TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Monday, July 18, 2011

Serikali yaweka kwapani bajeti ya madini Bungeni



WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amekata mzizi wa fitina kwa kuingilia kati na kuiondoa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini Bungeni ili iandaliwe upya na kurejeshwa tena baada ya wiki tatu, ikiwa ni hatua moja mbele kunusuru kukatiliwa kwa wingi wa kura za wabunge.

Tayari karibu wabunge wote waliochangia kutoka chama tawala na upinzani walikwishaonyesha msimamo wa kuikataa bajeti hiyo kutokana na mambo mbalimbali ikiwamo mikataba mibovu ya nishati na madini pamoja na tatizo sugu la mgawo wa umeme.

Katika kile kilichoonekana ni Serikali kusoma alama za nyakati, Pinda alichukua uamuzi huo wa kuahirisha bajeti hiyo jana baada ya kuona hata wabunge wa chama tawala ambao ni wengi bungeni wameigomea. Akitangaza hatua hiyo, Pinda alisema Serikali imezingatia kwa umakini michango iliyotolewa na wabunge hasa kuhusu tatizo la umeme linalolikabili taifa kwa sasa.

"Napenda kushukuru wabunge kwa michango yenu na ushauri wenu wa msingi na nasema nakubali kwa niaba ya Serikali," alisema Pinda.Waziri Mkuu ambaye ndiye kiongozi mkuu wa shughuli za kila za Serikali bungeni, alisema katika michango yao, wabunge walisema ili waridhike, ni lazima Serikali iwahakikishie kuwa tatizo la umeme litatatuliwa karibuni.

Pinda alikiri kuwa tatizo hilo ni la muda mrefu, kuanzia mwaka 2006 wakati taifa lilipokumbwa na ukame na mabwawa yake kukauka na matokeo yake uzalishaji wa umeme ukapungua.

Alisema wakati huo, Serikali iliweka mikakati ya kuacha kutegemea vyanzo vya umeme vya maji na kuweka mipango ya kutumia gesi asilia na makaa ya mawe, lakini mpango huo hadi sasa haujaleta mafanikio.

Kutokana na sababu hiyo, Waziri Mkuu alisema Serikali inazingatia ushauri uliotolewa na wabunge wa kuweka mpango wa kutatua tatizo hilo hata kama ikiwezekana viongozi wabanwe kwenye mapato na matumizi."Hata ikibidi tukate posho zetu, tubane matumizi ya magari, ili mradi tufanikishe mpango wa kuwapatia Watanzania umeme wa kuaminika," alisema Pinda.

Kwa kuzingatia hilo, Pinda aliliomba bunge litoe wiki tatu kwa Serikali ili iweze kurekebisha bajeti hiyo na ije na mkakati ambao utaweka wazi utatuzi wa tatizo la umeme nchini.

Pinda alitumia kipengele cha 55 cha kudumu za Bunge, kifungu kidogo cha 3(b) pia cha 69(1) ambavyo vinampa nafasi ya kuliambia Bunge sababu za kuahirisha bajeti na muda ambao utatumika katika kuirekebisha. Spika Anne Makinda alikubali hoja hiyo ya Serikali na alipohoji Bunge lilikubali.

Akifafanua kifungu hicho Makinda alisema hoja iliyotolewa na Waziri Mkuu ni mwongozo wa kanuni 69(1) isemayo: “Mbunge anayependa mjadala unaoendelea juu ya hoja yoyote kuahirishwa hadi wakati wa baadaye ,anaweza kutoa hoja kwamba mjadala huo uaharishwe hadi wakati gani na kulazimisha kutoa sababu kwa nini anataka mjadala uahirishwe na kwa wakati gani huku wananchi wategemee nini wakati mjadala umeahirishwa."

“Suala hili limevuta hisia za Watanzania wengi na wengine limeonekana kuwawakasirisha kwa kiasi kikubwa kwani limeonekana kuwavurugia uchumi wao na hata kusababisha Serikali kukosa mapato hivyo naungana mkono hoja na baada ya wiki tatu wajipange vizuri wakileta kitu kilicho katika ahadi za Serikali na zinazotekelezeka,” alisema.

Hatua hiyo ya serikali inafuatia msimamo mkali wa wabunge ambao waliikataa kutokana na sekta za madini na nishati kugubikwa na kashfa nyingi za kifisadi huku ikishindwa kuweka mkakati wa kutatua tatizo la umeme ambalo linaendelea kuangamiza uchumi wa nchi.

CCM watoa msimamo wao kuhusu hatua hiyo
Akizungumzia suala hilo jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema; "Nawapongeza sana wabunge wa CCM kwa usikivu wao kwa kilio cha wananchi sababu wao ndiyo wengi, wangelikuwa si wasikivu basi bajeti ile ingepita."

Alisema angewashangaa wabunge hao kama bajeti hiyo iliyokuwa ikilalamikiwa ingepita kwani kasoro zake zilikuwa nyingi na zilihitaji kufanyiwa marekebisho.

"Kwa niaba chama chetu cha Mapinduzi niwashukuru wabunge wetu waliofanya kazi kwa maslahi ya wananchi na hii inajibu kelele za siku nyingi za wapinzani wanaodai kwamba Serikali ya CCM haiwajali wananchi," alisema Nape.

Alisema huo ni mwanzo mzuri kwa CCM iliyojivua gamba ambayo sasa inafanya kazi kwa vitendo na kwa kusikiliza kilio cha wananchi."Sasa kinachotakiwa na tunachokisubiri ni kwa Serikali iwe sikivu irudi ijipange iweze kuleta mipango thabiti ya kuweza kuleta umeme wa uhakika, ambao ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa letu hili."

No comments: