TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, August 26, 2011

ZITTO AILIPUA SERIKALI



SERIKALI na Bunge zimeingia katika mkwaruzano mwingine baada ya Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, kuituhumu Serikali kuwa imemsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika Hodhi (CHC), Mathusela Mbajo, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kuvujisha siri za Serikali kwa Bunge.

Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alitoa tuhuma hizo jana wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2011/2012.Juzi Bunge liliingia katika mvutano na Serikali baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kumrejesha kazini Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo, bila Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kujadiliwa bungeni.

Kabla sakata hilo halijapoa, Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alidai kuwa hatua zilizochukuliwa na serikali dhidi ya Mbajo ni matokeo ya Azimio lililopitishwa na Bunge kuliongezea shirika hilo muda.

"Baada ya kufanya marekebisho hayo, azimio lililopelekwa na Serikali bungeni likiwa na nia ya kuunganisha shirika hilo na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Zitto alisema uamuzi huo wa Bunge haukuwafurahisha baadhi ya watendaji wa Serikali hivyo ikaamuliwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu huyo wa CHC, kwa tuhuma zilizojaa majungu kutoka kwa wanaojiita wafanyakazi wa CHC," alisema Zitto na kuongeza.

"Tuhuma hizo ziliwasilishwa kwangu binafsi na kunakiliwa kwa Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha. Kufuatia maagizo ya Waziri wa Fedha kwa Bodi ya Wakurugenzi wa CHC, Mtanzania huyu akasimamishwa kazi na CAG ameombwa kuchunguza majungu yale kutoka kwa wanaojiita wafanyakazi wa shirika hilo.

"Mheshimiwa Spika, nilikuandikia barua kukuomba hatua mwafaka zichukuliwe, kwani suala hili bado lipo katika mamlaka ya Bunge na kwa mujibu wa Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, Sheria namba 3 ya mwaka 1988, uamuzi huu Waziri wa Fedha ni sawa na kulidharau Bunge"

Waziri kivuli huyo aliongeza: "Barua ya wanaojiita wafanyakazi wa CHC (niliyoandikiwa Juni 24, 2011, siku mbili tangu kupitishwa kwa azimio la Bunge na kuwatuhumu mawaziri kuwa walishawishiwa), Barua ya maelekezo ya Serikali (iliyosainiwa na ndugu Mmbaga, Msaidizi wa Waziri Mkuu ya tarehe 10 Agosti 2011) na barua yangu ya majibu (18 Agosti 2011) niliyowapa, zimewasilishwa mezani kwako kama vithibitisho na kwa hatua zaidi utakazoona inafaa."

Zitto aliliomba Bunge kusimama imara ili kuzuia kuingiliwa kwa mamlaka yake na tawi la utendaji kwa kuwa mijadala ndani ya Bunge inalindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo lisipokuwa makini Bunge litaendelea kudharauliwa hatimaye kushindwa kufanya kazi yake ya kuwawakilisha wananchi, kutunga sheria na kuisimamia Serikali ipasavyo.

"Ninataka maelezo ya kina ya Waziri wa Fedha kwa nini amechukua hatua nilizoeleza hapo wakati akijua jambo hili lipo mezani kwa Spika wa Bunge."

Usimamizi wa mashirika ya Umma
Katika eneo hilo, Zitto aliituhumu Serikali kwa kushindwa kusimamia hisa zake katika makampuni akieleza kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) imekuwa dhaifu mno katika kusimamia mali za umma katika mashirika na kutoa mfano wa hisa za kampuni ya Oryx na Tigo.

"Kampuni ya Oryx ilikuwa inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 50 mpaka mwaka 2004. Mwaka 2004, kupitia ofisi ya TR Serikali iliuza hisa zake ambazo ni asilimia 50 kwa bei ya kutupa kwa thamani ya dola 2.5 milioni. Hivi sasa Oryx ni moja ya kampuni inayofanya vizuri sana katika sekta ya mafuta, lakini hatuna umiliki tena na pesa kiduchu tulizopata zimekwishatumika," alisema Zitto na kuongeza:

"Pia Serikali ilikuwa na hisa katika kampuni ya simu za mkononi ya Mobitel ambayo kwa sasa inajulikana kama “tigo”. Katika hatua ya kushangaza Serikali imeuza hisa zake asilimia 16 kwa thamani ya Dola 1.3 milioni mwaka 2006 na kwa sasa kampuni hiyo ni ya kigeni kwa asilimia mia moja jambo ambalo ni kinyume na sheria."
Zitto alisema kampuni za simu zinatakiwa kumilikiwa na Watanzania si chini ya asilimia 35.

Makusanyo ya kodi
Zitto alisema kambi ya upinzani nasikitishwa na pungufu ya makusanyo madogo ya kodi na kwamba, hali hiyo imetokana na Serikali kushindwa kusikiliza maoni yanayotolewa na kambi hiyo kila mwaka ambayo ni vyanzo mbadala vya kuongeza mapato.

Kuhusu bei ya dhahabu
Zitto alifafanua kwamba bei ya dhahabu katika soko la dunia imeongezeka mara dufu na hadi kufikia Agosti 23, mwaka huu. Kwa mujibu wa mtandao wa gold-alert bei ya dhahabu ilikuwa Dola za Marekani 1,902.61.
Alisema hilo ni ongezeko kubwa na hivyo kuna haja ya kuangalia namna ya kurekebisha kodi kwenye madini hayo ili taifa lifaidike na bidhaa hiyo.

Kutokana na ongezeko hilo la bei, alisema kambi ya upinzani inaitaka Mamlaka ya Mapato nchini(TRA) kuanza mara moja kufanya utafiti wa namna bora ya kutoza kodi ya faida kwenye dhahabu (windfall tax), ili kuongeza mapato ya Serikali kwa sababu wawekezaji wanapata faida mara dufu kwa sasa.

"Matokeo ya tafiti hii yaletwe bungeni kama muswada wa sheria ili kurekebisha sheria za kodi na kutoza aina hii mpya ya kodi," alisema Zitto

Alisema kambi ya upinzani inapendekeza kwa kuwa gharama ya kuzalisha wakia moja ya dhahabu hapa nchini ni wastani wa dola za marekani 650, basi bei ya dhahabu ikiwa ya kati ya dola 1,000 – 1,300, mrabaha uwe mara mbili ya tozo za sasa.

"Kwa mfumo huu, taifa litafaidika na kupanda kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia na pale ambapo bei zitashuka wawekezaji watalipa mrabaha wa kawaida," alifafanua aziri kivuli huyo.

Alisema iwapo mfumo huo wa kodi katika madini ungekuwa unatumika sasa na ambapo bei ya dhahabu imefikia zaidi ya dola 1,900 kwa wakia, na nchi inazalisha takribani tani 60 ya dhahabu kwa mwaka, Serikali ingekusanya takribani Sh450 bilioni kama mrabaha.

"Hii ingetuwezesha hata kutokopa kwa ajili ya umeme wa dharura kama tunavyoelekea kufanya sasa."

No comments: