TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Sunday, November 20, 2011

Bunge:Luhanjo, Jairo Washtakiwe

KAMATI teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni, imewasilisha taarifa yake huku ikimkangaa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa, David Jairo na Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo.Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Injinia Ramo Makani, aliliambia Bunge kuwa wengine wanaopaswa kuwajibishwa ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na, Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, Ludovick Uttoh .
Makani alisema baada ya kufanya uchunguzi wake uliowezesha kuwahoji watu 146, imebainika kuwa utaratibu uliotumiwa na Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kutoka katika taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kusaidia upitishaji wa bajeti bungeni, haukuwa wa kawaida na kwamba ulikiuka taratibu na sheria za fedha.
“Fedha zilizokusanywa zilikuwa kwa matumizi ambayo yasingehitaji uchangishaji kwa sababu yangeweza kugharamiwa na kasma zilizopo za wizara,” alisema Makani na kuongeza:
“Uchangishaji huo ulisababisha taasisi hizo kubebeshwa mzigo kwa kuwa hazina kasma mahususi kwa ajili ya kuchangia wizara kwa ajili ya maandalizi ya uwasilishaji wa bajeti bungeni”.
Alisema utafiti ulibaini kwamba Jairo akiwa Katibu Mkuu aliomba fedha kiasi cha Sh180 milioni kutoka taasisi nne ambazo ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lililoombwa Sh40 milioni, Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) Sh40 milioni, Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Sh50 milioni na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) Sh50 milioni.
Hata hivyo, kiasi kilichochangwa ni Sh140 milioni tu kutoka Tanesco, REA na TPDC wakati Ewura waligharamia chakula cha mchaka wa siku tatu pamoja na tafrija iliyokuwa imepangwa kufanyika baada ya kupitishwa kwa bajeti ambayo iliwagharimu Sh9.7 milioni.
Makani aliongeza kuwa uchunguzi zaidi ulibaini kuwa mbali na fedha hizo, kulikuwa na kiasi kingine cha Sh428.8 milioni kilichotoka katika Idara mbili za Wizara hiyo ambazo ni Idara ya Uhasibu Sh150.7milioni na Idara ya Sera na Mipango iliyotoa kiasi cha Sh278 milioni kwa ajili ya kusaidi upitishaji wa bajeti.
Alisema fedha zote hizo jumla yake ikiwa Sh568.8 milioni, ziliingizwa kwenye akaunti ya taasisi ya GST iliyopo mjini Dodoma lakini akasema kati ya hizo, Sh150.7 milioni zilikuwa kwa ajili ya gharama za vikao na semina na kiasi kilichokuwa mahususi kwa ajili ya uwasilishaji wa bajeti bungeni kilikuwa ni Sh418.8 milioni.
Makani alibainisha kuwa maelezo waliyopewa na Wizara husika, walifikia uamuzi wa kuomba fedha hizo kutokana na fungu ambalo hutumika kwa ajili ya shughuli za bajeti kubakiwa na Sh35 milioni tu kati ya Sh207 milioni zilizokuwa zikihitajika.
Hata hivyo, alisema Wizara haikuzingatia kanuni husika za fedha katika kuomba fedha hizo, na kwamba Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo alipohojiwa na kamati hiyo, alisema utaratibu uliotumiwa kwamba si halali.
“Sababu zilizoifanya Wizara kuchangisha fedha haziwezi kutiliwa maanani kwa sababu hadi kufikia Juni 25, 2011 Wizara ya Nishati na Madini ilikwishakupata mahitaji yote ya fedha za uwasilishaji wa bajeti baada ya kupokea Sh171.5 milioni za matumizi mengineyo (OC) kutoka hazina,” alisema Makani.
Kughushi nyaraka
Kamati Teule ya Bunge pia ilibaini kwamba kulikuwa na vitendo vya kughushi na udanganyifu katika hesabu za gharama za uendeshaji wa semina ya wabunge ya Juni 26, 2011 ambayo iliendeshwa na Wizara ya Nishati na Madini.
Kamati hiyo ilibaini kuwa ili kufanikisha semina hiyo, Jairo aliziandikia tena taasisi nne ambazo ni REA, Ewura, TPDC na Tanesco kutoa Sh22 milioni kila moja na fedha zote zilikusanywa na kufikia kiasi cha Sh88 milioni, fedha ambazo zililipwa kwa mhasibu wa wizara, Hawa Ramadhani.
Alisema kwa mujibu wa barua hiyo, Jairo aliainisha kwamba bajeti ya semina hiyo ni gharama za ukumbi Sh39 milioni na posho kwa wabunge Sh46 milioni, hivyo kufanya mahitaji kuwa Sh85 milioni tofauti na kiasi cha Sh88 milioni kilichochangishwa.
Alisema maelekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Bunge kuhusu malipo hayo ni viongozi wa Bunge kulipwa Sh250,000, Wabunge Sh110,000, Wakuu wa Idara Sh80,000, Maofisa Sh50,000 na Watoa huduma nyingine Sh20,000.
“Kamati Teule ilibaini kwamba baadhi ya viwango vya posho vilikuwa tofauti na maelekezo ya Ofisi ya Bunge. Kwa mfano wakati wabunge walilipwa Sh110,000 kila mmoja, ilionekana kuwa mtumishi wa ngazi ya mhudumu alilipwa Sh120,000, badala ya Sh20,000, wakurugenzi walilipwa Sh180,000 badala ya Sh80,000 na maofisa wengine Sh150,000 badala ya Sh50,000," alisema Makani.
Alisema utata huo uliilazimisha kamati kumhoji Mhasibu aliyelipa posho hizo kutoka Wizarani na sababu za kutofuata mwongozo wa Ofisi za Bunge na kwamba, jibu la mhasibu huyo ni kwamba alipewa maagizo ya mdomo na mmoja wa wakurugenzi kwamba aongeze kiasi cha Sh100,000 kwa malipo wahudumu na maofisa wengine.
Makani alisema hata hivyo walibaini kwamba malipo hayo yalighushiwa kwa kuongeza namba 1, mbele ya Sh20,000, Sh50,000 na Sh80,000 na kuzifanya kuwa Sh120,000, Sh150,000 na Sh180,000 kwa malipo hayo sawiya hali iliyosababisha upotevu wa kiasi cha Sh13.9 milioni.
"Malipo ya nyongeza yaliyoongezwa kwa kila mtumishi ya Sh100,000 si halali bali ni ya kughushi. Kutokana na kughushi huko jumla ya kiasi cha Sh39 milioni ambazo ni asilimia 15 ya jumla ya fedha zilizokusanywa (Sh88 milioni) ni malipo hewa," alisema.
Alisema kiasi cha Sh39milioni zilizotengwa kwa ajili ya malipo ya ukumbi pia ni dhahiri hayakutumika, kwani ukumbi uliotumika ni wa Bunge (Pius Msekwa) ambao ni wa bure kwani hauna malipo na kwamba watumishi wengine wanaotajwa kulipwa hawakuwapo Dodoma.
Kamati Teule ilibaini kwamba Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa na watumishi 243 wakati wa Bunge la Bajeti mjini Dodoma, hivyo kuitaka Serikali kutoka mwongozo wa idadi inayostahili kwa wizara wakati wa bajeti.
Ngeleja na Luhanjo
Kamati hiyo ilisema Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa Waziri Ngeleja kwa kuzingatia mwongozo wa wa Baraza la Mawaziri ambao unamtaja kuwa ndiye msimamizi mkuu wa Wizara na kwamba suala la uchangishaji wa fedha halikupaswa kufanyika bila yeye kujua.
Makani alisema licha ya kutokuwa na uthibitisho moja kwa moja uhusika wa Waziri au Naibu wake katika uchagishaji uliofanywa na Katibu Mkuu, lakini hilo halimwondoi Waziri katika nafasi ya kuwajibika akiwa msimamizi mkuu wa Wizara.
Kutokana na hali hiyo, Kamati hiyo imekosoa kanuni na taratibu za utendaji wa Wizara, ambazo ilisema zinatoa mamlaka makubwa kwa Makatibu Wakuu wa Wizara ambao huruhusiwa kufanya uamuzi mkubwa kuhusu masuala ya fedha bila kumshirikisha waziri husika.
Kwa upande wake, Luhanjo anatakiwa kuwajibika kwa kile Kamati ilichosema kuwa ni kumsafisha Jairo kwa kuficha ukweli wa Taarifa ya Ukaguzi Maalumu uliofanywa na CAG mara baada ya kutolewa kwa tuhuma hizo bungeni.



Makani alisema Luhanjo katika uamuzi wake ambao aliutoa mbele ya vyombo vya habari Agosti 23, 2001 hakuzingatia taarifa nzima ya CAG na badala yake alizingatia sehemu tu ya taarifa hiyo akilenga kumsadia Jairo kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe.
Kadhalika taarifa hiyo ya Kamati Teule ya Bunge inabainisha kuwa, Luhanjo alikosea kutoa taarifa ya uchunguzi wake wa awali kwenye vyombo vya habari pasipokuwasiliana na Waziri Mkuu ambaye ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni na kwamba kwa kufanya hivyo alimfedhehesha kiongozi huyo.
“Kitendo hiki hakikumtendea haki kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, kwa kuwa alikuwa ametoa kauli bungeni kuwa atalifikisha suala hili kwa mamlaka za juu na Bunge lilikuwa bado linasubiri majibu yake,” alisema.
Alisema kauli ya Luhanjo kwamba Jairo angeweza kwenda katika vyombo vingine vya sheria kushtaki au kudai haki zaidi ni dhahiri kwamba alikuwa akishawishi kuvunjwa kwa Ibara ya 100 ya Katiba ya nchi hivyo kuingilia haki na madaraka ya Bunge.
Uttoh na Jairo
Makani alisema: “Kamati imesikitishwa sana na jinsi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alivyoshindwa kutekeleza wajibu wake kikamilifu, hususan katika kutoa ushauri na hitimisho katika ripoti yake na jinsi alivyotoa taarifa yake kwenye vyombo vya habari”.
“Kwa kufanya hivyo ameshindwa kulisaidia Bunge na Umma kwa ujumla, badala yake amekuwa sehemu ya kuficha maovu. Hivyo Kamati Teule inapendekeza Serikali ichukue hatua zinazofaa kwa CAG kwa upotoshaji huo,”alisema Makani.
Alisema kasoro ya taarifa ya CAG kwa vyombo vya habari, ambayo haikujibu hadidu zote za rejea alizopewa na badala yake alijikita katika hoja iliyokuwa imetolewa Bungeni kuhusu idadi ya taasisi zilizochangishwa na kiasi cha fedha Sh1 bilioni kilichokuwa kimedaiwa kukusanya.
“Hatua hii ilikuwa ni upotoshaji mkubwa kwani taarifa nzima kwa ujumla wake ilikuwa na maudhui ambayo yangeweza kuonyesha makosa ya kinidhamu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,”alisema Makani.
Kuhusu Jairo, Makani alisema Katibu Mkuu huyo ambaye hivi sasa amesimamishwa, anapaswa kuchukuliwa hatua kwa matumuzi mabaya ya madaraka kwa kukusanya na kutumia fedha za umma na kuruhusu matumizi mbaya ya fedha za umma.
“Vilevile Serikali iwachukulie hatua za kinidhamu, kwa mujibu wa sheria watumishi wote wa Wizara ya Nishati na Madini waliotajwa kwenye taarifa hii kushiriki kwa namna moja au nyingine katika uchangishaji na matumizi ya fedha hizi za umma,”aliongeza mwenyekiti huyo wa Kamati Teule.
Miongoni mwa watumishi waliotajwa kwenye taarifa hiyo ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara hiyo ambaye alitoa ushauri usiofaa na wa upotoshaji wa kwa Katibu Mkuu kuhusu kuchangisha fedha huku akijua kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Michango ya wabunge

Wabunge wa CCM na wale wa upinzani,jana waling'aka wakitaka Serikali ichukue hatua kali dhidi ya waliotajwa katika taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Jairo kuchangisha fedha isivyo halali.
Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema ubadhirifu huo ni matokeo ya mfumo mbovu wa utawala ambao unawalinda wezi wa mali ya umma pia kuwepo kwa mfumo wa malipo ya posho ambayo yanatoa mwanya kwa watendaji serikalini kufanya ubadhirifu.
Mbunge wa Simanjiro (CCM),Christopher Ole Sendeka alisema Katibu Mkuu Kiongozi, Luhanjo na Jairo mbali na kuchukuliwa hatua za kinidhamu, wanastahili kufikishwa katika vyombo vya sheria ili washtakiwe.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR Mageuzi), Mosses Machali yeye alisema lazima Serikali ichukue hatua kali kwa watendaji waliohusika na kwamba wasipofanya hivyo.
Machali aliwataka Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima wajiuzulu ili kulinda heshima yao, hoja ambayo pia ilitolewa na Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli na Ezekia Wenje ambaye ni Mbunge wa Nyamagana (Chadema).
Bunge lilipitisha maazimio ya Kamati Teule ambayo Serikali kupitika kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe ilisema itayafanyia kazi mapema iwezekanavyo na kurejesha taarifa bungeni katika mkutano ujao wa sita.

No comments: