TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, May 26, 2011

UVCCM ARUSHA WATAKA MAPACHA WATATU WA UFISADI WANG'OKE HARAKA: HARAKA:



Hali si shwari ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha, na lile zengwe lilioanza wiki iliyopita likimtaka Katibu wa chama mkoa, Mary Chatanda, ang’oke limejibiwa kwa nguvu miongoni mwa makundi yanayokizana huku lawama zikielekezwa kwa viongozi watatu waandamizi.

Msuguano huu unaakisi harakati za kuwania kiti cha ubunge jimbo la Arusha Mjini ambacho chama hicho kilipoteza na kuchukuliwa na Godbless Lema (Chadema), huku mgombea wa CCM, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk. Batilda Buriani, akiangushwa.

Jana wanachama wa Umoja wa Vijana (UVCCM), waliibuka na kutoa madai mazito juu ya uchaguzi huo, huku wakitaka mapacha watatu wenye shutuma za ufisadi ndani ya chama hicho watimuliwe haraka kukinusuru chama hicho.

Waliwataja mapacha hao kuwa ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa huo, James Ole Millya, naye ametakiwa kuachia ngazi akidaiwa kuwa ni kibaraka wa mafisadi.

Viongozi wa UVCCM ngazi ya mashina, matawi, kata na wilaya zote za mkoa wa Arusha, pamoja na wanachama wa umoja huo, jana walikutana na waandishi wa habari ambapo walitoa tamko zito kuhusu masuala makuu sita waliyodai yanakivuruga chama hicho mkoani hapa.

Hata hivyo, kikao hicho hakikuhudhuriwa na Mwenyekiti wa umoja huo Mkoa, Millya pamoja na katibu wake Abdallah Mpokwa.

Akisoma tamko hilo jana, Ali Babu, aliyejitambulisha kuwa ni Mjumbe wa Baraza la Vijana wa Wilaya ya Arusha, alisema wanaunga mkono uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kwa kuona umuhimu wa kuifanyia kazi kwa vitendo falsafa ya kujivua gamba.

“Tunaipongeza na kuiunga mkono Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kutambua kwamba mafisadi wamechangia sana kukidhoofisha na kukipotezea mvuto chama chetu mbele ya umma wa Watanzania ... kwa mantiki hiyo, tunatamka kwa kauli moja kwamba mapacha hao watatu wa ufisadi ambao ni Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge na vibaraka wao wafukuzwe mara moja kwa maslahi ya CCM na Watanzania,” alisema.

Pia alisisitiza kuwa Chenge aondolewe kwenye Kamati ya Maadili ya CCM mara moja na wakati huo huo, Lowassa afukuzwe kwenye uenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya Umoja wa Vijana wa CCM Taifa haraka iwezekanavyo.

Azimio lingine ni kutaka Millya ambaye walidai kuwa ni kibaraka mkuu wa mafisadi mkoani hapa afukuzwe ili apate muda wa kuwatumikia mafisadi.

Katika tamko hilo, vijana hao walisema wameshaandika barua yenye kumbukumbu namba ARS/Malalamiko/01 kwenda CCM Makao Makuu kuelezea namna Millya alivyo mnafiki, mfitini, mwongo na namna asivyojali maslahi ya vijana wa UVCCM mkoa wa Arusha.

Aidha, walitoa onyo kwa mbunge wa viti maalum (Vijana), Catherine Magige, wakimtaka aache kutumia fedha za mafisadi kuwagawa vijana wa Arusha kabla hawajatumia haki yao ya kikanuni ya kumsimamisha ubunge.

Vijana hao katika tamko lao, walikiomba chama chao kiwafukuze makatibu wa UVCCM kutoka wilaya za Monduli, Arumeru, Longido na Karatu kwa kushiriki maandalizi ya maandamano haramu na kwa kukataa wito wa chama wa kwenda kutoa ushahidi wa malalamiko kuhusu mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa.

Walisema kitendo hicho cha kukataa wito wa chama ni dharau na ukosefu wa maadili.

Walisema ili kulinda hadhi ya CCM mkoa wa Arusha, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Onesmo Nangole, ajiuzulu mara moja kwa madai kuwa anafanya kazi za Lowassa.

“Kitendo cha yeye kufanya kazi ya mafisadi na si CCM, kimesababisha tupoteze majimbo mawili kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010,” tamko hilo lilisema.

Kadhalika, vijana hao katika tamko hilo walimuunga mkono Katibu wa CCM mkoani hapa, Mary Chatanda, kuwa ni mpiganaji na ni lulu ya CCM mkoa, kwa sababu amefanya mengi ya maana na wana CCM makini, wazalendo na wanaojali maslahi ya chama hicho wanatambua hilo.

Walimuunga mkono na kumtambua rasmi Mrisho Gambo kuwa ni mjumbe halali wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa kuwakilisha Mkoa wa Arusha ambaye alitangazwa kufukuzwa wadhifa wake baada ya kikao cha UVCCM kilichokaa wilayani Longido, hivi karibuni.

“Tunamuunga mkono kwa ujasiri wake, umahiri wake na uzalendo wake wa kupambana na ufisadi ndani ya chama na Tanzania kwa ujumla,” alisema.

Wakizungumza baada ya mkutano huo, Chacha Mwita Hamed, alisema anaunga mkono tamko la vijana kuhusu ufisadi.

“Vijana wametoa tamko zuri dhidi ya viongozi wao wa chama mkoa. Madai kwamba Chatanda ameuza jimbo la Arusha sio ya kweli,” alisema

Alidai kuwa Lowassa alijiingiza kwenye kampeni za Dk. Batilda Buriani jambo ambalo liliwaudhi sana wanachama na wapiga kura jimboni hapa na iwapo asingefanya hivyo huenda Buriani angeshinda.

Kwa upande wake, Odilia Abraham, alisema hawana imani na Millya na hawamtaki.



MILLYA AOMBA UCHUNGUZI

Akizungumza na blogu hii, Millya alikanusha kuwa kibaraka wa mafisadi mkoani hapa na akasema hawezi kukumbatia mafisadi.

Aliiomba Sekretariati ya CCM Taifa kutuma kamati teule mkoani hapa kuchunguza tuhuma mbalimbali za kupoteza jimbo, lakini alisema kwa maoni yake sababu kubwa ya kupoteza jimbo ni hujuma za baadhi ya wanachama.

Kuhusu Lowassa, alisema anamheshimu na kumpenda kiongozi huyo mstaafu kwa maelezo kuwa ni mwanachama mwadilifu wa CCM mkoani hapa.

Alisema vijana waliotoa kauli hiyo hawana nguvu kwa sababu hawawakilishi vijana wa mkoa wa Arusha, isipokuwa kata chache.

Alisema vijana waliotoa tamko hilo ni wale ambao walihusika katika kulipoteza jimbo hilo wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Alisema anashangaa kusikia akituhumiwa kuwa ni kibaraka wa mafisadi wakati huu, na akahoji walikuwa wapi kutoa tuhuma hizo mapema.

“Inaonekana kuwa sasa hivi wameshikwa pabaya…sasa watu wazima wakishikwa sehemu mbaya unaweza kufahamu maumivu yake,” alisema.



MWENYEKITI MKOA: NI UPUUZI

Mwenyekiti CCM Mkoa wa Arusha, Nangole alisema madai yaliyotolewa na vijana wa CCM, ya kumtaka ajiuzulu kwa sababu anafanya kazi ya fisadi ni upuuzi, kwa sababu taratibu za chama haziruhusu kufanya kazi ya mtu.

“Mimi ninafanya kazi ya CCM mkoa na sio kazi ya mtu, yaani Lowassa...na pia sifanyi kazi chini ya UVCCM, hivyo hawana uwezo wa kunishinikiza nijiuzulu...kwa kifupi hizo ni siasa za chuki za Arusha,” alisema.

Hata hivyo, alisema vijana hao wote ni wake, akimaanisha wale walioandamana wiki iliyopita na hao waliotoa tamko jana, hivyo anangalia taratibu za kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo la kutoelewana kwa pande mbili hizo.

Alisema madai kwamba mkoa wake umepoteza majimbo mawili sio hoja yenye nguvu ya kumtaka ajiuzulu kwa sababu ipo mikoa mingine ambayo imepoteza majimbo matano.

Alisema anafanya kazi kwa mujibu wa taratibu za chama na hawezi kukurupuka katika utendaji wake wa kazi.

Hivi karibuni, baadhi ya vijana waliotajwa kuwa ni wa UVCCM walifanya maandamano hadi CCM Mkoa wakimtaka Chatanda ambaye ni Katibu wa CCM Mkoa ajiuzulu kwa madai ya kukiangusha chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita.

No comments: