TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Tuesday, July 5, 2011

Waziri atajwa kupewa kontena la baiskeli kabla ya uchaguzi


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, ametajwa kupewa kontena la baiskeli za walemavu kupeleka jimboni miezi minane kabla ya uchaguzi mkuu mwaka jana.Akizungumzia utekelezaji dhana ya utawala bora wakati akichangia bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi kwa Ofisi ya Rais (Utumishi, Utawala bora, Uratibu na Uhusiano wa Jamii) bungeni jana, Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mnyaa, alisema kontena hilo alipewa Febuari 2, mwaka jana.

Kwa mujibu wa Mnyaa, kontena hilo ambalo lilitolewa na Asasi isiyo ya kiserikali ya Unit Diversity Foundation (UDF), inaacha maswali mengi katika dhana nzima ya usimamizi na utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Mnyaa alifafanua kwamba, asasi hiyo yenye makao yake makuu Dar es Salaam imekuwa ikitoa misaada ya baiskeli kwa walemavu na kuongeza kuwa, ni asasi isiyofanya biashara, hivyo kuhoji waziri kupewa kontena zima.

Waziri Maige alipopigiwa simu jana ili kupata ufafanuzi wa kitakwimu kujua idadi ya walemavu waliopo jimboni kwake kulinganisha na idadi ya baiskeli kwenye kontena hilo, simu yake ya kiganjani iliita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi (SMS), hakujibu.
Lakini, Mnyaa katika kuweka bayana hilo, alisema hata aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mufundi, mkoani Iringa, hadi Februari mwaka jana naye alipewa kontena kama hilo.

Mbunge huyo alienda mbali kuwa, baadhi ya mawaziri wamekuwa wakitumia ushawishi wao kuomba misaada katika asasi mbalimbali kwa nadharia ya, "Nipe ni kupe."
"Sisi wabunge wa kawaida tukienda kuomba misaada katika mashirika au kampuni mbalimbali hatupewi mikubwa, lakini mawaziri wanakwenda kwa nyadhifa zao na kupewa misaada mikubwa, hii inaondoa dhana nzima ya utawala bora,” alisisitiza.

Hata hivyo, alitetea asasi hiyo akisema inafanya kazi nzuri kusaidia walemavu na kwamba, hivi sasa inakabiliwa na ukosefu wa Sh58.5 milioni kwa ajili ya kutoa makontena mawili ya baiskeli bandarini.

Mnyaa alifafanua kwamba, asasi hiyo ambayo watendaji wake wamepiga kambi Dodoma imeonyesha nia ya kusaidia baiskeli tatu kwa kila mbunge kwa Sh50,000 baada ya kufanikiwa kuondoa kontena hilo.

No comments: