TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, August 5, 2011

Baraza la mawaziri lapigwa kombora

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila


. Kafulila asema limechoka mno
. Ndiyo maana wanachapa usingizi

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, jana aliwabana wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwataka waliondoe baraza lote la mawaziri lilipo kwa sababu limechoka na ni kikwazo cha maendeleo nchini.

Akichangia mjadala wa makadirio ya matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2011/12 jana mchana, Kafulila alisema maendeleo nchini hayawezi kufikiwa kwa sababu baraza la mawaziri lililopo limechoka, na ndiyo maana mawaziri siku hizi bungeni wanachapa tu usingizi.

“Mimi nawaomba wabunge wa CCM kwa maana naona kama kuna upepo unaelekea kubadilika hapa, sisi wa upinzani hatusemi kwamba tuingie madarakani leo asubuhi ama mchana ahaa! Hii serikali ni ya kwenu iondoeni ingizeni kikosi kingine si ya kwenu, mtakavyoamua tu, tuwape wiki moja, mkishindwa kuleta fedha ya kutosha takribani bilioni 470 kwa ajili ya kutengeneza reli, bandari na kuboresha usafiri wa anga baada ya miaka mitano tunawaondoa tuingize wengine,” alisema kisha akaongeza:

“Labda hiki chama hakina maaskari wengine kuchukua nafasi hii, kweli Mheshimiwa Spika kikosi hiki kimechoka ndio maana kila siku unaona magazeti watu wanachapa usingizi, tunazungumza hapa hawatekelezi, lakini zamani walikuwa wanatusikiliza hawatekelezi, hivi sasa wameamua na kulala ni tatizo hawa watu wamechoka.

“Juzi kuna waziri mmoja alikuwa amelala kiasi ambacho anafukuza mbu, ingizeni kikosi kingine ni nyie hawa hawa, sisi tutawaondoa miaka mitano ikimalizika hatuna ugomvi.”

Aliongeza: “Gharama ya kutofanya maamuzi huwa ni kubwa sana kuliko hata maamuzi ya kuiba, waziri anaweza kuamua mimi nipo tu mradi sijaiba kwa hiyo siwezi kufungwa, lakini kwenye dunia ya leo kwa kutofanya maamuzi pekee yake unapaswa kuhojiwa.” “Sio kwamba tutawahoji tu walioiba, lakini hata ambao hawafanyi maamuzi kwa sababu kutofanya maamuzi unaweza kusababisha hasara kubwa sana. Hili shirika la ATC si hoja ya leo, hoja ya Uda (Shirika la Usafiri la Dar es Salaam) si ya leo, lakini hadi watu wapige kelele ndio muamue halafu mnasema ni serikali sikivu?...toeni kikosi hiki chukueni vijana wengine tuwatest (tuwajaribu) na wao, si ni miaka mitano kama mtabadilisha mara saba, mtajua tunataka serikali ambayo inawajibika,” alisema Kafulila.

Alisema hawawezi kukaa na serikali ambayo haiwajibiki na kusisitiza: “Leo kuna wabunge wanasoma barua ya waziri kwenda kwa Waziri Mkuu wala waziri hashtuki, hiyo ni failure of the state (kushindwa kwa serikali). Katika mazingira ya kawaida mtu angeshtuka yaani kuna barua ya maoni ya waziri kwenda kwa Waziri Mkuu imevuja wabunge wanainukuu, waziri hushtuki na Waziri Mkuu unaona ni kawaida tu, duuu! Itakwenda kweli nchi hii! Katika mazingira ya kawaida tungeshasikia saa hizi kwamba nyie mnaonukuu hiyo barua mmeitoa wapi? Naamini kuwa barua hii ni confidential (siri), inatoka kwa waziri inaenda kwa Waziri Mkuu.”

Akizungumzia umuhimu wa reli, Kafulila alisema gharama ya kusafirisha mizigo kwa njia ya barabara ni karibu mara kumi ya gharama za kusafirisha kwa njia ya reli. Alisema: “Sizungumzi hivi kwa msingi wa kusema tuondoe fedha zile za barabara halafu tuzipeleke tena huku hapana ziacheni huko, hii nchi ina pesa, pesa zipo tatizo ni jinsi ya kuzitumia wakati Waziri Mkuu anazungumza kutoa Sh. bilioni 95 mpaka na jasho CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali) anatuambia mwaka uliopita misamaha ya kodi ni Sh. bilioni 680, haieleweki.”

“Haya mambo yanatufanya wengine tusielewe, hawa mawaziri hii cabinet (Baraza la Mawaziri), kuna mamlaka ambayo wananyimwa inawezekana labda tunawalaumu nyie labda hamna mamlaka mengine. Tuelezeni kama kuna matatizo ya madaraka tuambieni kwa sababu uwezo upo, rasilimali taifa hili linazo mnashindwaje kuboresha reli ikawa nafuu zaidi ya kutoa huduma katika nchi?

Mtaongeza ushindani wa biashara na kupunguza nakisi.”

Kwa mujibu wa Kafulila, huduma ya reli ni uzalishaji ambao utawezesha taifa kupata fedha kwa kusafirisha mizigo ya watu kutoka nchi mbalimbali.

Alisema reli na bandari vikifanya kazi kwa pamoja vinaweza kulifanya taifa kunufaika na mapato kutoka nchi mbalimbali za jirani.

Alisema watu hao watalipa fedha za kigeni ambazo zitasaidia kukuza uchumi.

“Hadi najiuliza hii Cabinet Mheshimiwa Spika ina mwaka mmoja inashindwa nini kama kweli wana dhamira ya dhati ya kufanya mambo ambayo yanaonekana? Mi siamini lazima kuna tatizo tu. Mheshimiwa Spika haiwezekani vitu vya namna hii vishindikane leo,” alisema.

Alisema watu wanazungumza kuwa kasungura kadogo ndio maana hakuna ndege, lakini Rwanda ni nchi ndogo ambayo ukubwa wake unafanana na mkoa wa Kagera, lakini wao pamoja na kutokuwa na rasilimali kama Tanzania wana ndege tano.

Alisema Tanzania imejaliwa kuwa na dhahabu, almasi, makaa ya mawe na gesi kwa kiwango kikubwa, lakini wanashindwa kuboresha usafiri wa ndege na reli na kuongeza kuwa lazima kuna tatizo.

“Na haya sizungumzi kama mpinzani, bali nazungumza kwa dhamira ya dhati kabisa hii Cabinet (Baraza la Mawaziri) lina tatizo la kufanya mambo, huwezi kuleta bajeti ya Shilingi bilioni 167 zinapigiwa kelele kidogo, unaongeza Shilingi bilioni 95 halafu unasema serikali hii ni sikivu. Ninavyojua Mheshimiwa Spika serikali sikivu ukisema inasikia, lakini serikali kiziwi watu wakipiga kelele ndio inasikia,” aliongeza.

“Serikali sio sikivu hapa waheshimiwa wabunge tukikomaa bila kujali itikadi zetu tukakomaa tu tukang’ang’ania nendeni wiki moja mje na mpango wa kutanzua mgogoro wa reli ili tuwe na reli ya uhakika mje na fedha za kutanzua tatizo la bandari hawa fedha wanazo nyie tukomae tu wataleta fedha tu.

“Kuna vitu vingi vinapachikwa kwenye bajeti humu na mifumo yetu ya bajeti ilivyo migumu sio rahisi kuona.”

Alisema juzi waliambiwa katika sekta ya ujenzi kuna karibu Sh. bilioni 300 ambazo zinasubiri ikitokea mwekezaji hana uwezo wa kutosha, serikali inaweza kuongeza kidogo na shuguli ikaendelea.

“Wizara nyingine zinakuwa na fedha za namna hiyo, lakini nyingine zinakuwa na nakisi kubwa kiasi hiki (Wizara ya Uchukuzi) tatizo hapa nini? Hapa inaelekea tatizo ni competence (uwezo ) ya waziri, hapa inaonyesha kuwa Waziri Magufuli (Waziri wa Ujenzi), ana uwezo mkubwa wa kudai bajeti yake kuliko waziri wetu (Nundu),” alisema.

Alisema kwa hali ya kawaida bajeti ya wizara hiyo ilitegemewa kuwa na kiasi kikubwa kuliko hata ile ya Wizara ya Ujenzi na kwamba kamwe haiwezekani kuboresha maisha ya Watanzania kama mfumo wa reli ni mbovu. Alisema kwa mikoa ya Kigoma na Tabora bado ni tatizo kubwa kwa kuwa ingawa kuna barabara zinajengwa, lakini haziwezi kuisha hivi sasa.

No comments: