TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, July 15, 2011

SUNZU NIMEKUJA SIMBA KUFANYA KAZI

Mshambuliaji wazamani wa FC Lupopo na Alh-Hilal Felix Sunzu (kulia) akiongozana na Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Simba Geoffrey Nyange Kaburi (kushoto) badaa ya mchezaji huyo na mkewe (katikati) kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarega Nyerere jana jijini Dar es Salaam.


MSHAMBULIAJI wa Al Hilal na timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’, Felix Mumba Sunzu ametua nchini jana akitokea Nigeria kwa ajili ya kufanikisha usajili wake na klabu ya Simba huku akiahidi kumaliza ukame wa mabao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere, mshambuliaji Sunzu alisema huu ni wakati wa mafanikio makubwa kwa Simba na kwamba lazima awe mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania bara.

Sunzu ambaye aliwasili katika Uwanja huo saa 3:30 asubuhi akiwa na mkewe na kupokelewa na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange Kaburu pamoja na mashabiki wachache wa timu hiyo alisema kama mambo yote yatakwenda vizuri basi hana shaka yoyote juu ya kuipatia timu hiyo mafanikio.

“Nimekuja Simba kwa ajili ya mazungumzo na endapo mambo yatakwenda vizuri nitakuwa mali yao na kazi yangu kwao itakuwa ni moja tu kuipatia Simba mataji mengi katika kipindi chote nitakachokuwa na timu hiyo pili lazima niwe mfungaji bora wa ligi,” alisema Sunzu.

Alisema,“Mimi huwa napenda kuwa mfungaji bora kwa sababu ufungaji ndiyo kazi yangu hivyo lazima hilo litimie baada ya kumalizana na timu hiyo ili kazi yangu iwe moja tu…… mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.”

Tangu mwaka 2002 hadi 2008, Sunzu alicheza mechi rasmi 85 na kufunga mabao 43 akiwa na klabu za Afrisport F.C, Konkola Blades, AS Marsa, LB Chateauroux ya Ufaransa pamoja na timu za taifa za vijana na wakubwa.

Mchezaji huyo raia wa Zambia na mchezaji wa zamani wa FC Lupopo na Al-Hilal ya Sudani inayoshiriki mashindano ya Klabu bingwa Afrika alisema mbali na mashabiki wa Simba kumtegemea katika upachikaji mabao, pia wampe ushirikiano.

Sunzu ambaye amemalizana na Al Hilal ya Sudan aliyoitumikia kwa miezi sita, aliondoka Zambia wiki iliyopita na kukaa Nigeria kwa mapumziko alikotokea kabla ya kutua Tanzania na kuliambia Mwananchi kuwa amekuja Tanzania kwa ajili ya kuifanyia kazi Simba ili ichukue ubingwa wa mashindano mbalimbali.

‘’Nimekuja Tanzania kwa ajili ya Simba na kama mambo yanaenda sawa nikafanikiwa kuitumikia timu hiyo kazi itakuwa ni kufunga tu, nitafunga mabao mengi zaidi ya niliyopiga Chalenji nikiwa na Chipolopolo ili Simba ichukue ubingwa wa michuano mbalimbali,’’alisema Sunzu aliyewahi kuzichezea FC Lupopo ya Congo, Konkola Blades ya Zambia kabla ya kutua Al Hilal ambayo ilimsajili baada ya kumwona kwenye Chalenji.

Sunzu ambaye pia ni kaka wa tatu wa beki wa TP Mazembe, Stopilla Sunzu anatarajiwa kuimarisha safu ya ushambuliaji ya Simba ambayo inaonyesha kusuasua.

Kuhusu upinzani wa Simba na Yanga pamoja na wachezaji hatari waliopo kwenye timu hizo kwa hivi sasa Sunzu alisema, “Simfahamu mchezaji yeyote katika timu hizo zaidi ya ndugu yangu Davies Mwape anayecheza Yanga ingawa natambua kuwa Tanzania kuna ushindani mkubwa wa Simba na Yanga.

Awali mchezaji huyo aliwahi kunukuliwa katika vyombo vya habari akidai kuwa anavutiwa na soka la Yanga kwa sababu wanacheza mpira wa kasi na nguvu kuliko Simba huku akiweka bayana kwamba Yanga ikimhitaji atakuwa tayari kujiunga nao ingawa nafasi yake ilikuwa wazi zaidi kwa timu yoyote.

Naye Kaburu alisema; ‘’Nimefurahia ujio wake, tunafahamu uwezo wa Sunzu uwezO na ndiyo maana yuko hapa, tunaamini ataisaidia Simba kwa michuano mbalimbali, tuko naye na mambo yatakamilika muda si mrefu.’’

Dirisha la uhamisho limefungwa jana, Simba hadi sasa ina wachezaji wa kulipwa Jerry Santo wa Kenya, Patrick Mafisango kutoka Rwanda, Wills Ochieng kutoka Kenya, Derrick Walulya na Emanuel Okwi kutoka Uganda.

No comments: