KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.Wilbrod Slaa, ameiumbua tena serikali ya Chama cha Mapinduzi(CCM) kwa kufichua waraka maalumu wenye lengo la kudhibiti na kufuatilia kwa makini nyendo za watumishi wa serikali wanaoshabikia vyama vya upinzani.
Akihutubia juzi katika mkutano wa hadhara uliyofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Nzovwe na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu, Dk. Slaa alisema waraka huo kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi ) unawataka Makatibu Tawala wa Mikoa yote nchini kufuatilia na kupeleka takwimu za wafanyakazi wanaojihusisha na siasa sehemu za kazi.
Alisema ili kutimiza azma hiyo wametakiwa kuorodhesha kila mtumishi kwa majina kamili, kazi anayofanya, cheo kazini, itikadi ya siasa na cheo alichonacho ndani ya chama husika lengo likiwa ni kuwapata watumishi wanachama wa vyama vya siasa pinzani nchini.
Dk. Slaa ambaye alikuwa akishangiliwa kila wakati na umati mkubwa watu, alisema hatua hiyo ya serikali ni ya hatari kubwa, na akaitaka kusitisha na kuacha kuwatisha wananchi walio huru ndani ya nchi yao.
Alisema kinachojaribu kufanywa na serikali ni kutaka kudhoofisha nguvu ya upinzani, jambo litakalosababisha kuzuka kwa vurugu.
“Mchezo huu si mzuri na hauwezi kuvumilika hata kidogo kwa kuwa nchi hii ni yetu sote na yenye kutawaliwa kwa mfumo wa vyama vingi na hawa watumishi wanaruhusiwa kuendesha siasa wakati wa nje ya kazi, kwa nini serikali iamue kutoa waraka huu?” alihoji.
Dk. Slaa alisema ndani ya waraka huo kuna maelekezo kuwa Katibu Tawala yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu hayo aliyopewa na wizara basi jina lake litapelekwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ili ashughulikiwe ipasavyo.
Alisema CHADEMA itaendelea na maandamano nchi nzima kupinga baadhi ya mambo ya kifisadi ambayo serikali inayafanya na kamwe hawataogopa kufanya hivyo hata kama watakamatwa na polisi na kupelekwa mahakamani.
Aidha Dk. Slaa katika suala zima la uundwaji wa Katiba mpya alisema Chama cha Mapinduzi kupitia kikao chake cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kilitoa waraka uliowataka viongozi wa chama hicho ngazi zote kusimamia zoezi hilo katika kuhakikisha mawazo yote yatakayotolewa na wananchi yawe kwa manufaa ya CCM.
Alisema alifikiri kuwa mchakato wa Katiba ni kwa manufaa ya Watanzania wote kumbe CCM inauchukulia kwa manufaa yake na si ya wananchi.
“Tazameni, yaani haya ni mambo ya ajabu kabisa yanayofanywa na viongozi hawa, badala ya kujadili mambo ya mustakabali wa nchi juu ya hali ngumu ya maisha kwa wananchi, wao wanapanga ni jinsi gani watatekeleza azma yao ndani ya Katiba mpya kwa maslahi ya CCM na si ya Watanzania,” alisema.
CCM yahaha kumzima
Katika hali isiyotarajiwa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa juzi, ilibuni mbinu za kuzuia kutangazwa kwa mkutano wa Dk. Slaa baada ya kuitisha kikao na waandishi wa habari wa vyombo vyote katika muda ambao katibu huyo wa CHADEMA alikuwa akihutubia.
Habari za uhakika kutoka ndani ya CCM, zilisema kuwa ingawa ilidaiwa kuwa mkutano huo na waandishi wa habari ulikuwa na lengo la kumtambulisha katibu mpya wa chama hicho wilaya ya Mbeya mjini ambaye amefika baada ya yule wa awali kuhamishwa, lakini nia kubwa ilikuwa kuukwamisha mkutano wa Dk. Slaa.
Habari zinadai kuwa CCM iliwaambia waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo kuwa walitaka pia kuzungumzia masuala yahusuyo mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya ambapo wamelenga kutuma makada wa chama hicho kuelimisha umma juu ya jambo hilo.
Katibu mpya wa CCM wilaya, Raimond Mwangwale, alisema uelimishaji huo utafanyika siku tatu mfululizo kuanzia Januari 12, katika kata 36 za jimbo la Mbeya mjini.
Mmoja wa makada maarufu wa CCM alilithibitishia Tanzania Daima ukweli wa mkutano huo na waandishi, ingawa alikiri kuwa mbinu yao haikufanikiwa sana.
Alikiri kuwa hotuba za Dk. Slaa zimekuwa na madhara makubwa kwa CCM na imekuwa ni vigumu zaidi kuzifuta katika akili za wananchi ambao wameonyesha kuamini kila akisemacho.
Aendesha kikao kizito usiku
Baraza Kuu la CHADEMA mkoani hapa limepangua safu ya uongozi wa juu wa mkoa kwa kuwateua viongozi wa muda watakaokiongoza chama hicho hadi Mei.
Kikao hicho kizito kilifanyika karibu usiku mzima chini ya usimamizi wa Dk. Slaa ambaye baadaye alitangaza safu mpya ya uongozi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Nzovwe mjini hapa.
Dk. Slaa alimtangaza Peter Mwamboneke kuwa kaimu mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mbeya, nafasi ambayo ilikuwa wazi baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Sambwee Shitambala kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM)
Diwani wa kata ya Forest katika halmashauri ya jiji la Mbeya, Boid Mwabulanga, alitangazwa kuwa kaimu katibu wa chama hicho akichukua nafasi ya Eddo Mwamalala Makata.
Dk. Slaa alimtaja Joseph Kasambala kuwa ameteuliwa kuwa Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA) mkoa wa Mbeya, akichukua nafasi ya Exavery Mwalyembe.
Seleman Simbayanje ameteuliwa kuwa Kaimu Katibu wa Baraza la Wazee wakati Tamali Mbarasya alitagazwa kuwa mratibu wa wanawake wa chama hicho.
Juzi usiku Dk. Slaa ambaye ameambatana na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Rwakatare, alihamia kwenye kikao cha Baraza la Chama hicho wilaya ya Mbeya Mjini, ambako baadhi ya wanachama walidai kwamba hawana imani na Mwenyekiti wa CHADEMA Mbeya Mjini, David Mwambigija, maarufu kwa jina la Mzee wa Upako.
Habari kutoka ndani ya mkutano huo zimeeleza kuwa wajumbe wa baraza hilo waliamua kumweka kando mzee wa upako na kisha kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Kwa mujibu wa chanzo chetu kura zilizopigwa zilikuwa 231 na ni kura tano tu ndizo zilizomkataa Mwambigija huku kura 226 zikimkubali.
“Kura ya kutokuwa na imani na Mzee wa Upako ilifanyika lakini wajumbe wengi wameoyesha kumwamini na hivyo anaendelea na wadhifa wake,” kilisema chanzo chetu.
Habari zimesema kuwa kufanyika kwa mabadiliko hayo, kutaongeza kasi zaidi ya utendaji kazi hasa kwa kuzingatia kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi ndani ya chama hicho
No comments:
Post a Comment