TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, January 12, 2012

Jaji Shangwa atupiwa tena zigo la CUF
Mbunge wa Wawi kwa tiketi ya CUF, Hamadi Rashid Mohamed (mwenye kaundasuti) na wenzake wakitoka Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, juzi, kuwasilisha kiapo cha mahakama kwa kulalamikia viongozi wa Cuf walikataa oda ya mahakama hiyo iliyozuia kufanyika kwa mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho Januari 4. Kushoto ni Shoka Khamis Juma, mmoja kati ya wanachama wanne wa Cuf walivuliwa uwanachama akiwemo na Hamadi. Picha na Said Powa

JAJI wa Mahakama Kuu, Augustine Shangwa ambaye ndiye aliyetoa amri ya kulitaka Baraza Kuu la CUF kusitisha mchakato wa kuwafukuza uanachama Hamad Rashid na wenzake kumi na moja, amepangwa kusikiliza maombi ya makada hao kupinga uamuzi wa chama hicho kukaidi agizo hilo.

Maombi hayo yaliyowasilishwa juzi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kina Hamad, yataanza kusikilizwa Alhamisi ijayo. Hamad Rashid na wenzake waliwasilisha maombi mahakamani hapo wakiiomba hiyo iwaamuru watendaji wa CUF waitwe kujieleza ni kwa nini wasitiwe hatiani na kufungwa kwa kupuuza amri yake. Pia, waliiomba mahakama ibatilishe uamuzi wa Baraza Kuu la CUF wa kuwafukuza uanachama na itamke kuwa wao bado ni wanachama halali wa chama hicho.

Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Wakili wa walalamikaji, Agustine Kusalika zinasema kuwa maombi hayo yatasikilizwa na Jaji Shangwa ambaye pia ndiye anayesikiliza kesi ya msingi.

Ikiwa mahakama itakubaliana na maombi hayo, itaagiza wadhamini wa chama hicho na wajumbe wa Baraza Kuu waliopitisha uamuzi wa kuwafukuza uanachama Hamad Rashid na wenzake, akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad wapandishwe kizimbani kwa kupuuza amri ya Mahakama.

Januari 4, mwaka huu Jaji Shangwa ililiagiza Baraza Kuu la CUF lisitishe mchakato wa kuwasimamisha au kuwafukuza uanachama Rashid na wenzake wala kuendelea kuwajadili wakati wa mkutano wake uliofanyika siku hiyo huko Zanzibar.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya Hamad Rashid na wenzake kuwasilisha maombi Januari 3, mwaka huu wakiiomba mahakama hiyo iamuru mkutano huo ambao ulikuwa na lengo la kuwafukuza uanachama usitishwe hadi kesi yao ya msingi itakapomalizika. Katika kesi yao hiyo, namba 1 ya mwaka 2012, Hamad Rashid na wenzake wanahoji uhalali wa Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho na uteuzi wa wajumbe wake.

Kamati hiyo ndiyo iliyowahoji wanachama hao waliofukuzwa na kisha kupendekeza kwa Baraza Kuu wafukuzwe uanachama. Wakili Kusalika alisema ingawa Seif ambaye alikuwa ni mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo ni Makamu wa Rais wa Zanzibar, kuna uwezekano wa kumtia hatiani kwa kuwa alikuwa akifanya kazi za chama na si za Serikali.

“Kimsingi sisi tumewalalamikia wadhamini wa chama na wajumbe wa Baraza Kuu kwani ndiyo waliokiuka amri ya Mahakama, sasa wakati wa hearing (usikilizwaji) wa maombi yetu mahakamani ndipo itajulikana ni nani ataitwa mahakamani,” alisema Kusalika. Akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya kuwasilisha maombi hayo, Hamad Rashid alisema CUF wamevunja Katiba ya nchi kwa kuidharau amri ya Mahakama pamoja na Katiba ya chama chao.

Alisema Ibara ya 4 ya katiba ya chama hicho inasema kuwa mahakama ndiyo itakayoamua mambo yote yakiwemo yahusuyo migogoro baina ya wanachama bila kuingiliwa isipokuwa kwa kukata rufaa tu na kwamba Ibara ya 5 inasisitiza kuwa juu ya utawala wa Sheria. Alisema kutokana na chama hicho kukiuka amri halali ya mahakama, yeye bado ni Mbunge halali wa Wawi na kwamba hata kwenye vikao vya kamati za Bunge vitakavyoanza Januari 15 atashiriki.

Alisisitiza kuwa tayari ameshawalisha taarifa na vielelezo kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na kwamba kwa mujibu wa kanuni za Bunge kama jambo liko mahakamani haliwezi kuchukua hatua yoyote hadi mahakama itakapokuwa imetoa uamuzi wake.

No comments: