TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, July 29, 2011

SERIKALI CHALIIIIII MBELE YA BOSI WA RICHMOND, AIGALAGAZA VIBAYA MAHAKAMANI

MITAMBO YA KUFUA UMEME WA DHARURA YA RICHMOND ILIORITHIWA NA KAMPUNI YA DOWANS POWER PLANT

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imemwachia huru mfanyabiashara Naeem Adam Gile, Mkurugenzi wa Kampuni ya Richmond Tanzania Ltd.

Katika kesi hiyo, Gile alikuwa akikabiliwa na makosa ya kughushi, kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali kuhusu kampuni ya Richmond, yenye makao makuu yake Texas, nchini Marekani.

Uamuzi wa kumuachia huru mtuhumiwa huyo, ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Waliarwande Lema aliyesema ushahidi uliotolewa na serikali ni dhaifu.

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa, na Richard Rweyongeza, wakati serikali iliwakilishwa na mawakili wa serikali, Fredrick Manyanda na Shadrack Kimaro.

Hakimu Lema alisema amefikia uamuzi huo baada ya kupitia maelezo ya mashahidi wote tisa na vielelezo vilivyotolewa na serikali ambapo amebaini ushahidi na vielelezo hivyo ni dhaifu vyenye upungufu unaoacha maswali mengi.

Alisema kutokana na hilo mahakama imeamua kutumia kifungu cha 330 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 kinachotoa mamlaka ya kumwachia huru mshtakiwa.

“Hii kesi ina upungufu mwingi wa kisheria tena uko wazi kabisa na simung’unyi maneno, kesi hii ni miongoni mwa kesi za jinai zinazofunguliwa na serikali bila ushahidi wa kutosha mwisho wa siku mahakama zinajikuta zikitupiwa lawama kwa kuwaachia huru watuhumiwa,” alisisitiza hakimu Waliarwande.

Hakimu huyo alisema Gile alikuwa akikabiliwa na makosa ya kughushi, kutoa hati ya uwakilishi (Power of Attorney), kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali ambao ni wajumbe wa bodi ya wazabuni ya Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) na timu ya tathmini.

Januari 13, 2009 Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Stanslaus Boniface, alidai kuwa Machi 13 mwaka 2006, jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu, mshtakiwa huyo alighushi hati ya uwakilishi ya Machi 13, 2006.

Boniface alidai hati hiyo ilionyesha Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas ya Marekani, Mohamed Gile, ambaye ni kaka wa mtuhumiwa anayeishi Marekani, alimuidhinisha mshtakiwa kuiwakilisha hapa Tanzania.

Kwa mujibu wa hakimu Waliarwande katika hati ya mashtaka, Jamhuri inadai kuwa Machi 20 mwaka 2006 eneo la Umeme park, barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu mshtakiwa huyo alitoa hati ya uwakilishi kwa maofisa hao wa serikali.

Aliongeza kuwa hati hiyo ilisainiwa na Mohamed Gile kuonyesha kuwa Mohamed amemteua mshtakiwa kuiwakilisha kampuni hiyo hapa nchini kinyume na kifungu cha 333; 335(e)(3); 337; 342 na 122(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Akitoa uamuzi huo, hakimu huyo alianza kulichambua kosa la kughushi ambalo ni kinyume cha kifungu cha 333 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

“Hivyo basi katika kutatua mgogoro wa hati hiyo ya uwakilishi, Jamhuri ilileta mashahidi watatu kwa ajili ya kuutatua mgogoro huo miongoni mwa mashahidi hao ni mawakili wawili waliyoiandaa hati na shahidi wa sita akiwemo mtaalam wa maandishi kutoka Jeshi la Polisi, Hamis Hamad.

“…Licha ya kuletwa kwa mashahidi hao watatu kwa ajili ya kuutatua mgogoro huo, mahakama hii imebaini hakuna ushahidi unaonyesha hati hiyo ya uwakilishi ilighushiwa, hakuna ushahidi uliotolewa ukionyesha mshtakiwa huyo alighushi hati hiyo kwa kuwa hata huyo shahidi wa sita ambaye ni mtaalamu wa maandishi kutoka polisi, hakuweza kutoa upungufu uliokuwepo kwenye ile hati ya uwakilishi inayodaiwa kughushiwa.”

Kuhusu shtaka la pili na la tano ambalo ni la kuwasilisha hati iliyoghushiwa kwa maofisa wa serikali, hakimu huyo alisema kosa la kwanza la kughushi hati hiyo ya wakili, Jamhuri imeshindwa kulithibitisha. Ni wazi kabisa hati hiyo ya uwakilishi iliyowasilishwa kwa maofisa wa TANESCO haikughushiwa.

Hakimu aliendelea kusema, kosa la tatu na la nne ambalo Gile anadaiwa kutoa taarifa ya uongo kuwa mitambo ya Richmond ina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100 huku akijua si kweli, serikali imeshindwa kuthibitisha.

Alisema kuwa ushahidi ulioletwa mahakamani ulisema kikao cha kwanza cha ufunguzi wa zabuni ya Richmond kilichofanyika Machi 2, 2006 kampuni zote zilisailiwa na bodi na timu hiyo ikabaini hakuna kampuni iliyokidhi vigezo na ikaamuru usaili ufanyike upya.

Aliongeza kwamba hata ulipofanyika usaili, hakuna kampuni iliyoshinda kukidhi vigezo, lakini shahidi wa tatu mhandisi wa TANESCO, Simon Jilima, mwaka 2006, aliteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, kusimamia ufungwaji wa mitambo ya Richmond.

“Kwa ujumla mahakama hii inasema Jamhuri imeleta ushahidi dhahifu ambao umeshindwa kuishawishi mahakama imuone mshtakiwa ana kesi ya kujibu,” alirudia hakimu Waliarwande.

Aliongeza hakuna ushahidi unaonyesha nyaraka za kampuni ya Richmond zilizowasilishwa bodi ya TANESCO ziliwasilishwa na mshtakiwa ila kwa mujibu wa shahidi wa nne aliyeiambia mahakama kuwa nyaraka hizo ziliwasilishwa kwenye bodi hiyo na mwenyekiti wa Richmond, Mohamed.

Aliwatambulisha wajumbe wa bodi kuwa mshtakiwa ni mdogo yake na kwamba ndiye amempa jukumu la kuiwakilisha kampuni yake hiyo hapa Tanzania.

“Na kwa kuwa Jamhuri ilidai mshtakiwa alighushi saini ya Mohamed Gile katika ile hati ya uwakilishi, Jamhuri ilipaswa imlete Mohamed hapa mahakamani aje kutoa ushahidi kwamba hakumpa mshtakiwa mamlaka ya kuiwakilisha kampuni yake nchini Tanzania.

“…Jamhuri imeshindwa kutekeleza jukumu lake ili mwisho wa siku mahakama ilaumiwe, mahakama hii inamwachiria huru mshtakiwa na inamfutia kesi hiyo,” alisema.

Baada ya kutoa uamuzi huo wakili wa serikali Shadrack Kimaro alisema Jamhuri haijaridhishwa na uamuzi huo hivyo inaomba ipatiwe mwenendo wa kesi hiyo kwa lengo la kukata rufaa, Mahakama Kuu.

Kwa upande wake mtuhumiwa huyo aliwaeleza waandishi wa habari nje ya viwanja vya mahakama kwamba amefurahishwa na uamuzi huo kwa kuwa haki imetenda.

Gile alifikishwa mahakamani hapo Januari 13, 2009 takriban mwaka mmoja baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, kujiuzulu nyadhifa zao kwa kashfa ya kuwepo kwa rushwa kwenye zabuni ya kufua umeme wa megwati 100 iliyopewa kampuni ya Richmond.

No comments: