TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Saturday, February 18, 2012

SIMBA CHINJA KIYOVU HAO



SIMBA inapambana na Kiyovu FC ya Rwanda leo Jumamosi katika mechi ya kwanza ya mtoano ya Kombe la Shirikisho itakayochezwa katika Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali.
Wekundu wa Msimbazi wanafukuzia ushindi ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kusonga mbele katika michuano hiyo.

Timu hiyo ndiyo yenye rekodi nzuri katika michuano ya klabu barani Afrika kwa hapa nchini. Ilifika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, ilifika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974 na ilitinga kwenye makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003.

Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti, wachezaji wa timu hiyo wameuzungumzia mchezo huo na kusema ni mgumu.

Juma Kaseja
Ni kipa namba moja wa Simba ambaye amekuwa muhimili mkubwa wa klabu hiyo. Ana uzoefu mkubwa na mashindano ya Afrika na pia alikuwemo katika kikosi cha Simba kilichocheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2003.

Kaseja, ambaye ndiye nahodha, amesema watapigana kufa na kupona ili kushinda mchezo huo.

�Utakuwa mchezo mgumu tofauti na watu wanavyotarajia, si kazi rahisi, kwani katika mpira lolote linaweza kutokea," alieleza Kaseja, ambaye alisema wamepata maandalizi mazuri.

Nassor Said `Chollo'
Beki wa pembeni mwenye kasi, nguvu na hapitiki kirahisi. Ni mzuri katika kupanda kusaidia mashambulizi, ila tatizo lake ni mpira wake wa mwisho. Anapenda kupiga mashuti makali ambayo mara nyingi hayalengi lango.

�Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huu, lengo letu ni moja tu, ushindi. Ninachowaomba wachezaji wote tujitume kuhakikisha tunashinda mchezo.�

Juma Jabu
Ni beki mahiri ingawa kwa siku za karibuni ameonekana kucheza chini ya kiwango, labda anaweza akabadilika leo kwa sababu ni mechi ya kimataifa. �Utakuwa mchezo mgumu, lakini naamini kutokana na ubora wa kikosi chetu, tutashinda.�

Juma Nyoso
Zamani alikuwa anacheza mpira wa nguvu bila kutumia akili, lakini sasa ameonekana kutulia na kucheza vizuri kama beki wa kati na watu wengi wanakiri hilo kuwa amebadilika ingawa mara nyingine kiwango chake kimekuwa kama homa za vipindi - kinapanda na kushuka.

�Kinachotakiwa ni kuhakikisha tunajilinda ili Kiyovu wasipate bao, mashabiki wasiwe na hofu tunakwenda kuwawakilisha vizuri.�

Kelvin Yondani �Vidic�
Waliompa jina la Vidic hawakukosea kwani jamaa anacheza vizuri nafasi ya beki wa kati. Tangu arejee kikosini baada ya kuitosa Simba amekuwa akipangwa na kocha Milovan Cirkovic kila mechi.

Mserbia huyo mara nyingi amekuwa akipangua safu yake ya ulinzi, lakini Yondani hamuachi nje hata siku moja. Hata hivyo, tatizo lake kubwa hana mbio.

�Mechi itakuwa ngumu lakini watu wasijali kwani tunakwenda huko kikazi, hakuna masihara, kazi ni moja tu kucheza soka na kurudi na ushindi.�

Shomari Kapombe
Kiraka wa Simba ni kinda lakini anacheza namba nyingi uwanjani. Kila namba anayopangwa amekuwa akifanya vizuri. Mchezeshe beki wa pembeni, kati, kiungo na hata winga, yeye sawa tu anakupigia kazi.
�Wachezaji wote tukitambua majukumu yetu uwanjani hakuna linaloshindikana. Simba ina wachezaji wazuri wenye viwango vya juu, hivyo naamini ushindi upo, tunachotakiwa kufanya ni kushinda, hatutaki sare.�

Uhuru Selemani
Tangu aumie goti na kukaa nje kwa muda mrefu bado hajarudisha makali yake ya zamani ingawa kuna baadhi ya mechi amekuwa msaada kwa timu yake.
�Usiulize kuhusu suala la ushindi, kwetu ni lazima kwani tuko kamili kwa mapambano. Watu wasubiri furaha tukienda Rwanda.�

Mwinyi Kazimoto
Kiungo mchezeshaji wa Simba na msumbufu uwanjani, lakini bado hajarudi katika kiwango chake kwa asilimia 100 tangu aumie Julai 10, 2011 kwenye michuano ya Kombe la Kagame na kukaa nje kwa miezi miwili.
�Watu watuombee tu hakuna linaloshindikana mbele za Mungu, tumeajiandaa vizuri, tutakwenda kupambana kwa nguvu lolote litakalotokea ni matokeo ya mpira.�

Felix Sunzu
Ana ushirikiano mzuri na Okwi kwenye eneo la ushambuliaji, sifa yake kubwa ni nguvu ya kupambana na mabeki wa timu pinzani na huwa hachoki. Ni mzuri kwa mipira ya juu kutokana na urefu wake.

�Tumejiandaa vizuri, tukishirikiana vizuri na wenzangu mambo yatakuwa poa, kinachotakiwa kila mmoja acheze kwa malengo.�

Emmanuel Okwi
Injini ya mabao ya Simba na asipokuwepo mambo yanakuwa mabaya katika eneo la ushambuliaji. Anategemewa kuimaliza Kiyovu leo Jumamosi na yeye ameapa lazima afunge bao.
�Hawatoki wale kwao, ni lazima tuwamalize. Simba hatuna masihara hata kidogo tunawafunga kwao halafu tunakuja kuwamaliza hapa nyumbani pia.�

Patrick Mafisango
Kiungo mkabaji wa timu hiyo ambaye kocha Milovan amemhamisha na kucheza kama winga mshambuliaji kutokana na ushindani wa namba uliopo katika timu hiyo.
�Soka la Rwanda nalijua na hata wachezaji wa Kiyovu nawajua, sina presha. Tutawabana na kuibuka na ushindi."

No comments: