TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Wednesday, June 22, 2011

CCM wajifunza kwa viboko Arusha • Wamsikia Lowassa, CHADEMA yatwaa unaibu meya

MGOGORO wa umeya katika jiji la Arusha uliosababisha vifo vya watu watatu mwanzoni mwa mwaka huu umemalizika jana baada ya madiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukubaliana kugawana madaraka.

Kumalizika kwa mgogoro huo kumekuja baada ya madiwani wa vyama hivyo kukubali kuweka kando tofauti zao za kisiasa na kuitisha mkutano maalum wa Baraza la Madiwani lililokutana jana chini ya uenyekiti wa Diwani wa Sokoni (1), Michael Kivuyo, anayetokana na chama cha Tanzania Labour (TLP).

Hatua ya CCM kukubali kukaa meza moja na CHADEMA na hatimaye kukubaliana kumaliza mgogoro huo, imekuja ikiwa ni miezi zaidi ya sita tangu viongozi wa juu wa chama hicho tawala chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Yussuf Makamba, walipoamua kuupinga ushauri uliotolewa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyetaka vyama hivyo vikae chini na kumaliza mvutano wao kwa amani.

Katika kikao hicho cha usuluhishi kilichotanguliwa na vile vya kamati za vyama hivyo kilimalizika kwa kumchagua pasipo kupingwa, Estomih Mallah wa CHADEMA kuwa Naibu Meja wa Arusha. Mallah ndiye aliyekuwa mgombea wa umeya wakati mgogoro huo ulipoibuka.

Akizungumzia ushindi huo wa Mallah, Meya wa Arusha Gaudence Lyimo, ambaye kuchaguliwa kwake kulipingwa na CHADEMA hata kusababisha maandamano yaliyofuatiwa na vifo vya watu watatu waliouawa na polisi kwa kupigwa risasi, alimpongeza naibu wake akimwelezea kuwa ni mtu mwenye busara na hekima na ambaye anao uwezo wa kushughulikia ipasavyo kero za madiwani.

Chini ya makubaliano hayo, vyama vya CHADEMA na CCM vimekubaliana kuongoza Kamati za Kudumu kwa kupokezana wakati kwa upande wa wadhifa wa unaibu meya utashikiliwa na CHADEMA kwa kipindi cha miaka minne, huku kwa kipindi cha mwaka mmoja utakaokuwa umebaki, nafasi hiyo itashikwa na diwani anayetokana na TLP.

Mbali ya kumchagua naibu meya, mkutano huo maalum wa baraza la madiwani ulichagua wenyeviti wa kamati za kudumu ikiwemo ya Uchumi , Elimu na Afya ambapo alichaguliwa Diwani wa Elerai, John Bayo (CHADEMA) wakati Kamati ya Mipango Miji, Mazingira na Ujenzi ilikwenda kwa Ismail Katamboi (CCM).

Akizungumza baada ya kikao hicho, Meya Lyimo aliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni pasipo kupendelea chama chochote.

Katika kuonyesha mshikamano, madiwani hao walishikana mikono na kuimba wimbo wa kuonyesha mshikamano hali iliyosababisha ukumbi mzima kulipuka kwa shangwe iliyoashiria kumalizika kwa tofauti za kisiasa zilizohitimishwa kwa maafa.

Mara baada ya kutoka katika kikao hicho, madiwani wa vyama vyote hawakuwa tayari kuzungumzia mgogoro miongoni mwao wakisisitiza kwamba walikuwa wamefikia hatua ya kuangalia mbele kwa maslahi ya wakazi wa jiji la Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mikutano, Kivuyo aliyekuwa mwenyekiti wa vikao vya usuluhishi alisema madiwani wanaounda baraza lao kutoka vyama vya CCM, CHADEMA na TLP, walianza kukutana miezi minne iliyopita, katika vikao ambavyo vilimhusisha pia Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Raymond Mushi aliyekuwa mshauri.

Kivuyo alisema kuwa walifikia uamuzi wa kutafuta ufumbuzi wa mgogoro kwa pamoja baada ya kutafakari kwa kina na kubaini kuwa suala hilo linaweza kusababisha kudumaa kwa maendeleo ya wananchi wa Arusha.

Akizungumzia usuluhishi huo na ushindi wake, Naibu Meya, Mallah, alisema alikuwa ana imani kubwa kwamba baada ya kumalizika kwa tofauti zao walikuwa na wajibu wa kukaa pamoja kama madiwani waliochaguliwa na wananchi kwa ajili ya kupanga na kutekeleza wajibu waliotumwa na wapiga kura wao.

“Kikubwa mimi ni diwani na ninaendelea kuwa diwani. Nafasi niliyokuwa nayo hainibadilishi. Sasa tumeungana madiwani wote tunapaswa kukaa pamoja kujadili, kupanga na kutekeleza majukumu yetu kwa kuzingatia maslahi ya wananchi wa Arusha waliotutuma tukawawakilishe,” alisema Mallah.

Akizungumza kwa simu kutoka Dodoma anakohudhuria vikao vya Bunge, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (CHADEMA), alisema kuwa yeye hana shida na uamuzi uliofikiwa kwenye kikao hicho, ili mradi tu suala hilo liwe limefikiwa kwa kuzingatia sheria, kanuni, haki, ukweli na uwazi.

“Mpaka sasa bado sijapata taarifa rasmi juu ya suala hilo ila hao waliotuwakilisha kwenye vikao vya usuluhishi ni watu tunaowaheshimu na kuwaamini hivyo mimi sina tatizo endapo maamuzi hayo yamefanyika kwa misingi ya haki, ukweli na uwazi,” alisema mbunge huyo.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Arusha, Mushi, akijibu maswali ya waandishi endapo njia waliyoitumia kumaliza mgogoro huo haitadumaza demokrasia, alinukuu kauli aliyodai ilitolewa na Rais Kikwete kuhusiana na mgogoro huo kuwa jambo hilo ni la bahati mbaya na asingependa litokee tena.

Kwa upande wa wananchi, mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa anaamini hawatakuwa na pingamizi lolote kwani waliwachagua madiwani wao wakawawakilishe kwenye halmashauri na si kwa nafazi za umeya au unaibu meya.

Mushi alimsifu Naibu Meya, Mallah, kwa ushirikiano aliounyesha katika kipindi chote cha vikao vya kutafuta suluhu kwa madai kuwa alihakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi kwa maslahi ya wananchi wa Arusha.

Wajumbe wa CCM waliokuwa wakiingia katika baraza hilo la usuluhishi walikuwa, madiwani Abdulrahman Tojo, Ismail Katamboi, Lillian Mmasi, Karim Moshi, Meya Lyimo na Katibu wa chama hicho wilayani Arusha, Mussa Sunja.

Kwa upande wa CHADEMA wajumbe walikuwa ni madiwani Ephata Nanyaro, John Bayo, Naibu Meya Mallah na katibu wa chama hicho mkoani hapa, Amani Golugwa, wakati TLP iliwakilishwa na Kivuyo aliyekuwa mwenyekiti wa vikao hivyo.

Uchaguzi wa Meya Arusha uliingia dosari baada ya kufanyika bila ya kuhusisha madiwani wa CHADEMA, hali ambayo ilisabisha chama hicho cha upinzani kuitisha maandamano ya amani Januari 5, mwaka huu, ambayo yalizuiwa na polisi ambao katika kujaribu kuwatawanya waandamanaji waliwaua watu watatu.

Mauaji hayo yalisababisha pia kukamatwa kwa viongozi wa juu wa CHADEMA waliokuwa wakiongozwa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe, na Katibu Mkuu wake, Dk. Wilibrod Slaa, ambao na wenzao wengine walifunguliwa mashtaka. Kesi yao bado inaendelea.

No comments: