Mbunge wa Monduli(CCM),Edward Lowassa.
UCHUNGUZI wa Bunge kuhusu ufisadi wa zaidi ya Sh205.9 bilioni unaodaiwa kufanywa kupitia Kampuni ya Meremeta iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), umeingia katika sura mpya baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuhamishia jukumu hilo katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa.
Awali, Spika alikuwa amepeleka suala hilo katika Kamati ya Nishati na Madini ili lifanyiwe kazi na Kamati Ndogo ambayo imepewa kibali cha kufanyia kazi sekta ya gesi hasa nafasi ya Kampuni ya Pan African Energy katika uzalishaji na usambazaji wa gesi nchini.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel zinasema Spika Makinda alibatilisha uamuzi wake wa awali, hivyo kuamua kupeleka suala hilo katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
“Ni kweli suala la Meremeta Spika amelihamishia Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, maana hiyo ndiyo inayohusika na masuala hayo, nadhani watakuwa wameshapewa taarifa," alisema na kuongeza:
“Kamati hiyo ndiyo hasa inayohusika na suala hilo la Meremeta, hivyo baada ya uamuzi wa Spika niliijulisha Idara ya Shughuli za Bunge, pengine watakuwa wameshaitaarifu kamati hiyo, naomba unitafute kuanzia tarehe 9 (Septemba) nitakuwa nimefahamu ‘position’ (nafasi) ya kila kamati iliyopangiwa kazi na Spika.”
Zitto ahofia
Hata hivyo, mwasisi wa hoja hiyo ya kuchunguzwa kwa Meremeta, Zitto Kabwe alisema juzi kuwa ameshtushwa na uamuzi huo wa Spika na kwamba anahofia huenda taarifa hiyo isiwekwe wazi kwa umma.
Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema), ameonyesha hofu hiyo ya kuwapo kwa usiri pengine kutokana na kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwahi kusema bungeni kwamba ni bora asulubiwe kuliko kutoa siri za Meremeta hadharani, kwani kufanya hivyo ni kuanika hadharani siri za JWTZ na Usalama wa Taifa.
Hoja inayotakiwa kufanyiwa kazi na Kamati hiyo inayoongozwa na Lowassa ni kuchunguza uhalali wa malipo ya dola milioni 132 (wastani wa Sh205.9 bilioni kwa viwango cha sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1,560 dhidi ya Dola ya Marekani) ambazo zilitoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwenda Ned Bank ya Afrika Kusini ikiwa ni malipo ya mkopo wa Dola 10 milioni, uliokuwa umechukuliwa na Kampuni ya Meremeta Ltd.
Kumekuwa na mvutano baina ya wabunge tangu enzi za Bunge la Tisa na Serikali kuhusu kufanyika kwa uchunguzi ndani ya Meremeta kwa maelezo kwamba suala hilo linagusa masuala ya usalama wa nchi.
Habari zilizopatikana zinasema hoja hiyo ndiyo iliyosababisha Spika Makinda kuhamishia uchunguzi wake kutoka Kamati ya Nishati na Madini kwenda Kamati inayohusika na masuala ya ulinzi na usalama wa nchi.
Zitto akizungumzia uchunguzi huo, alikiri kupata barua kutoka kwa Spika Makinda kwamba suala hilo limehamishiwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama lakini akasema hofu yake ni iwapo taarifa ya matokeo ya uchunguzi huo “itawekwa wazi kwa Bunge na umma.”
Alisema awali alipongeza uamuzi wa Spika wa suala hilo kufanyiwa kazi na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa sababu alifahamu kwamba mambo yote yatakayobainika yangewekwa wazi, lakini akahofu kwamba uwazi huo hauwezi kuwepo katika Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
“Nasema nimeshutushwa na uamuzi wa Spika kwa sababu awali, suala hili lilikuwa liundiwe Kamati Teule ya Bunge kama nilivyoomba, lakini kwa busara zake, Spika akaamua lipelekwe Kamati ya Nishati na Madini ambako mimi nilidhani alikuwa sahihi sana,” alisema Zitto na kuongeza:
“Lakini katika kamati hii ya masuala ya Ulinzi na Usalama, sidhani kama kutakuwa na uwazi, kwa nini… wewe unafahamu kwamba mambo ya ulinzi na usalama huwa wanasema taarifa zao ni za siri, sidhani hapo kama kutakuwa na uwazi wa kusema kile kilichotokea na fedha za walipa kodi kufujwa kiasi kile.”
Uzoefu wa utendaji wa Kamati za Bunge, unathibitisha kuwapo kwa usiri mkubwa ndani ya Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, ukitiliwa nguvu na nyongeza ya saba katika kanuni za Bunge toleo la 2007 zinazoiweka kamati hiyo kuwa miongoni mwa kamati zinazotakiwa kufanya kazi zake kwa faragha.
Zitto alisema kwa kuzingatia maslahi ya taifa ndani ya suala hilo la Meremeta, ikiwa Kamati iliyopewa jukumu hilo itaamua kuunda kamati ndogo, basi Lowassa anapaswa kuunda timu imara ambayo itafanya kazi yake kwa maslahi ya umma.
“Mimi niko tayari kushirikiana na kamati ya Mheshimiwa Lowassa kwa kuwapa vielelezo vyote nilivyo navyo ambavyo vitawezesha kufanya kazi yao vizuri, nitafanya hivi kwa sababu fedha zilizopotea hapa ni nyingi mno, wakilegea hatutaweza ku -achieve (kufanikisha) kile ambacho tulikusudia,” alisema Zitto.
Kauli ya Lowassa
Kwa upande wake, Lowassa akizungumza kwa simu alisema bado hajapata taarifa rasmi iwapo suala la uchunguzi wa Meremeta limewekwa chini ya kamati anayoiongoza.“Kwa kweli sina taarifa hizo, ujue mimi niliondoka mapema pale Dodoma na hadi naondoka sikuwa nimepewa taarifa hizo, ngoja nitafuatilia kesho (jana) ili nifahamu usahihi wa taarifa hiyo,” alisema Lowassa.
Kwa sababu hiyo, hadi sasa haijafahamika iwapo Kamati hiyo ikishapewa taarifa hizo itaunda kamati ndogo kuchunguza suala hilo au italifanyia kazi ikiwa na wajumbe wake wote.
Kanuni ya 114 fasili ya 18 ya Kanuni za Bunge toleo la 2007 inaruhusu Kamati za Kudumu za Bunge kuunda kamati ndogo, kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli zake kadri itakavyoona inafaa.
“Kamati yoyote inaweza kuunda kamati ndogo kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli zake, kadri itakavyoona inafaa na kila kamati ndogo itapangiwa kazi zake na kamati ya kudumu husika,” inaeleza sehemu ya kanuni hizo.
Chimbuko la Uchunguzi
Zitto alianzisha hoja ya kuchunguzwa kwa Meremeta alipowasilisha barua kwa Katibu wa Bunge akitoa taarifa ya hoja ya kuunda Kamati Teule kwa ajili ya kuchunguza tuhuma za ufisadi kupitia Kampuni hiyo ya uchimbaji wa dhahabu.
Barua hiyo ilitanguliwa na taarifa yake ya mdomo aliyoitoa bungeni Julai 13, 2011 kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge Namba 117 (2)-(a) inayomruhusu kutoa taarifa ya kusudio lake la kuwasilisha hoja ya kutaka Bunge liunde Kamati Teule.
Mbunge huyo alimwandikia Spika Makinda barua kutoa taarifa ya hoja husika Julai 15, mwaka huu akisema: “Kuna haja ya kujua uhalali wa ongezeko la Dola 122milioni zilizoongezeka katika malipo yaliyofanywa."
Historia ya Meremeta
Serikali imekuwa haiko tayari kuzungumzia Maremeta kwa maelezo kwamba ni suala ambalo lina maslahi ya usalama kwa taifa.
Awali, ilisema Meremeta Ltd ni kampuni ya Kitanzania iliyokuwa ikimilikiwa na JWTZ kwa ajili ya mradi wake wa Nyumbu, Mkoa wa Pwani huku taarifa za usajili zilizotolewa na Msajili wa Makampuni wa Uingereza na Wales zikisema kuwa kampuni hiyo iliandikishwa nchini humo mwaka 1997 na baadaye ilifilisiwa hukohuko mwaka 2006.
Taarifa ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ya Mei 31, 2005 inabainisha kwamba Meremeta Ltd, ni tawi la kampuni ya kigeni iliyosajiliwa Tanzania, Oktoba 3, 1997 na kwamba hisa 50 za kampuni hiyo zilikuwa zinamilikiwa na Kampuni ya Triennex (Pty) Ltd. ya Afrika Kusini, wakati hisa 50 zilizobaki zilikuwa zinamilikiwa na Serikali ya Tanzania.
Utata kuhusu umiliki wa Meremeta Ltd unatokana na taarifa ya Brela ambayo pia inazitambua kampuni mbili za Kiingereza, London Law Services Ltd na London Law Secretarial Ltd kuwa wamiliki wa hisa moja kila moja ndani ya Meremeta.
Licha ya Serikali kutokuwa mmiliki pekee wa kampuni hiyo, BoT inadaiwa kuwa ililipa madeni yote ya Meremeta badala ya kusaidiana na na washirika wake ambao kisheria wanaonekana kuwa walikuwa wakimiliki hisa katika kampuni hiyo.
Serikali Tanzania ilikuwa ikimiliki asilimia 50 ya hisa na kwa mujibu wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), uhalali wa malipo hayo ulikuwa na walakini kwani kiutaratibu Nedbank Ltd ilitakiwa iachwe idai fedha zake kutoka kwa mfilisi wa kampuni hiyo sawa na wadeni wengine.
No comments:
Post a Comment