TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Sunday, July 3, 2011

Wahadhiri Ustawi wa Jamii wagoma

Wahadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii jijini Dar es Salaam wamegoma kuingia darasani kufundisha wakiushinikiza uongozi wa chuo o uondoke na bodi yake iundwe upya.

Aidha, wamesema uamuzi huo umefikiwa baada ya wenzao kumi kufukuzwa kazi katika kipindi cha miezi mitatu bila sababu za msingi.

Uamuzi huo wa kutoingia madarasani ulitangazwa jana baada ya kukaa kikao ambacho kiliamua kitakuwa kikifanyika kila siku kuanzia jana hadi madai yao yatakapopata ufumbuzi.

Mwenyekiti wa kikao hicho, Faustine Nzigu, alisema wameamua kutoingia darasani baada ya juzi wenzao saba kupewa barua za kufukuzwa kazi.

Nzigu ambaye aliongoza kikao hicho, alisema sababu zilizotajwa kwenye barua za wenzao waliofukuzwa sio za msingi ndio maana wameamua kutofundisha.

Alisema Februari mwaka huu, walienda ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, kumuelezea malalamiko yao kuwa chuo hicho hakina uongozi na kwamba waliopo wanakaimu nafasi zilizokuwa wazi, lakini aliwaeleza kuwa analifanyika kazi suala hilo na kwamba hadi Machi 2011 litakuwa limeshapatiwa ufumbuzi lakini mpaka sasa hakuna utekelezaji.

“Msimamo tuliofikia leo (jana) hatupo tayari kufanya kazi na uongozi huu ambao hauna vigezo pamoja na bodi inayokiuka taratibu za kumfukuzisha mfanyakazi kazi na kutoa maamuzi pasipo kufuata taratibu za kisheria hivyo bodi iundwe upya, alisema.

Kadhalika, alisema Agosti, mwaka jana walimuandikia barua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ya kumueleza malalamiko yao kuhusiana na uongozi ulipo, alkini hawajajibiwa.

Mmoja wa wahadhiri wa chuoni hapo ambaye hakutaja jina lake liandikwe, alisema kati ya watu kumi waliofukuzwa wanne ni wahadhiri, watano ni wafanyakazi wa maeneo tofauti na mmoja ni Mkuu wa Chuo hicho.

Kadhalika alisema watu wengine zaidi ya watano kwa nyakati tofauti wamepewa barua za kusitishiwa nyongeza za mishahara ya mwaka ambayo hata hivyo haijawahi kutolewa kutoka mwaka 2007.

Baadhi ya wanafunzi walisema kuwa kutoka Jumatatu ya wiki hii wahadhiri hawaingii madarasani bila sababu.

Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Miwande Madihi, alipotafutwa, ofisi yake ilikuwa umefungwa na baadaye Katibu Muhtasi alijibu kuwa alikuwa hayupo.

Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja, alisema ofisi yake haina taarifa za malalamiko ya watumishi wa chuo hicho na kwamba Nyoni kwa sasa yupo safarini nje ya nchi.

Baadaye jioni polisi aliyejitambulisha kuwa ni Dictative of Police alifika chuoni hapo na kuwakuta wahadhiri hao wakiwa wamekaa eneo moja na kuwataka watawanyike, lakini walikaidi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alipoulizwa kwa njia ya simu kama anataarifa zozote juu ya askari huyo, alisema kuwa inawezekana askari huyo alitumwa hapo, lakini hana taarifa za tukio hilo.

No comments: