Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja
WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja ameibuka na kuwapa Watanzania matumaini mengine akisema makali ya mgawo wa umeme yatapungua kwa kiasi kikubwa kuanzia wiki ijayo baada ya kuanza kwa uzalishaji wa megawati 235.7.
Ahadi hiyo ya Ngeleja si ya kwanza kwani mapema mwaka huu akiapishwa baada ya kuteuliwa tena kushika wadhifa huo, aliutangazia umma kwamba mgawo wa umeme ungekuwa historia, lakini wiki moja baadaye nchi ilitikiswa na mgawo mkubwa.
Akizungumza jana, Ngeleja alisema megawati hizo zitazalishwa katika mitambo ya Jacobsen, Symbion na Aggreko iliyopo Ubungo, Dar es Salaam, huku akisisitiza kwamba mpaka kufikia Desemba, mwaka huu kutakuwa na uzalishaji wa megawati 572 ambao utamaliza kabisa tatizo la umeme.
Mpango huo wa kuanza uzalishaji uliogawanyika katika vipindi viwili, vya kuanzia Agosti hadi Desemba, mwaka huu na kuanzia Januari mwakani hadi Desemba mwakani, unatarajiwa kutumia jumla ya Sh1.2 trilioni ambazo tayari ziliidhinishwa katika mkutano wa Bunge la Bajeti.
Ngeleja ambaye jana alitembelea miradi hiyo alisema uzalishaji huo ni mwendelezo wa mpango wa Serikali wa kumaliza tatizo la mgawo wa umeme na kusisitiza kwamba kuanzia kesho, megawati zitakazoanza kuzalishwa ni 135.7 kutoka katika mitambo ya Aggreko na Symbion na kwamba uzalishaji huo utaziba pengo la upungufu wa megawati 250 hadi 300 za umeme katika gridi ya taifa.
Julai 18, katika Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, wabunge waliikataa Bajeti iliyowasilishwa awali ya Wizara ya Nishati na Madini kutokana na kutoonyesha mkakati wa kutatua tatizo hilo la nishati ya umeme ndipo baadaye ikaja na mpango huo wa Sh1.2 trilioni.
Mtambo yaanza kazi
Ngeleja alisema uzalishaji wa megawati 100 katika mitambo ya Serikali inayofungwa na Kampuni ya Jacobsen, utakamilika Desemba mwaka huu. Alisema mtambo huo una mashine tatu na kila moja ina uwezo wa kuzalisha megawati 35.“Mtambo huu ilikuwa ukamilike na kuanza kuzalisha umeme Juni, 2012 lakini kutokana na tatizo la mgawo wa umeme utaanza kuzalisha umeme Desemba mwaka huu, ukikamilika utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa kero ya mgawo wa umeme,” alisema Ngeleja.
Alisema mitambo ya Symbion yenye uwezo wa kuzalisha megawati 112 ambayo inatumia gesi na mafuta mepesi, mpaka sasa inazalisha megawati 75 tu.
“Megawati nyingine 35.7 za mtambo wa Symbion zitaanza kuzalishwa kesho (leo) baada ya kuwasili kwa mafuta mepesi.”Msimamizi wa mtambo huo, Moses Mwandenga alisema mtambo huo una uwezo wa kutumia gesi na mafuta mepesi kuzalisha umeme na kwamba kinachosubiriwa ni lita 140,000 za mafuta mepesi tayari kuanza uzalishaji.
“Huu mtambo una uwezo wa kuzalisha megawati 112 ila kwa sasa zinazozalishwa ni 75, mafuta haya ni kwa ajili ya kuzalisha megawati 35.7 kwa kuwa gesi haitoshi kuzalisha megawati zote,” alisema Mwandenga.
Ngeleja alisema kutokana na mitambo ya kuzalisha umeme ya Serikali kutumia gesi itakapokamilika, juhudi za kuleta gesi zinafanyika ikiwa ni pamoja na kujenga bomba kubwa la kusafirishia gesi kutoka Bambabay na ujenzi wake utakamilika mwishoni mwa mwaka 2012.
Alisema mitambo ya Jacobson na Symbion ikianza kuzalisha umeme kwa kutumia gesi itapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uzalishaji na kuongeza kuwa upanuzi wa miundombinu ya Songosongo.Kuhusu mitambo ya Aggreko ambayo inatumia dizeli, Ngeleja alisema: “Itazalisha megawati 100 kwa muda wa mwaka mmoja, itaanza kuzalisha umeme kuanzia kesho.”
Alisema mashine za mtambo huo zipo eneo la Ubungo na Tegeta. Ile ya Ubungo itakuwa ikizalisha megawati 50 na Tegeta pia megawati 50. Waziri huyo mwenye dhamana ya nishati, alisema katika eneo la Ubungo, Aggreko ina jenereta 63 ambazo ni nyingi kuliko makubaliano yao na kusisitiza kuwa hali hiyo inaonyesha jinsi kampuni hiyo ilivyojipanga kuhakikisha kuwa uzalishaji wa umeme haukwami kwa kuharibika kwa jenereta.
Ngeleja alilitaka Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) kutoa taarifa kwa wananchi kila kunapotokea hitilafu za kiufundi... “Hivi sasa kuna mgawo wa umeme lakini pia wakati mgawo ukiendelea huwa zinatokea hitilafu za kiufundi… ni vyema mkawapa taarifa wananchi ili kuepusha mvutano, msipofanya hivyo hawatatuelewa kabisa,” alisema Ngeleja na kuongeza: “Wananchi ni lazima wafahamu ratiba za umeme pamoja na tatizo lolote linalotokea kipindi cha mgawo”.
Katika ziara hiyo, Ngeleja ambaye aliongozana na Kaimu Katibu Mkuu wa wizara yake, Eliakim Maswi na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando.
No comments:
Post a Comment