Mwili wa Marehemu Steven Kanumba mara baada ya kufikishwa katika sehemu ya kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya Muhimbili.
Florence Majani na Suzzy Butondo
MADAKTARI wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wamethibitisha kuwa msanii nyota wa filamu nchini Steven Kanumba, amefariki kwa tatizo la mtikisiko wa ubongo unaojulikana kitalaamu kama `brain concussion�.
`Brain concussion� ni hali ya ubongo kushindwa kufanya kazi kwa muda kutokana na mtu kuumizwa kichwa au kushikwa na kiwewe kikali.
Taarifa hizo za ndani, zilizopatikana jana Jumatatu kutoka kwa jopo la madaktari bingwa watano walioufanyia uchunguzi mwili wa Kanumba, zinaeleza kuwa tatizo hilo linaweza kumfanya mtu apoteze maisha mara moja au baada ya siku kadhaa.
Mmoja wa madaktari hao wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa kuwa si msemaji, alisema waligundua tatizo hilo baada ya kumfanyia uchunguzi huo kwa zaidi ya saa mbili.
"Tulianza kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kuanzia muda wa saa nne asubuhi hadi saa saba kasoro za mchana na tukagundua kuwa marehemu alifariki kutokana na mtikisiko wa ubongo, kwa kitaalamu brain concussion," alisema daktari huyo.
Daktari mwingine aliyeshiriki katika uchunguzi huo alizungumza kwa kifupi kuwa waligundua kuwa ubongo ulikuwa umevimba na kushuka mpaka karibu na uti wa mgongo na hivyo kuathiri mfumo wa upumuaji na ndiyo maana msanii huyo alikufa pale pale.
Daktari wa awali alisema Kanumba alipata mtikisiko wa ubongo ambao husababisha kufeli kwa mfumo wa upumuaji (cardio-respiratory failure).
�Kilichomuua hasa ni mtikisiko wa ubongo, ambao endapo unatokea katika sehemu ya nyuma ya ubongo (cerebrum), huua kwa haraka,� alisema daktari huyo.
Aliongeza kuwa, mtikisiko wa ubongo wa nyuma, husababisha matatizo ya mfumo wa upumuaji na hilo limeonekana katika mwili wa Kanumba.
Alisema: �Baada ya ubongo wake kutikiswa kwa nguvu, mfumo wa upumuaji ulifeli na ndiyo maana tumekuta kucha za Kanumba zikiwa na rangi ya bluu, huku mapafu yake yakiwa yamevilia damu na kubadilika kuwa kama maini, hizo ndizo dalili za kufeli kwa mfumo wa upumuaji.�
Aliongeza; �Mtu aliyepata mtikisiko wa ubongo huweza kutokwa na mapovu mdomoni na hukoroma kabla ya kukata roho, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kanumba kabla hajafariki.�
Daktari huyo alisema, sehemu ya maini, na maji maji ya machoni ya marehemu, vimepelekwa kwa mkemia mkuu ili kubaini endapo kuna sumu au kitu kingine katika mwili huo.
Baba mzazi azungumza
Baba mzazi wa Kanumba, Charles Musekwa Kanumba, alisimulia jinsi alivyopokea taarifa za kushtusha za kifo cha mwanaye na kusema, kilimfanya aishiwe nguvu.
Baba wa marehemu alisema alipata taarifa Jumamosi saa 10:00 usiku baada ya kupigiwa simu na dada wa marehemu aitwaye Sara Kanumba.
�Sara aliniuliza �Una taarifa yeyote kuhusu mwanao Kanumba?�, Nikamjibu kuwa sina taarifa yeyote, ndipo aliponieleza habari za kifo hicho,� alisimulia.
Alisema; �Nilizungumza na Sara kwa njia ya simu ndipo aliponiambia, Kanumba hatupo naye tena amefariki kwa kuanguka, amekorofishana na mpenzi wake amesukumwa na kuangukia kisogo na kufa palepale.�
Mzee huyo aliongeza kuwa, taarifa hizo zilimsababisha aishiwe nguvu kwa kuwa kilikuwa kifo cha ghafla na Kanumba hakuwa akiugua.
�Sikupata taarifa zozote za kuugua, basi kuanzia hapo nilianza kupigiwa simu za kupewa pole, ndipo niliamini kumbe mwanangu amefariki kweli,� alisema.
Akizungumzia kuchelewa kufika msibani, alisema hiyo imetokana na tatizo la mawasiliano kutokana na yeye kuwa amepanga mtoto wake Kanumba azikiwe Mwanza kwa babu yake ndiyo maana hakufika mapema msibani.
�Mimi nilikuwa nimepanga mtoto wangu Kanumba apitishwe hapa kwangu Shinyanga aje aagwe halafu tumpeleke mkoani Mwanza kwa babu yake kumzika huko, lakini alipokuja mama yake alinishauri kuwa huko kutakuwa na nafasi ndogo kwa sababu watu ni wengi, pia alikuwa na marafiki wengi wengine wa kutoka nje ya nchi kwa hiyo alinishawishi na tukakubaliana kumzika Dar es Salaam,� alisema Mzee Kanumba.
Pia alifuta uvumi wa baadhi ya watu ambao wamekuwa wakihoji mbona baba yake (yaani yeye baba mzazi), hajafika msibani labda kwa vile walikuwa na ugomvi na kuongeza kwamba, ugomvi katika familia upo lakini unakwisha na tayari yeye na mwanaye walishamaliza tofauti zao.
Baba wa marehemu alitarajiwa kufika jana Jumatatu usiku Dar es Salaam tayari kwa mazishi leo Jumanne katika makaburi ya Kinondoni.
No comments:
Post a Comment