TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Saturday, July 2, 2011

PINDA AJIBU MAPIGO YA LOWASAWAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amemjibu mtangulizi wake ambaye pia ni mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kuhusu kauli yake kwamba Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imekuwa ikisita kufanya uamuzi mgumu, akieleza kwamba serika hiyo imekuwa ikizingatia hilo kwa umakini mkubwa.Pinda aliyasema hayo jana mjini Dodoma alipokuwa akijibu hoja mbalimbali, zilizotolewa na wabunge waliokuwa wakichangia hotuba ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2011/12, mjini Dodoma.

Pinda ambaye alianza kujibu hoja hiyo, bila kuwataja watu walioichangia kama alivyokuwa akifanya katika hoja nyingine, alisema hata hatua ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kulivunja Baraza la Mawazi lililokuwa ulikuwa ni uamuzi mgumu sana.Ijumaa iliyopita, Lowassa alisema Serikali ya Rais Kikwete inasumbuliwa na ugonjwa wa woga katika kutoa uamuzi magumu na matokeo yake mambo yake mengi hayaendi kama yalivyopangwa.

Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza chini ya Kikwete, pia aliitaka Serikali hiyo kubadilika.Alisema kuwa ni bora kulaumiwa kwa kufanya uamuzi mgumu kuliko kulaumiwa kwa kutofanya uamuzi na kwamba Serikali inapaswa kufanya uamuzi bila kujali matokeo yake huku akipendekeza kwa kuanzia, ikope kwa kutumia rasilmali za nchi.

"Ni bora kulaumiwa kwa kufanya maamuzi kuliko kulaumiwa kwa kutofanya maamuzi kabisa,"alisema Lowassa.Bila kueleza ni maamuzi gani ambayo serikali hiyo imeshindwa kufanya, Lowassa alisema ugonjwa wa viongozi kuogopa kufanya maamuzi ni hatari kwa uchumi wa taifa kwa kuwa kuthubutu ni msingi wa mafanikio katika nyanja mbalimbali kijamii na kiuchumi.

"Kuna ugonjwa wa kutokutoa maamuzi hapa na lazima tukubali kubadilike. Ni heri mtu ukosee kutoa maamuzi kuliko kukaa kimya kabisa, heri uhukumiwe kwa kutoa maamuzi kuliko ulaumiwe kwa kushindwa kutoa maamuzi,"alisema.

Lowassa alitoa kauli hiyo huku serikali ikionekana kushindwa kutatua matatizo mbalimbali yaliyoko nchini hivi sasa ikiwemo matatizo ya usafiri wa reli, msongamano na makontena bandarini na ujenzi wa bandari pamoja na taifa kukabiliwa na mgawo wa mara kwa mara wa nishati ya umeme uliodumu tangu mwaka 2006.

Lakini jana akijibu hoja hiyo, Pinda alisema serikali imefanya uamuzi mgumu sana ikiwa ni pamoja na kuwafikisha baadhi ya mawairi wanaokabiliwa na mashitaka mbalimbali mahakamani.Alisema pia kuwa, ujenzi wa shule za kata nchi nzima pamoja na chuo kikuu cha Dodoma, ni moja ya hatua ya uamuzi mgumu ambao serikali imeyachukua.

“Kuna wabunge wengi wamekuwa wakichangia juu ya serikali kuchukua maamuzi, wengi wamekuwa wakiita maamuzi magumu, Serikali ya Awamu ya Nne imekuwa ikifanya maamuzi mengi magumu lakini kwa umakini mkubwa na kwa kufuata misingi ya sheria, alisema Pinda na kuongeza:"Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete imekuwa ikifanya maamuzi magumu sana, … ni awamu hii iliyofanya uamuzi mgumu wa kuvunja Baraza la Mawaziri baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kujiuzulu.”

Pinda alianza kujibu hoja hiyo kwa kueleza mambo ambayo yamefanywa na serikali zote zilizotangulia ikiwa, ikiwa ni pamoja na awamu ya kwanza aliyosema ilifanya maamuzi magumu sana ambayo mengine mpaka leo yamekuwa yakiinyima serikali iliyopo baadhi ya frusa.

Kwa mujibu wa Pinda, Serikali ya Awamu ya pili ilifanya maamuzi magumu pia hali iliyofanya mpaka Rais wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi, kupewa jina la Ruksa.Pinda alibainisha kwamba, katika awamu ya tatu licha ya hali ngumu ya uchumi, serikali ya wakati huo ilichukuuwa uamuzi mgumu mara kadhaa ili kuisaidia nchi kufanya vizuri.

Baraza la Mawaziri
Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alikuwa amejibu hoja pamoja nile iliyotolewa na Mbunge Viti Maalum Chadema, Suzan Lyimo kutaka Baraza la Mawaziri livunjwe ili kuipunguzia serikali matumizi, zinalindwa na Ibara ya 36 na 37 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lukuvi alisema "Ibara ya 36 na 37 ya Katiba imempa rais mamlaka ya kuunda na kuvunja wizara na Baraza la Mawaziri hivyo majibu yangu naomba yaishie hapo. Ila tuelewe tu kuwa kutaka hayo yafanyike ni mchakato mrefu unaohusisha mabadiliko ya ibara hizi za katiba,".

Suala la ukubwa wa serikali lilizungumzwa pia na Lowassa ambaye aliishauri Serikali itenganishe Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na kueleza mafanikio ya chama tawala, CCM na Serikali katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu inashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kuwa ni kubwa mno, hivyo inastahili kugawanywa kwa kuiondoa ofisi hiyo ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa."Ofisi hii ni kubwa sana, kuna Maafa, Uratibu, Bunge, Uwezeshaji, Uwekezaji na Tamisemi. Tamisemi yenyewe pia imegawanyika katika mambo mengi sana.

Dawa za kulevya
Wakati huo huo serikali ilisema kuwa itawaonyesha wabunge video ya picha za viongozi wa dini na vigogo wengine wa dawa za kulevya katika semina maalumu itakayoandaliwa katika kipindi cha mkutano huu wa bunge unaoendelea mjini Dodoma.Akijibu hoja mbalimbali za wabunge walizochangia katika Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Lukuvi alisema semina hiyo itakayoendeshwa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, ina lengo la kuwaonyesha wawakilishi hao wa wananchi jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali katika kudhibiti tatizo hilo

"Hoja ya dawa za kulevya iliulizwa na Pindi Chana, Amina Abdallah Amour, Faharia Shomari. Baada ya kuona hizi changamoto nyingi, ambazo wabunge wamezitoa. Tumeamua kama serikali kwamba ile timu yetu ya task force (kikosi kazi), ambayo inafanya kazi hii, ije itoe semina hapa kwa waheshimiwa wabunge," alisema Lukuvi na kuendelea:

"Katika kipindi hiki cha Bunge tutaomba nafasi na nitaomba wabunge wote wahudhurie ili angalau tuwaonyeshe mambo yanayofanyika, watu wanaohusika tutawaonyesha, aina ya dawa tulizozikamata na mbinu mbalimbali zinazotumiwa na hao watu kutoka huko wanakozitoa dawa mpaka kufika hapa na soko lao na waathirika wote."
Waziri Lukuvi aliendelea kulieleza bunge kuwa "Nimeshawaagiza tume ya dawa za kulevya na task force wajiandae vizuri, maana sisi walituonyesha juzi kwenye semina elekezi. Waje hapa wawaonyeshe waheshimiwa wabunge jinsi vijana wetu wanavyoathirika na watu hao mnaowaita vigogo, maana vigogo tafsiri yake mara nyingi huchukuliwa kama ni watu wa serikali."

Lakini kwa Mujibu wa Waziri Lukuvi, vigogo kwa tafsiri pana sio viongozi wa serikali pekee bali pia ni watu wenye uwezo wanaojihusisha na shughuli za dawa za kulevya wakiwamo wale aliowasema Rais Kikwete kuwa hata baadhi ya viongozi wa dini wanahusika."Tutawaonyesha moja kwa moja muwaone na shughuli wanazozifanya na walivyokamatwa ili waheshimiwa wabunge kama wawakilishi tushikiriane vizuri na serikali lakini mkiwa mmearifiwa vizuri," alisemna Lukuvi na kuendelea:

"Kwa hiyo nataka kuwaomba wote waliotoa changamoto katika eneo hili, wakubali kwamba ushauri wao tumepokea, tunautekeleza, lakini zaidi ingawa hapa nimetaja hata huyo kiongozi wa dini ambaye ni rai wa Nigeria, ni kiongozi wa kanisa la Lord Choosen Charistmatic Rivival Church lililopo Kinondoni Biafara, ambaye alikamatwa na jumla ya kilo 81 za Cocain maeneo ya Kunduchi Mtongani."

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, hapa nchini Kanisa hilo lina matawi katika mikoa ya Mwanza na Arusha wakati pia lina matawi nchini Kenya, Afrika Kusini na Uingereza."Kabla hatujatangaza taarifa hii, ukiwauliza waumini, maana ana waumini wengi sana kwa maelfu, mchungaji wenu yuko wapi wanasema amesafiri, kumbe tumemshika. Sasa angalau wanajua kwamba yuko wapi," alisema.

Kuonyeshwa kwa vigogo hao kwa njia ya video kutamaliza mvutano ulioibuka kati ya viongozi wa dini na rais Jakaya Kikwete baada ya raisa kueleza kuwa viongozi wa dini ni sehemu ya tatizo la dawa za kulevya nchini.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga wakati wa ibada maalumu ya kupewa daraja la uaskofu na kusimikwa kwa Askofu wa jimbo hilo, Mhashamu John Ndimbo, katika kanisa la kiaskofu la Mtakatifu Killian.No comments: