Na Mwandishi Wetu,Songea
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linamsaka Omary Almasi Mkazi wa Kijiji cha Pacha nne kilichopo katika Kata ya Nakapanya Wilayani Tunduru kwa tuhuma za kumuua mke wake wakiwa shambani kisha kumtundika juu ya mti akisingizia kuwa mkewe amejinyonga.
Habari zilizopatikana jana mjini hapa ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael kamuhanda zimesema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 1 mwaka huu majira ya saa 8.10 mchana huko katika Kijiji cha Pacha nne.
Kamuhanda amemtaja mwanamke aliyeuawa na mume wake kuwa ni Somoe Mastawi (48) Mkazi wa Kijiji cha Pacha nne Wilayani Tunduru.
Amefafanua kuwa inadaiwa siku hiyo kabla ya tukio hilo kutokea Omary na mke wake Somoe waliondoka nyumbani kwao na kuelekea shambani kulima shamba la Mahindi na baadae majira ya saa nane na dakika kumi katika hali ambayo siyo ya kawaida Somoe alianza kupata kipigo kutoka kwa mume wake na kumsababishia kifo.
Amesema kuwa mwanamke huyo Somoe aliuwawa na mume wake wakiwa Shambani na baada ya kumfanyia kitendo hicho cha kinyama mke wake alichukua kamba na kumfunga shingoni kisha alimtundika juu ya mti mrefu kwa kusingizia kuwa mwanamke huyo amejinyonga.
Kamanda Kamuhanda ameeleza zaidi kuwa Omary baada ya kugundua kuwa watu wameshafahamu kuwa kitendo hicho cha kinyama amekifanya alikimbia na kutokomea kusikojulikana na kwamba Polisi bado wanachunguza chanzo cha tukio hilo huku wakiendelea kumsaka mtuhumiwa.
No comments:
Post a Comment