huo iliyowafanya wanafunzi kuwa wazembe, maendeleo ya elimu yanakwamishwa na kuwapo kwa mazingira mabovu shuleni ikiwa ni pamoja na uhaba wa walimu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

Jambo jingine linaloonekana kuwa hatari katika siku zijazo, ni kitendo cha kuwatumia walimu ambao hawana sifa katika ufundishaji. Matokeo yake ni kuendelea kuwalaumu walimu wakati wanaotakiwa kulaumiwa ni wale wanaoruhusu kuwatumia walimu wasiokuwa na sifa.

Swali: Wadau wengi wanataka kurejeshwa kwa mtihani wa kidato cha pili na ule wa darasa la nne, nini umuhimu wa mitihani hii katika mfumo wetu wa elimu?
Jibu: Unajua mtihani ni kipimo muhimu kwa mwanafunzi kuweza kufahamu kama amefanikiwa kuelewa mambo aliyofundishwa au la.Mitihani huwapa wanafunzi ari katika kujisomea.

Kitendo cha kuondoa mtihani huo ni sawa na utovu wa nidhamu shuleni, maana mtihani huo ulikuwa unamjenga mwanafunzi kuwa na utayari wa kufanya mtihani na kuacha uzembe akiwa shuleni. Hivi sasa wanafunzi wana hali mbaya kwani wameanza kuwa wavivu

Swali:Uhaba wa walimu umekuwa changamoto kubwa nchini kwa miaka mingi. Kwa nini shule zikose walimu ilhali maelfu ya wanafunzi wa ualimu wanahitimu kila mwaka vyuoni?
Jibu: Sikubaliani na kauli kuwa kuna ukosefu wa walimu. Walimu wapo wengi na kila mwaka vyuo vikuu vinatoa maelfu ya walimu, lakini sababu kubwa inayowakimbiza ni kuwapo kwa mazingira mabovu ya kufanyia kazi. Ni kwa sababu hii, wanaamua kufanya kazi tofauti na ualimu.

Unajua hakuna mtu ambaye hataki kufanya kazi katika mazingira bora na maslahi bora. Ukitaka kuamini nenda katika shule binafsi, utaona miujiza kwani kila kitu kipo kuanzia maabara, maktaba na walimu.
Kwa nini matatizo yapo katika shule za serikali peke yake? Ni wazi serikali ikiamua shule za kata nazo zinaweza kuwa kama hizi binafsi.

Swali: Lakini ualimu ndio fani waliyoisomea tena baada ya kuichagua wao wenyewe?
Jibu: Unajua kwa sasa, wengi wanaichukulia fani ya ualimu kama njia ya kupita hasa walimu wa sayansi. Walimu wa sayansi kwa mfano, wanapata asilimia 100 ya mkopo, kwa hiyo baada ya kumaliza masomo yao wanakwenda kufanya kazi katika shule binafsi au kazi zingine tofauti na ualimu.Pia ukumbuke watu waliosoma sayansi wana nafasi kubwa katika soko la ajira.

Shule zinakosa walimu wa sayansi kwa sababu kila mtu anaposoma fani fulani, anahitaji fani hiyo aifanye kwa vitendo. Lakini, kitendo cha mwalimu aliyesoma sayansi kumpeleka katika shule ambayo haina maabara pamoja na vifaa vyake ni sawa na kumharibia utaalamu wake

Swali: Kwa nini shule za vijijini zinafanya vibaya zaidi kuliko zile za mijini?
Jibu: Shule kuwa kijijini sio sababu ya kuwafanya wanafunzi wafeli, bali shule za serikali zimetelekezwa na walimu wanaotegemewa, wametupwa huko bila kupewa vitendea kazi. Pia wanapewa maslahi duni.

Kuna utafiti ambao umefanyika sehemu za vijijini kuhusu shule za watu binafsi na shule za serikali.Iligundulika kuwa shule za watu binafsi ambazo ziko vijijini na zina kila kitu kama vifaa vya kufundishia na kujifunzia, walimu wa kutosha na wenye sifa zinafanya vizuri.

Swali: Kwa haya uliyoyasema na hata uzoefu wa mambo ulivyo, bila shaka elimu yetu inaporomoka, tufanyeje?
Jibu: Kutokana na hali ya elimu kuendelea kuporomoka, hakuna haja ya kuendelea kutafakari, bali sasa tuchukue hatua. Haiwezekani kuendelea kulifumbia macho suala hili kwani kufanya hivyo ni kuendelea kujenga taifa lisilokuwa na watu wa kuliendeleza taifa lenyewe.

No comments: