TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Wednesday, July 13, 2011

Wabunge wajipanga kumkabili Ngeleja


KATIKA kile kinachoonyesha kuwa utendaji wa Wizara ya Nishati na Madini hauridhishi, baadhi ya wabunge wametahadharisha kuwa bajeti wa Wizara hiyo inayotarajiwa kusomwa kesho kutwa bungeni itakumbana na kingingi na huenda isipitishwe.Jana baadhi ya wabunge waliozungumza na Mwananchi walitahadharisha kuwa lazima bajeti hiyo ije na majibu ya uhakika kwa ajili ya kumkomboa mwananchi katika kupata huduma ya umeme na si kiini macho.

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, anatarajia kuwasilisha bajeti yake kesho kutwa ambayo itajadiliwa kwa muda wa siku mbili na kuhitimishwa siku ya Jumatatu ya wiki ijayo.

Akizungumza na Mwananchi jana Mbunge wa Mtera, Livingston Lusinde (CCM), alisema bajeti hiyo lazima ije na majibu ya kutosha kwa wananchi, vinginevyo hatakuwa tayari kuipitisha kwa kuwa kufanya hivyo atakuwa akiwasaliti wapiga kura wake.
Lusinde maarufu kama ‘Kibajaji’, alisema kma majibu ya Serikali itakuja mipango mingi isiyotekelezeka, safari hii haitavumiliwa na atakuwa mtu wa kwanza kuipinga.

“Mimi kama mbunge ninayetoka chama tawala ni wajibu wangu kuipitisha bajeti ile, lakini siwezi kuipitisha kama haitakuwa na majibu kwa wananchi wa Mtera, kwa kuwa kufanya hivyo nitakuwa nawasaliti wapiga kura wangu ambao wanatoka kwenye chanzo cha umeme, lakini kazi yao ni kulinda tu,’’alisema Lusinde.

Kwa upande wake Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi(CCM), alisema kama bajeti ya Nishati haitaleta majibu ya kutosha itazua mjadala mzito kwa kuwa kila mtu anaisubiri bajeti hiyo na kila mtu angependa kuichangia.Zambi alisema kelele za wabunge si tu kwamba wanataka kuonekana na kusikika, bali ni kutokana na Serikali kushindwa kuweka vipaumbele katika maeneo muhimu ikiwemo miradi ya maendeleo ambako kwa sehemu kubwa imekuwwa ikipangiwa fedha kutoka kwa wahisani bila ya kujua kuwa wanaweza kusitisha kutoa misaada.

“Kwa mfano, wabunge wanataka kujua katika kipindi cha mwaka huu Serikali ilisema kuwa imewekeza fedha nyingi katika miradi ya umeme, kwa hiyo kama kipaumbele kimewekwa huko tunatarajia kuona mambo makubwa, vingine ukumbi wa Bunge hautatosha,’’alisema Zambi.
Alisema Serikali itahitaji kuwa na majibu ya kutosha na yenye kuondoa mashaka kwa wananchi wanaotegemea kuona mambo mazuri kutoka ndani ya bajeti.

Mbunge mwingine aliyeitahadharisha Nishati na Madini ni David Kafulila (Kigoma Kusini-NCCR), ambaye alisema hali itakuwa tete siku itakapowasilishwa bajeti ya Wizara hiyo.

Kafulila alisema Wizara hiyo ni mboni ya jicho la Watanzania kwa hivyo kila mtu anategemea kuona mambo mazuri, vinginevyo ukumbi utakuwa ni mdogo siku ya Ijumaa na Jumatatu.Katika hatua nyingine, Chadema imemwandalia zengwe Waziri Ngeleja anayetarajia kusoma bajeti hiyo baada ya kusambaza waraka unaowataka wabunge wagome kuipitisha.Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa chama hicho kimeomba wabunge wagomee bajeti hiyo mpaka Waziri Ngeleja atakapokuja na mipango mbadala ya kumaliza tatizo la mgawo umeme.

Kwa mujibu wa habari hizo ambazo baadaye zilithibitishwa na taarifa rasmi iliyoandikwa na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, kama Waziri Ngeleja hatakuwa na jipya, anapaswa kutangaza kujiuzulu siku hiyo ya bajeti.Kwa mjibu wa taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari, tatizo la mgao wa umeme linaloendelea hivi sasa ni matokeo ya udhaifu wa viongozi hao wa Serikali.

Alisema hadi sasa Serikali imeendelea kutoa majibu yenye kukatisha tamaa kuhusu namna inavyoshughulikia tatizo la mgawo wa umeme na upungufu wa gesi asilia hapa nchini.“Leo (jana), Julai 12 mwaka huu, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima ametoa majibu yenye kuthibitisha kwamba Serikali inaendelea kuachia mgawo huu mkubwa wa umeme na upungufu wa gesi asilia uendelee kwa muda mrefu zaidi,”alisema Manyika katika taarifa hiyo.

Mbunge huyo wa Ubungo aliitaka Serikali kuwa taayari kujibu hoja zilizomo kwenye bajeti mbadala itakayowasilishwa na kambi ya upinzani bungeni na kutishia kuwa kama haitatoa majibu ya kuridhisha Chadema wataongoza maandamano nchi nzima.

“Kambi rasmi ya upinzani itawasilisha bajeti mbadala yenye kutoa mwelekeo wa kulinusuru taifa katika sekta ya nishati na madini kwa mwaka wa fedha 2011/12, hivyo tunaitaka Serikali kutoa majibu ya kuridhisha…,” alisema Mnyika.

Alisema Serikali kwa nyakati tofauti imeonyesha kuwa haina mikakati ya kutatua tatizo hilo huku akidai imekuwa ikitoa kauli za kumkingia kifua Waziri Ngeleja badala ya kuonyesha nia ya kutatua tatizo hilo.Manyika alikumbusha kwamba, Julai 6, 2011 Rais Kikwete alitoa kauli ya kumtetea Waziri Ngeleja kuwa si chanzo cha mgawo wa umeme, bali tatizo kuu ni kupungua mabwawa ya maji katika mitambo ya kuzalisha umeme.Manyika alisema kauli hiyo haikujibu hoja za msingi kuhusu umeme kwa kwa kuwa haikueleza hatua za haraka ambazo Serikali imechukua kuondokana na mgawo na upungufu wa gesi asilia.

HABARI KWA HISANI YA GAZETI LA MWANANCHI

No comments: