TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, May 26, 2011

WANAHARAKATI WATOA TAMKO KUHUSU MUONGOZO WA BAJETI

TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI
MADAI YETU KWA MUONGOZO WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012- 2015/16

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia kikundi kazi chake cha uchambuzi wa bajeti (Budget Analysis Task Team) wakishirikiana na wanaharakati wengine kutoka ngazi ya jamii wamefanya uchambuzi wa muongozo wa mpango wa miaka mitano wa bajeti kwa mwaka wa fedha utakaoanza Julai mwaka 2011/2012 hadi 2015/16 . uchambuzi huu umefanywa kwa mtazamo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi, wakiongozwa na kauli mbiu ya “Haki ya Uchumi: Rasilimali Ziwanufaishe wanawake walioko Pembezoni”.

Uchambuzi huu umefanyika katika muktadha ambapo ndio kwanza nchi imetoka katika uchaguzi na bunge ni jipya pamoja na hali ya vuguvugu la kudai mabadiliko ya katiba mpya ambayo ni homa kubwa kwa serikali pamoja na wananchi. Kwa hiyo mategemeo makubwa yalikuwa kuona msimamo wa serikali katika kutetea haki ya wananchi, kwa kuelekeza rasilimali za kutosha ili kufanikisha mchakato huu wa mabadiliko ya katiba, ambao ndio mhimili kwa wapiga kura walio wengi, hasa wanawake walioko pembezoni. Tumeshangaa kuona kuwa hakuna mikakati mahususi ya kuelekeza rasilimali ktaika eneo la katiba.

Vipaumbele vilivyoainishwa katika muongozo wa bajeti kwa mpango wa miaka mitano vimeelekezwa zaidi kwenye; Kilimo, miundo mbinu, viwanda, uwekezaji katika rasilimali watu,mazingira endelevu,usimamizi wa ardhi, mipango miji na makazi,kuimarisha mahusiano kati ya sekta ya umma na binafsi na kuendeleza mafanikio katika sekta za kijamii. Je vipaumbele hivi vimetokana na mpango wa uibuaji wa fursa na vikwazo kwa maendeleo (O & OD) ambao unatoa nafasi kwa walio wengi kuibua vipaumbele vyao wenyewe? Nani anafunaika zaidi, wawekezaji wakubwa au wawekezaji wadogo.Kwa upande wa kuwekeza katika rasilimali watu, ni kwavipi kila sekta iatongeza ajira kwa watu na ni ajira za namna gani?

Muongozo wa bajeti uliopangwa kwa mwaka 2011/2012 unatarajiwa kuwa Shilingi. 11,970,356 ukilinganisha na 11,609,557 mwaka 2009/2010ambapo bajeti inazidi kuwa kubwa wakati huohuo mapato ya ndani yanazidi kushuka. Ikizingatiwa kuwa bajeti ya serikali ni tegemezi kwa kiasi kikubwa kwa wafadhili na deni la taifa linazidi kukua kutoka Shilingi 7.6 bilioni (2008/2009) hadi Sh10.5 trilioni (2009/2010) ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 38 (Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali), je ni kwavipi serikali inapanga kuongeza ukubwa wa bajeti wakati mikopo na misaada ya wafadhili haitabiriki?Tunadai serikali ipunguze utegemezi wa bajeti kutoka kwa wafadhili kwa kuboresha ukusanyai wa mapato ya ndani na kupunguza ukubwa wa serikali, yaani wizara, mawaziri na manaibu Waziri kufikia kiasi ambacho hakitaathiri sana ukubwa wa bajeti.

Muongozo wa bajeti unasisitiza uimarishaji na uendelezaji wa masuala ya uchumi mpana na siasa kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kuzuia mfumuko wa bei, kuendeleza sekta binafsi, kusimamia usawa katika bei ya mafuta kwa kuwekeza kupitia rasilimali watu. Sisi kama wanaharakati tulitarajia kuona muongozo huu wa bajeti unaweka kipaumbele katika kusimamia mgawanyo sawa wa rasilimali katika jamii, kurasimisha kazi zisizo na kipato zinazofanywa na wanawake. Pamoja na masuala mengine, suala la ‘mabadiliko ya dhana’ yaani ‘paradigm shift’ na kuipa ‘fursa’ kipaumbele zaidi kuliko ‘mahitaji ya watu’ inatupa wasiwasi sana; tunadai kwamba inatakiwa mdahalo wa kitaifa juu ya mawazo haya, maana inaweza kuwa na matokeo ya ajabu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa na wa watu wake.Tunapinga suala la kuweka kipaumbele katika uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kwa wawekezaji wakubwa wakatai soko la ndani la bidhaa linakufa.

Tumeshangazwa sana kuona kwamba pamoja na juhudi zote za serikali kuendeleza kilimo na kuwa na mkakati wa mapinduzi ya kijani “Kilimo Kwanza”, ukuaji wa kilimo unatarajiwa kukua na kufikia wastani wa 5.5% tu. Ukuaji huu hauendani kabisa na umuhimu wa kilimo kwa watanzania walio wengi. Halikadhalika pamoja na kilimo kuwekewa kipaumbele, mchango wa kilimo katika pato la taifa unatarajiwa kupungua kutoka asilimia 21.9 (2010) hadi 18.7 (2011) na hii itakuwa na athari kubwa kwa wakulima wadogo wengi wanaotegemea sana kilimo hasa jamii wengi wao wakiwa wanawake.

Tunasikitishwa kuwa bado hakuna mkakati wa wazi au chanzo mbadala cha nishati kama vile gesi, upepo au makaa ya mawe kwa ajili ya kutatua changamoto iliyopo ya umeme. Miaka 50 baada ya uhuru tunadai kwamba kila Mtanzanaia ana haki ya umeme akiwa kijijini au mjini. Pia tulitarajia kuona serikali inaliimarisha shirika la umeme nchini (TANESCO) kwa kulijengea uwezo ili kuondokana na tatizo la ukodishaji mitambo ya uzalishaji umeme, ambapo mara kwa mara mitambo hiyo imekua ikiligharimu taifa kutokana na kuwepo kwa udanganyifu katika manunuzi na ukodishwaji wake. Tunadai uwajibikaji kuanzia kwa Waziri hadi maafisa wengine wanaohusika na suala la nishati ya umeme nchini.

Kwa upande wa sekta ya elimu, serikali kuendelea kubajeti wastani wa shilingi 1,500 kwa kila mwanafunzi kwa siku kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari haiendani na hali halisi ya mahitaji ya lishe na kupanda kwa maisha. Asilimia 40 ya “capitation grant” kwa wanafunzi hutolewa kwa ajili ya ununuzi wa vitabu lakini hali halisi iliyopo inaonyesha kwamba shule nyingi za msingi kufikia mwezi Disemba 2010 zimepokea kiasi kisichozidi jumla ya Shilingi 60, 000 hadi 300,000/= kwa ajili ya kununulia vitabu vya kiada na ziada kwa mwaka 2009/2010 (rejea report ya Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2010). Hali hii tunayoiona ni kwamba shule nyingi hazina vitabu na kila mtoto anaambiwa ajinunulie vitabu. Tunahoji pesa hizi zinakwenda wapi?

Katika Sekta ya Afya muongozo haukueleza ni jinsi gani serikali itakabiliana na changamoto za uzazi salama. Tunakumbuka na kuunga mkono ahadi ya Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii kwamba kila mama mjamzito atapewa vifaa vya kujifungulia bure,tunadai utekelezaji wa ahadi hiyo ya wizara. Tulitarajia kuona muongozo unaelekeza kutengwa kwa bajeti ya Afya inayoanzia 15% kama ilivoelekezwa katika azimio la Abuja pamoja na mikakati mahususi ya kuhakikisha eneo la afya linaboreshwa. Na je pia kuna vivutio gani vitatolewa kwa manesi wakunga wanaofanya kazi katika mazingira magumu?

Kutokana na yaliyojitokeza katika muongozo wa bajeti, sisi kama wanaharakati wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi tunadai yafuatayo:

• Kutengwa kwa rasilimali zakutosha zitakazowezesha mchakato wa mabadiliko ya katiba kufanyika kwa ufanisi zaidi.
• Ushiriki zaidi wa wananchi katika kuainisha vipaumbele vyao.
• Mikakati ya kuimarisha soko la bidhaa za ndani kwa kuimarisha barabara za vijijini zitakazosaidia kuchukua mazao ya wakulima wadogo wadogo ambao wengi wao ni wanawake ili kuinua pato la ndani la taifa na kuimarisha uchumi mkuu.
• Mikakati maalum ya kuongeza ajira, maisha endelevu na kipato kwa wote, wanawake na wanaume, mijini na vijijini.

Hitimisho

Mwongozo wa bajeti ni lazima ulenge namna uchumi wa nchi utakavyojenga maisha ya watu wake kwanza na si kuangalia wageni , suala la ajira na maisha endelevu kwa wote liwekewe kipaumbele. Mahsharti yawekwe kwa wawekezaji ili kila mmoja (awe wa ndani au nje) aongeze idadi ya wafanyakazi kwa asilimia kadhaa kufuatana na sekta husika. Katika utekelezaji wa malengo ya MKUKUTA II lazima muongozo uzingatie masuala ambayo yataleta maendeleo kwa wananchi hasa wanawake walioko pembezoni na si kuangalia masuala ambayo yatawafanya wawe watumwa katika nchi yao. Suala la mahusiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) litazamwe kwa kina zaidi kuona nani anafaidika zaidi, wawekezaji au wananchi? Kwa hiyo tunadai mwongozo wa bajeti ambao utaboresha maisha ya jamii maskini hasa wanawake walioko pembezoni.

No comments: