TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Sunday, January 29, 2012

UFISADI KILA MAHALI. TBS WAFUNGUA MATAWI HEWA ULAYA,WAIIBIA SERIKALI MABILIONI YA HELA


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Nchini (TBS), Charles Ekelege

KAMATI ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) imemlipua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Nchini (TBS), Charles Ekelege baada ya kubaini kuwa shirika hilo lina ofisi hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi.

Imesema kutokana na hali hiyo fedha za ukaguzi zinazotolewa na wanunuzi wa magari, zinaishia mikononi wa wajanja huku ikisisitiza kuwa itaanika madudu mengine ya TBS katika kikao cha Bunge kinachoanza wiki ijayo na kwamba hali hiyo ndio chanzo cha kujazana kwa magari mabovu nchini. Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Hesabu za Serikali, (PAC), Makamu Mwenyekiti POAC, Deo Filikunjombe alisema waligundua madudu hayo baada ya kamati yake kutembelea vituo vya ukaguzi wa magari nchini Singapore na mjini Hong Kong, China.

Wakati Filikunjombe akieleza hayo mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Joyce Mapunjo, Ekelege alionekana kuishiwa nguvu na kupata mshangao. Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, John Cheyo alisema a walilazimika kuwaita wajumbe wa POAC katika kikao hicho kwa kuwa suala hilo ni nyeti. “Tulikwenda Hong Kong na Singapore na tumegundua kwamba TBS ni wababaishaji, huwezi kuamini anachokifanya Mkurugenzi (Ekelege) huko nje”,

“Ninasema haya bila woga wowote na hata nikiwekewa sumu, wajumbe wengine wa kamati yangu watasema,” alisema. Alisema walipotembelea Hong Kong, waligundua kuwa ukaguzi wa magari haufanyiki na kwamba fedha zinazotolewa na wanunuzi zinaliwa na wajanja.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa kamati,Ekelege aliwapeleka katika ofisi hewa ambayo baadaye waligundua kuwa haikuwa ya ukaguzi wa magari. “Katibu (Mapunjo) ili ulinde heshima yako usimbebe Ekelege, tumekwenda Hong Kong na akatupeleka katika ofisi feki na tulipombana akasema kuwa aliomba kwa muda kuitumia ofisi hiyo,” alisema Filikunjombe. Alisema kampuni inayotumiwa na TBS kukagua magari nje ya nchi inapasaw ieleweke huku akifafanua kuwa wakati wakiwa Hong Kong, walinunua cheti feki cha TBS mtaani. “Huyu Ekelege si mkweli, ukaguzi wa magari haufanyiki sisi tumekwenda na kujionea wazi, ndio maana magari mengi yakifika hapa yanakuwa mabovu na gharama za usafirishaji na ukaguzi zinakuwa kubwa,” alisema Filikunjombe.

Kwa mujibu wa Filikunjombe baadhi ya watu waliowakuta katika kampuni hizo waliwaeleza kuwa Ekelege amekuwa akiwaeleza kwamba fedha za ukaguzi zinazopatikana wazitumie kununulia vifaa vya magari. Alisema walipokwenda Singapore pia hawakukuta kampuni ya kukagua magari na kwamba walipomuuliza Ekelege akashindwa kuwapeleka zilipo ofisi za ukaguzi wa magari. “Jamani mashirika yetu ya umma yananyonywa na wajanja wachache, fedha zinaliwa na wakati tupo huko tuliomba namba za simu na kupewa za uongo,” alisema Filikunjombe.

Alisema kama Mapunj) anambeba Ekelege, wao kama wabunge hawatakuwa tayari kuvumilia suala hilo huku akisisitiza kuwa wana mengi ya kuzungumza kuhusu mkurugenzi huyo. “Hayo ni machache sana kuna mengi ambayo kamati tumeyagundua katika ziara yetu na tutayaanika hadharani Dodoma,” alisema Filikunjombe.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugora alisema walipokuwa nchini humo alitaka kupigana waziwazi na Ekelege baada ya kugundua jinsi walivyokuwa wakidanganywa kama watoto wadogo. Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ester Bulaya alisema a ripoti ya TBS inaonyesha kuwa ukaguzi wa magari ni Dola150 lakini ofisi hizo za ukaguzi zinataka zilipwe Dola300. “Mimi mwenyewe walitaka kunitapeli nilikuwa nataka kununua gari na wakanieleza niwatumie Dola300 wakati kawaida natakiwa kulipia Dola150, nilipowaeleza wakasema wana mtandao mkubwa na hata niende wapi siwezi kuwakamata,” alisema Bulaya.

Mapema Cheyo aliiponda ripoti ya TBS ya mwaka 2011 na kueleza kuwa ina upungufu mkubwa.
“Ripoti ina upungufu, kwanza haina takwimu zinazoonyesha magari mangapi yalikaguliwa na ukaguzi uliingiza fedha kiasi gani na zilizobaki ni kiasi gani” alisema Cheyo. Alisema licha ya taarifa ya CAG kueleza kuwa zoezi la ukaguzi wa magari halikufanyika ipasavyo, bado ukaguzi wa kucha bandia na nywele uliendelea kufanywa na kampuni hizo hewa.

“Hata vitu vilivyokaguliwa na kuonekana kuwa havifai haijulikani viko wapi, haijulikani kama vimetupwa ama laa, hakuna ushahidi vilikuwa kiasi gani” alisisitiza. Alisema kuwa kutokana na hali hiyo kamati yake haitaipitisha ripoti hiyo huku akimwagiza Mapunjo kuandaa upya ripoti hiyo na kuiwasilisha mbele ya kamati yake kabla ya Februari 2 na iwe imekaguliwa na CAG.

“Hakuna haja ya kuendelea kubishana tunaitaka wizara mpaka kufika Alhamisi ijayo (Februari 2) tupate takwimu zote na ziwe zimekaguliwa na CAG,” alisema Cheyo. Cheyo alimweleza Mapunjo kwamba kabla ya kumalizika kwa kikao cha Bunge mjini Dodoma watakutaka na Waziri wa Viwanda Biashara na Masoko na Kamati ya PAC na POAC ili kulijadili kwa kina suala hilo.

“Pia tutamweleza Spika wa Bunge ili kuona kama suala hili tunaweza kulifikisha bungeni ili wabunge watoe maoni yao,” alisema Cheyo. Ekelege anena Baada ya kikao hicho kumalizika Mwananchi lilimtafuta Ekelege ili ajibu tuhuma hizo ambapo alisema kuwa hawezi kuzungumza lolote huku akitaka atafutwe leo ofisini kwake.

Huku akionekana kuwa na kigugumizi Ekelege alisema,“Kwa leo siwezi kusema lolote kwa kuwa sina data (vielelezo), kesho (leo) njoo ofisini kwangu nitakueleza kila kitu, ila kwa sasa siwezi kusema lolote” alisema Ekelege Kauli ya Wizara Kwa upande wake Mapunjo alisema kuwa hawezi kueleza chochote kwa kuwa hajaipata ripoti ya CAG na kusisitiza kuwa atakapoipata ripoti atatoa ufafanuzi.

No comments: