TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Tuesday, August 9, 2011

Serikali, wauza mafuta sasa wafikia pabaya

MOJA YA VITUO VYA KUUZA MAFUTA VILIVYOGOMA KAMA VINAVYOONEKANA KATIKA PICHA HII
WAKATI mamlaka za Serikali zikianza uchunguzi kuona kama kampuni zinazoagiza mafuta ya jumla zimekiuka Sheria ya Ushindani wa Kibiashara, wamiliki wa vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam wamepuuza onyo la Serikali na kuendelea na mgomo.

Mbali na uchunguzi huo, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), huenda ikawasilisha ombi maalumu kwa Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC), la kufutwa kwa Chama cha Kampuni za Kuuza Mafuta Tanzania (Taomac).

Vurugu katika soko la mafuta zilianza Agosti 4, mwaka huu baada Ewura kushusha bei ya petroli kwa Sh202.37 kwa lita ambayo ni sawa na asimilia 9.17, dizeli kwa Sh173.49 ambayo ni sawa na asilimia 8.32 na mafuta ya taa kwa 181.37, sawa na asilimia 8.70.

Wakati baadhi ya kampuni zikificha bidhaa hiyo, taarifa zinasema zimekuwa zikipanga na kuzungumza kuhusu kufanya mgomo baridi.Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani wa Kibiashara (FCC), Gregory Ndanu aliliambia gazeti hili kwamba tayari wameanza mkakati wa kuchunguza mwenendo mzima wa wafanyabiashara hao.

Ndanu alifafanua uchunguzi wa mwenendo huo umezingatia kwamba baada ya Tanzania kuingia katika mfumo wa soko huria, ni kosa kwa wafanyabiashara kukaa pamoja ili kupanga bei ya soko.

“Katika uchunguzi wetu tukiwatia hatiani kwa kosa hilo, watatozwa faini kwa mujibu wa kifungu cha tisa cha Sheria namba 8 ya mwaka 2003 na kifungu cha 20 cha Sheria za Ewura,” alisema Ndanu.Mkurugenzi huyo alisema Tume yake ipo mbioni kukutana na waandishi wa habari ili kuuarifu umma juu ya mpango wake. Alisema kampuni zitakazotiwa hatiani kila moja itatozwa faini ya asilimia tano hadi 10 ya mapato yake katika mwaka uliopita.

“Katika soko huria bei hazipangwi ili kuruhusu ushindani wa kibiashara na tayari tumepata malalamiko kwamba wauzaji wa jumla ndiyo wanaovunja sheria hiyo."Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu alisema Bodi ya mamlaka hiyo inatarajiwa kufanya kikao Dar es Salaam leo kujadili na kuweka bayana ushahidi kwamba wafanyabiashara hao wamekuwa wakiwasiliana ili kupanga bei ya mafuta sokoni.

“Bodi itafanya kikao kesho (leo) na miongoni mwa mambo ambayo tunatarajia kuyafanya ni kuandaa vielelezo vya uvunjaji sheria vinavyofanywa na wafanyabiashara wa mafuta nchini ili viwasilishwe FCC,” alisema Masebu.

Ingawa Masebu alikataa kuzungumzia juu ya adhabu inayoweza kuwakabili wafanyabiashara hao, mmoja wa maofisa wa Ewura alisema mbali na kutozwa faini, kampuni inaweza kufilisiwa iwapo itaonekana kuonyesha kiburi na tatizo hilo wamekuwa wakilifanya kwa muda mrefu.Ofisa hiyo aliongeza kwamba wataishauri FCC ikifute Taomac, kwa kuwa kimekuwa ni moja ya kichocheo kwa wafanyabiashara hao kugomea mpango wa Serikali wa kupunguza gharama za maisha nchini.

Ufafanuzi wa Taomac
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Toamac, Salum Bisarara alikanusha kuhusu suala la wafanyabiashara hao kupanga bei akisisitiza vikao vya Ewura ndivyo vinavyowakutanisha katika kujadili mipango ya Serikali kwenye uagizaji wa bidhaa hizo.

Aliendelea kulalamikia bei mpya akidai kwamba wakiuza kwa kutumia bei elekezi ziliyotolewa na Ewura, wanapata hasara ya Sh150 mpaka 250 kwa kila lita ya mafuta wanayouza. Alisema jana kuwa sheria inakataza wanachama wa umoja huo kukaa pamoja na kujadili masuala ya bei za mafuta na kwa hivyo isingewezekana kukaa kwani kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Bisarara alisema kufuatia utekelezaji wa bei mpya za mafuta zilizoanza kutumika mwanzoni mwa mwezi huu, kampuni zimekuwa zikiuza kwa bei ya hasara jambo ambalo hata hivyo, lilipokewa kwa mtizamo tofauti kutoka kampuni moja hadi nyingine.

“Baada ya kutangazwa kwa bei mpya, kampuni zilijikuta zikipata hasara ya kati ya Sh150 na 250 kwa kila lita. Baadaye zilikuwa na mkutano na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Ewura kwa ajili ya kujadili suala hili. Katibu Mkuu aliyaomba yaendelee kuuza kwa bei ya hasara wakati suala hilo likitafutiwa ufumbuzi,” alisema.

Bisarara alisema wawakilishi wa kampuni hizo walimwomba Katibu Mkuu awape muda ili waweze kuwasiliana na wakubwa zao kabla ya kutoa jibu la ndiyo au hapana kuhusiana na pendekezo hilo.

“Baada ya hapo kila mwakilishi aliwasiliana na wakuu zake. Mwakilishi wa Engen aliambiwa na wakuu wake anaweza kuuza kwa bei ya hasara kwa saa 24. Lakini baadhi ya vyombo vya habari viliripoti vibaya kuwa aliipa Serikali saa 24 kurekebisha bei jambo ambalo siyo la kweli hata kidogo.”

Alisema kuna tofauti kutoka kwa kampuni moja ya mafuta hadi nyingine na kuongeza kuwa zipo kubwa na ndogo na hata uwezo wao pia unatofautiana na ndiyo sababu kila kampuni ilipokea suala la bei kwa mtazamo wake.

Mwakilishi wa Engen, Seelen Naidoo anayetuhumiwa kuipa Serikali saa 24 iwe imefidia hasara hiyo alisema kilichotokea ni kuwa alipewa ruhusa ya kuuza kwa bei ya hasara kwa saa 24 tu na huo ulikuwa ni msimamo wa kampuni yake akisisitiza haukuwa na uhusiano wowote na kampuni nyingine.

Hata hivyo alisisitiza: “Hasara ya kati ya Sh150 hadi 250 kwa lita siyo ndogo. Wakubwa zangu walisema uwezo wetu wa kuuza kwa hasara ni saa 24 kwa sababu tungeendelea zaidi ya hapo tungeweza kupata hasara kubwa zaidi na hata kulazimika kufunga biashara maana tungekuwa tunakula mtaji.”

Vituo Dar vurugu tupu
Kutokana na idadi kubwa ya wafanyabiashara kusitisha kuuza mafuta, vituo vichache vilivyotii agizo la Serikali jana vilikuwa na misururu mirefu kiasi cha kuweka ‘kanuni’ za uuzaji. Kwa mfano katika Kituo cha Big Bon, Sinza hakuna aliyeruhusiwa kununua mafuta ya Sh 10,000 ili na wengine wapate.

Hali katika kituo hicho ilikuwa tete kwani foleni ilikuwa kubwa na kufanya watumiaji wengine wa njia hiyo kushindwa kupita. Foleni kutoka katika kituo hicho kilichopo Sinza Mori ilifika mpaka Palestina hadi mchana baada ya wahudumu kusitisha uuzaji kutokana na ghasia ambazo zilisababishwa na watu waliokuwa wakilazimisha kununua mafuta kwa kutumia ‘vidumu’.Vituo vingi katika maeneo ya Tabata vilikuwa vikiuza mafuta ya taa na dizeli tu bila ya petroli.

No comments: