Rais Jakaya Mrisho Kikwete
RAIS Jakaya Kikwete ametaka marekebisho yanayofanywa katika Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma, yatumike pia kuwabana matajiri wasio watumishi wa umma ili kujua kama mali walizo nazo wamezipata kihalali au la.
Akizungumza katika hafla fupi ya kufunga mafunzo ya upelelezi na uchunguzi kwa maofisa 50 wa sekretarieti hiyo iliyofanyika katika Chuo cha Maofisa wa Polisi Kidatu, Morogoro jana alisema hatua hiyo itawezesha watu binafsi kuchunguzwa.
Aliitaka Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma kuingiza kipengele kitakachoipa nguvu kuchunguza mali za watu binafsi wakiwamo wafanyabiashara katika sheria inayofanyiwa mapitio.
Alisema sheria ya sasa inawabana watendaji wa umma pekee, huku watu binafsi waliojilimbikizia mali wakibaki huru.
“Wako watu binafsi waliojilimbikizia mali pengine wamezipata kwa kuuza dawa za kulevya au njia nyingine zisizo halali, watu hawa pia wafikie mahali pa kuchunguzwa ili waeleze walikozipata mali hizo,” alisema Kikwete.
Alisema wakati wa uhuru kipindi cha utawala wa chama kimoja cha siasa, maadili yaliwakataza watumishi wa umma kumiliki mali, kutumia madaraka vibaya, kujipatia mali na kupata mali kwa njia ya rushwa, lakini akasema kubadilika kwa mfumo wa siasa kutoka katika Azimio la Arusha na sasa mfumo wa soko huru kumetoa ruhusa kwa watu kumiliki mali.
“Hivyo kupitia mfumo huo, watu wote wakiwamo watumishi wa umma wameweza kumiliki mali, lakini tunachosema si kumiliki mali, hoja ni umezipataje mali hizo?”
Rais Kikwete alisema kazi ya Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma ni kuwachunguza watumishi wote wa umma kwa kuwataka kujaza fomu za kutaja mali zao na jinsi walivyozipata na kusisitiza kuwa sekretarieti hiyo imeamuriwa kuanza kufuatilia ukweli wa kilichojazwa katika fomu hizo.
Rais alisema bado kuna watumishi wadanganyifu ambao hawatoi taarifa sahihi hivyo ni lazima kufuatiliwa.
Alisema japokuwa urejeshaji wa fomu za matamko ya watumishi wa umma umeonyesha kuongezeka kutoka watumishi 6,007 sawa na asilimia 76.8 hadi kufikia watumishi 8,465 sawa na asilimia 94 lakini kiwango hicho hakitoshi inapaswa kufikia asilimia 100.
Ili kufikia lengo hilo, Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma imetakiwa kuwashirikisha wananchi katika kutambua mali za viongozi na jinsi walivyozipata.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Baraza la Maadili ya Umma, Jaji mstaafu Damian Lubuva alimwomba Rais Kikwete kuwa mkali na kuwachukulia hatua watumishi wa umma wanaobainika kuvunja maadili ili kujenga imani na baraza hilo kwa wananchi.
Mwaka jana, Baraza hilo lilipokea malalamiko 41 na kati ya hayo, 24 yalibainika kuwa ya ukweli na wahusika walichukuliwa hatua za kinidhamu.
No comments:
Post a Comment