TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, September 9, 2011

VIGOGO WAUMBUANA KUHUSU MACHINGA COMPLEX

Meya wa Jiji la Dares Salaam, Dk Didas Massaburi

HALI ya mambo katika soko la Machinga Complex bado haijatulia baada ya wafanyabiashara ndogondogo sokoni hapo kuipa Serikali siku 14 iwe imewatatulia kero zinazowakabili katika soko.Moja ya kero wanayotaka itatuliwe ni kufunguliwa kwa vizimba vilivyofungwa kwa makufuli.

Machinga complex ni soko ambalo limeibua mvutano mkubwa baada ya Meya wa Jiji la Dares Salaam, Dk Didas Massaburi kutuhumu bodi inayoongozwa na mbunge Mussa Azzan Zungu wa Ilala, kwamba imefanya ufisadi kwa kujenga vizimba hivyo ambavyo alivifananisha na vile vya kufugia simba licha ya kutumika Sh1.2 bilioni katika ujenzi.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa wafanyabiashara wote wa jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Soko la Machinga Compex, Abubakar Rakesh alisema Serikali ihakikishe ndani ya siku 14 menejimenti ya uvunjaji wa makufuli inatekeleza majukumu kwa kuvunja makufuli yote katika vizimba vilivyofungwa ambavyo havifanyi kazi.

Rakesh alisema wafanyabiashara wa soko hilo hawafanyi biashara kutokana na vizimba vingi kufungwa na makufuli
Alisema vizimba vilivyofungwa vinatakiwa vifunguliwe ili wafanyabiashara wenye sifa waweze kuingia katika vizimba hivyo kufanya biashara.“Kwa umoja wetu tunaitaka Serikali ndani ya siku 14 iwe imeshavunja makufuli ya vizimba ambavyo havifanyi kazi ili waweze kuingia wafanyabiashara wenye sifa waweze kufanya biashara kwenye soko hili”

“Inabidi tufanye mageuzi kutetea njaa tuliokuwa nao hatufanyi biashara yeyote zaidi ya kuingiza hasara kwa siku unaposhinda unaumia Sh600 kwa kulipia choo, chakula cha kununua Sh1500 na bado nauli ya daladala haujalipia kwa siku unatumia zaidi ya Sh3,000 hivyo hatuhitaji umaarufu wa wanasiasa tunataka utendaji ufanyike”, alisema Rakesh.

Pia alisema soko hilo halijawahi kutangazwa na halijulikani kama kuna soko la wafanyabiashara wadogowadogo hivyo wanaitaka Serikali waanze kulitangaza soko hilo.

“Watu wengi hawalijui hili soko wengi wao wanasema ni jengo la makumbusho hivyo tunahitaji ndani ya wiki mbili waanze kulitangaza ili watu waweze kulifahamu na waweze kufika katika soko letu kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa mbalimbali,” alisema Rakesh.

Alisema soko hilo halijajengwa katika miundombinu mizuri kama kituo cha basi hakuna hiyo wanaitaka Serikali iweke kituo cha mabasi katika soko hilo.Mfanyabiashara wa soko hilo Juma Malecha alisema wanaitaka Serikali iwalipe fidia ya kuwadanganya wenye ulemavu waondoke walikokuwa ili waende kwenye soko ambalo halina biashara.

No comments: