TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Monday, September 26, 2011

BEI YA PETROL YAZIDI KUPAA

Kituo cha ma futa kikiendelea na kazi ya kuuza mafuta

BAADA ya bei ya petroli kushuka kwa wiki nne mfululizo, leo bei ya bidhaa zinazotokana na nishati hiyo zitapanda na kudumu kwa wiki mbili zijazo.Safari hii petroli katika jiji la Dar es Salaam itauzwa kwa Sh 2,102 kwa lita moja ikilinganishwa na Sh 2,031 kwa bei, iliyoishia jana.

Kupanda na kushuka kwa bei ya nishati hiyo ya mafuta kwa lita, ni sehemu ya utekelezaji wa kanuni ya ukokotoaji inayotumiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Wiki mbili zilizopita, Ewura ilitoa bei elekezi ambazo petroli ilishuka kwa Sh38.03 sawa na asilimia 1.84, dizeli Sh 45.15 sawa na asilimia 2.26 na mafuta ya taa bei ilishuka kwa Sh46.15 sawa na asilimia 2.33.

Hata hivyo, jana Ewura katika bei hizo mpya inayoanza kutumika leo imetangaza kupanda kwa bei ya rejareja ya petroli kwa Sh 70.12 sawa na asilimia 3.57 wakati dizeli imepanda kwa Sh 44.88 sawa na asilimia 2.38 na mafuta ya taa kwa Sh 33.02 sawa na asilimia 1.77.

Mkurugenzi wa Petroli wa Ewura, Mutaekulwa Mutegeki alitangaza bei hiyo jana, huku ikionyesha kuwa kwa Dar es Salaam petroli itauzwa kwa Sh 2,102, mafuta ya taa Sh1,967 na dizeli Sh1,999 kwa bei ya rejareja.

Bei ya rejareja katika miji mingine mikubwa ni Arusha ambako petrol itauzwa Sh2,186, mafuta ya taa Sh2,051 na dizeli Sh2083.

Mbeya, petroli itauzwa Sh2,209 kwa lita moja, mafuta ya taa Sh2,074 na dizeli Sh2,106, wakati Mwanza petroli itauzwa kwa Sh2,251, mafuta ya taa Sh2,116 na dizeli Sh2,149.

Sababu za kupanda
Ewura walisema sababu za kupanda kwa bei hiyo ya mafuta ni kutokana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia.

Ewura katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, ilifafanua kuwa petroli imepanda kwa asilimia 5.16, dizeli 2.98 na mafuta ya taa kwa asilimia 2.35.

Pia Ewura imetangaza sababu nyingine, ni kuendelea kupomoroka kwa shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani kwa kiwango cha asilimia 0.55.

Mkurugenzi huyo wa Petroli alisema, kuporomoka kwa shilingi dhidi ya dola ambayo ni fedha ya kimataifa ya manunuzi kumefanya manunuzi ya ndani nayo kuongezeka.

Mchakato kuanzia Agosti 2
Mchakato wa marekebisho ya bei za mafuta, ulianza Agosti 2, mwaka huu ambapo Ewura ilitangaza kushusha bei ya mafuta ambayo petroli ilishuka kwa Sh202.37 kwa lita ambayo ni sawa na asimilia 9.17, dizeli ilishuka kwa Sh173.49 ambayo ni sawa na asilimia 8.32 na mafuta ya taa yalishuka bei kwa Sh181.37, sawa na asilimia 8.70.

Hata hivyo, uamuzi huo uliibua mvutano kati ya wamiliki wa makampuni ya mafuta na serikali huku wamiliki hao wakitunisha msuli na kugoma kuuza nishati hiyo muhimu.

Lakini, Agosti 10 serikali ilitoa saa 24 kwa kampuni hizo za mafuta kutangaza kwanini yasichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka agizo halali la serikali.

Ewura baadaye ilitoa onyo kwa kampuni zilizogoma ikiwemo Engen, Camel Oil, huku ikimfungulia mashitaka mkurugenzi mkuu wa BP kwa kushindwa kutii amri ya kushusha bei.

Lakini, siku 11 baada ya kushusha bei na nchi kutikiswa na mgomo Ewura ilipandisha tena bei kwa kisingizio cha kuporomoka kwa shilingi na kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia.

Hata hivyo, wiki mbili zilizopita hadi kuishia jana Ewura ilitangaza kushusha bei tena ya mafuta na kutoa ahueni kwa watumiaji nchini.

No comments: