BAADA ya kuvuja kwa taarifa za kupanda kwa posho za vikao vya wabunge, Ofisi ya Bunge jana iliibuka na kutoa ufafanuzi kuwa, ingawa mjadala huo upo, posho hizo hazijaanza kulipwa. Juma lililopita gazeti hili liliripoti taarifa za ndani kwamba posho za wabunge zimepanda kutoka Sh70,000 hadi 200,000 hivyo kufanya bajeti ya posho hizo kwa mwaka kufikia Sh28 bilioni.
Kutokana na ongezeko hilo, taarifa hizo zilisema kila mbunge atakuwa akilipwa Sh80,000 kama posho ya kujikimu (perdiem) anapokuwa nje ya jimbo lake, posho ya vikao (sitting allowance) Sh200,000 na mafuta ya gari Sh50,000 kila siku, sawa na Sh330,000 kwa siku.
Wakati taarifa hiyo inaripotiwa, Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashililah alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu yeye si msemaji wa Bunge na akashauri atafutwe Spika wa bunge.
Lakini, baada ya mjadala wa takriban juma moja wa wanaharakati, wabunge na wasomi kupinga nyongeza hiyo ya posho, jana Dk. Kashililah aliibuka na kukiri kuwa wabunge wanataka waongezewe posho za vikao, lakini mapendekezo hayo, hayajaanza kutekelezwa. Dk. Kashililah alitoa kauli hiyo katika taarifa yake aliyoisambaza kwa vyombo vya habari jana.
Kwa mujibu wa Katibu huyo bunge, mapendekezo ya kutaka posho za wabunge zipande, yaliibuka katika mkutano wa wabunge mjini Dodoma Novemba 8 mwaka huu, lakini hadi sasa hayajaanza kutekelezwa. "Suala la mabadiliko ya posho za vikao vya Bunge lilijitokeza katika Mkutano wa Wabunge, tarehe 8 Novemba, 2011 walipoiomba Serikali iangalie upya suala hilo kwa lengo la kuboresha,” alisema Dk Kashililah katika taarifa hiyo na kuongeza: ”Hadi tunapotoa tangazo hili (jana), Serikali haijatoa taarifa iwapo posho hiyo imeongezeka kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000."
Dk Kashililah aliendelea kueleza "Kwa mujibu wa Waraka wa Rais kuhusu Masharti ya Mbunge uliotolewa tarehe 25 Oktoba,2010, wenye Kumbukumbu namba CAB111/338/01/83 na kusainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, pamoja na stahili zingine, Mbunge anastahili kulipwa posho ya kikao ambayo ni sawa na Sh70,000 kwa kila kikao na masharti hayo hayajafanyiwa marekebisho wala kufutwa."
"Kwa hiyo, taarifa hiyo iliyotolewa siyo sahihi, lakini endapo itatokea, mwenye mamlaka ya kupitisha kiwango kipya cha posho za vikao vya Bunge, itakuwa ni uamuzi kama uamuzi mwingine anaoutoa wa kuwaongezea watumishi wa umma mishahara, posho, marupurupu na mafao mengine."
Baada ya taarifa hiyo kuripotiwa Novemba 28 mwaka huu, wasomi, wanaharakati, wanasiasa na wabunge walitofautiana kwa kupinga na kukubali. Baadhi ya wabunge waliopinga nyongeza hiyo ni Januari Makamba wa jimbo la Bumbuli,mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe na Mbunge wa Hai Freeman Mbowe.
Mbowe alisema walivyokuwa wakipinga posho hizo wakati zilivyokuwa Sh70,000 waandishi wa habari walichukua suala hilo kama ajenda ya Chadema, hivyo kupandishwa kwa posho hizo ni matokeo ya watu kuwapuuza walivyokuwa wakizipinga.
“Msimamo wetu sisi tulishautoa tangu wakati posho zikiwa Sh70,000 wakati sisi tukipinga hizi posho waandishi wa habari na Watanzania mlichukulia suala hili kama ajenda ya Chadema, sisi wenyewe tupo wachache bungeni, tulichotaka ni kuonyesha jinsi fedha za Watanzania zinavyotumika vibaya,” alisema na kuongeza:
“Achilia mbali hizo 200,000 za wabunge kuna watu huko serikalini wanalipwa mpaka Sh400,000 au Sh1 milioni kwa siku nyie ulizeni.”
Makamba ashutushwa Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, alieleza kushangazwa na ongezeko hilo la ghafla akisema kamwe wabunge wasifikiri kuwa wanaweza kumaliza matatizo yao au ya wapigakura wao kwa fedha ya posho.
“Kwenye jamii lazima kuwe na usawa, kama watu tupo kwenye hali mbaya (ugumu wa maisha) lazima wote tuenende sawa. Wabunge kuongezewa posho kwa asilimia 185 siyo sawa kabisa, tunajiweka mbali na wananchi na wanatuona tunafaidika sana wakati wao wanateseka kwa ugumu wa maisha,” alisema Makamba. Alisema kuwa, kutokana na msimamo wake huo, Juni mwaka huu alikataa posho iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini baada ya kuhudhuria semina iliyoandaliwa na wizara hiyo. “Tulikaa kwenye semina kwa saa mbili, tunamaliza naletewa karatasi nisaini posho ya Sh280,000 nilikataa.
Nilikataa kwa sababu nilitambua kuwa ile ni kazi yangu kama mbunge, sasa unanilipa hela ya kazi gani?” alihoji Makamba. Zitto adai ni usaliti Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, alisema kuwa amestushwa na taarifa za kupandishwa kwa posho za vikao kwa wabunge huku wananchi wakiugulia ugumu wa maisha na kusema kuwa ipo siku Watanzania watawapiga mawe kwa usaliti huo.
“Nimeshtushwa zaidi kwamba posho hizi zimeanza kulipwa katika mkutano wa Bunge uliopita kabla hata Rais hajaamua, maana maslahi yote ya wabunge huamuliwa na Rais baada ya kupokea mapendekezo ya Bunge kupitia Tume ya Bunge,” alisema Zitto.
Aliwata wabunge wote kutambua kwamba, kuamua kujipandishia posho bila kuzingatia hali ya maisha ya mwananchi wa kawaida ni usaliti usio na mfano. “Mbunge yeyote ambaye anabariki jambo hili labda anaishi hewani, haoni taabu za wananchi au ni mwizi tu na anaona ubunge ni kama nafasi ya kujitajirisha binafsi,” alisema Zitto.
Wakati wabunge hao wakipinga John Shibuda wa Maswa Magharibi na mbunge wa Ludewa Deo Filikunjombe walizikubali wakisema ni sahihi. Filikunjombe alisema kuongezeka kwa posho hizo kunatokana na wabunge kuwa wanalipwa mishahara midogo kulingana na kazi wanayofanya.
“Ninachosema mimi, siyo wabunge peke yao, lakini watumishi wote wa umma wanalipwa mishahara midogo sana mimi binafsi sitegemei posho za Bunge, kabla ya kuingia bungeni nilikuwa nimefanya kazi kwa miaka 14 na nilikuwa napata mshahara mzuri tu,” alisema Filikunjombe. Shibuda adai posho muhimu Mbunge wa Maswa Mashariki (Chadema), John Shibuda alisema suala la wabunge kuongezewa posho halina ubaya wowote kwa kuwa litawafanya wasiwe ombaomba.
“Umefikia wakati Waafrika tulinde fedheha kwa viongozi wetu ili wasiwe ombaomba. Viongozi wakilipwa vizuri wataweza kuitumikia nchi na jamii inayowazunguka, ipasavyo. Kutokulipwa vizuri ndio mwanzo wa viongozi kusaini mikataba mibovu,” alisema Shibuda.
Tucta wawaka
Kwa upande wake Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), kitendo cha wabunge hao kujiongezea posho ni ishara ya kushindwa kutetea maslahi ya wananchi wao waliowapeleka bungeni. “Tucta inalaani kitendo cha wabunge kujiongezea posho kubwa kama hizo huku wakijua kuwa wananchi waliowachagua wanawategemea wao, hasa katika kipindi hiki kigumu cha maisha.
Jambo hilo linaonyesha wazi kuwa hawako kwa ajili ya kutetea maslahi ya wananchi, bali kujinufaisha wenyewe,”alisema Nicolaus Mgaya. Mwisho
No comments:
Post a Comment