WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda jana alikuwa miongoni mwa viongozi mbalimbali wa kitaifa waliofika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kumjulia hali, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe muda mfupi kabla ya kupelekwa India kwa matibabu zaidi.Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema, anakuwa kiongozi wa nne kupelekwa India kwa matibabu katika kipindi kisichozidi miezi mitatu, akitanguliwa na mawaziri wawili na naibu waziri mmoja. Hao ni Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe.
Mbali ya Pinda, viongozi wengine waliofika kumjulia hali mbunge huyo ambaye alikuwa amelazwa katika chumba za uangalizi maalumu (ICU) ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, Waziri Mkuu Mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim na Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed.
Katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, viongozi kadhaa wa Serikali wakiwamo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira walimjulia hali na kumtakia safari njema.
Baada ya kumwona, Pinda hakuwa tayari kuzungumza lolote juu ya afya ya Zitto ambaye pia Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na badala yake kuwataka waandishi wa habari waliokuwapo Muhimbili kuzungumza na daktari aliyekuwa akimtibu.
Daktari wa Mbunge huyo, Profesa Victor Mwafongo alisema: “Mgonjwa anaendelea vizuri leo (jana) zaidi ya juzi. Hakupelekwa ICU kwa sababu alikuwa mahututi, tulimuweka hapa ili tuweze kuangalia afya yake kwa karibu zaidi.”
Profesa Mwafongo alisema wingi wa watu ndiyo uliwalazimisha kumhamishia ICU ili madaktari wapate fursa ya kumhudumia vizuri.
Alisema mbunge huyo amepelekwa India kwa lengo la kufanyiwa uchunguzi zaidi licha ya wao kubaini kuwapo kwa vijidudu 150 vya malaria.
“Vipimo vinatofautiana, sisi tumempima, lakini pia wenzetu ni wataalamu zaidi, hivyo tunaamini kuwa kupelekwa huko kutasaidia kubaini matatizo yake,” alisema.
Kuhusiana vijidudu 150 vya malaria, Dk Mwafongo alisema ni hali ya kawaida kwa mgonjwa yoyote kukutwa na vidudu hivyo na kwamba inategemea utamaduni wa kuangalia afya yake.
Kauli ya Zitto
Jana asubuhi, Zitto alitembelewa na mwandishi wetu na kueleza kuwa hali yake ilikuwa imeimarika na tatizo la maumivu ya kichwa lililokuwa likimsumbua limepungua kidogo.
“Hali yangu inazidi kuimarika, nimetumia dawa za malaria, lakini bado tatizo la kichwa linanisumbua kidogo,” alisema Zitto.
Zitto aliwataka Watanzania kuondoa hofu na badala yake wamuombee kwa Mungu apone haraka ili aweze kushiriki katika Mkutano wa 10 wa Bunge.“Naendelea vyema, naomba Watanzania waelewe hivyo, waondoe wasiwasi na uvumi unaoenezwa,” alisema Zitto.
Alisema tangu aanze kupata matibabu Muhimbili, amemudu kula chakula kama kawaida na hali ya uchovu imepungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, alisema: “Ninakwenda India kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwani kichwa kinauma,” alisema.
Udhibiti Muhimbili
Kulikuwa na udhibiti mkubwa wa watu kuingia katika wodi alikokuwa amelazwa mbunge huyo kijana kutoka na kile kilichoelezwa kuwa ni kumpa fursa ya kupumzika kutokana na maradhi aliyonayo.
Msemaji wa Hospitali ya Muhimbili, Jezza Waziri alisema Spika wa Bunge, Anna Makinda alitoa maagizo ya kutoruhusiwa kwa mtu yoyote kuingia katika chumba alicholazwa Zitto isipokuwa kwa utaratibu maalumu.
“Spika ameacha maagizo hayo kwamba taarifa za hali ya Zitto zitatolewa na Profesa Mwafongo, ila kwa ufupi Zitto anaendelea vizuri,” alisema Jezza.
Hata alipokuwa akiondolewa hospitalini hapo kwenda uwanja wa ndege, kulitumika udhibiti wa aina yake hasa wa kukutana na kalamu na kamera za waandishi wa habari. Baada ya matayarisho yote ya safari kukamilika, waandishi wote waliokuwapo Muhimbili waliitwa kuzungumza na kaka yake Zitto, Salum kuhusu taratibu za safari hiyo.
Wakati akifanya kazi hiyo pamoja na kujibu maswali kadhaa, muda huo ulitumika vyema kumtoa wodini na kumpakia kwenye gari na kuondoka.
Safari ya India
Kutoka Muhimbili, Zitto alikuwa katika gari la kawaida lililosindikizwa na mengine mawili ambayo kwa pamoja, yalitanguliwa na pikipiki ya polisi. Msafara huo ulifika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere saa 8.55 mchana.
Baada ya kuwasili uwanjani hapo, Zitto aliteremka katika gari mojawapo lililokuwa katikati ya yale mawili na kisha kutembea mwenyewe hadi katika chumba cha Watu Mashuhuri (VIP). Lakini muda wote huo alikuwa amezungukwa na watu waliodhaniwa kuwa ni maofisa wa usalama.
Baadaye ilibainika kwamba katika msafara huo alikuwapo pia Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na watu wengine waliotajwa kuwa ni ndugu zake.
Waandishi wa habari waliokuwa uwanjani hapo waliondolewa na kupelekwa mbali na aliposhukia mbunge huyo na hata baada ya kuingia katika chumba cha VIP hawakuruhusiwa kusogea karibu na eneo hilo.
Zitto aliondoka jana mchana akiwa na kaka yake, Salum Kabwe na mmoja wa wauguzi wa Muhimbili ambaye jina lake halikufahamika mara moja.
Dk Slaa anena
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa ameipongeza Ofisi ya Bunge kwa jinsi ilivyojitoa kushughulikia tatizo la kiongozi huyo.
“Ninatoa shukrani kwa Ofisi ya Bunge kwa namna inavyowashughulikia viongozi, wamekuwa bega kwa bega tangu alipougua na kulazwa katika Hosptali ya Aga Khan na Hospitali ya Muhimbili na ndiyo wanaoratibu mipango ya kumsafirisha kwenda India kwa matibabu” alisema Dk Slaa.
No comments:
Post a Comment