TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, July 14, 2011

LOWASAA NA CHENGE JIPIMENI WENYEWE KAMA ROSTAM
UAMUZI wa mbunge wa Igunga na mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz, kutangaza kujivua ubunge na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) unaweza ukawa mtihani mzito kwa wanasiasa wengine wawili wenye majina makubwa ndani ya chama hicho.

Wanasiasa hao ambao kwa namna yoyote wanaweza wakawa wameguswa na uamuzi huo wa Rostam kwa namna tofauti ni waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Mbunge wa Maswa Magharibi, Andrew Chenge.

Kikubwa kinachowaunganisha wanasiasa hao watatu ni kauli ambazo zimekuwa zikiwalenga tangu kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM miezi mitatu iliyopita ambacho kinadaiwa kupitisha azimio la kuwataka kuachia nafasi zao za kisiasa wanazoshikilia kutokana na kukabiliwa na tuhuma tofauti za ufisadi.

Baadhi ya wadadisi wa kisiasa wanaielezea hatua hiyo ya Rostam kuwa inaweza kuwaweka katika hatua ngumu zaidi ya kutetea nyadhifa zao za kisiasa, Lowassa na Chenge.

Wachambuzi hao wa mambo wanaielezea hatua hiyo kuwa inaweza ikatumiwa na viongozi wapya wa CCM kama Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye, kuendeleza kauli zake kwa kuwataka Lowassa na Chenge kuiga mfano wa Rostam.

“Uamuzi wa Rostam kujiuzulu ubunge na ujumbe wa NEC ni ushindi kwa Nape, sekretarieti mpya ya chama hicho na Rais Jakaya Kikwete ambao ndiyo waratibu wakuu wa ajenda ya kujivua gamba,” alieleza mchambuzi mmoja wa habari.

Hata hivyo, mbunge mmoja wa CCM aliyezungumza na blog hii alisema uamuzi wa Rostam kujiuzulu ubunge unaweza ukawa pigo kubwa kwa chama hicho tawala iwapo kitalipoteza jimbo hilo kwenda kwa upinzani.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, tishio hilo la CCM kupoteza jimbo moja la uchaguzi, si tu inaweza ikawa pigo kwa chama hicho bali kikwazo cha kuendelea kutekelezeka kwa dhana hiyo ya kujivua gamba.

Mbunge huyo anasema iwapo hilo litatokea basi yale yaliyokuwa yakielezwa kuwa dhamira ya kukisafisha chama hicho ili kiendelee kukubalika machoni mwa wananchi kinaweza kikawa kushindwa kwa maamuzi mazito ya viongozi hao wapya wa CCM.

Uchunguzi uliofanywa na blog hii kuanzia jana alasiri baada ya habari kuhusu Rostam kusambaa ulionyesha kuwa watu wengi waliokuwa wamesikia taarifa hizo, walipeleka mawazo yao kwa wanasiasa hao wawili.

Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti hili walieleza kwamba hatua hiyo ya Rostam kujivua ubunge inaweza ikawaweka katika wakati mgumu wanasiasa hao wawili.

Mmoja wa watu waliotoa kauli akiwalenga wanasiasa hao pasipo kuwataja kwa majina ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), ambaye katika mazungumzo yake na gazeti hili alielezea kuunga mkono hatua hiyo ya Rostam.

Lembeli mbunge ambaye amekuwa akijitambulisha kuwa kamanda wa ufisadi mbali ya kueleza kwamba hatua hiyo ya Rostam inaonyesha ukomavu wa kisiasa, aliwataka wanasiasa wengine wenye tuhuma kufanya kile alichokieleza kuwa ni kukinusuru chama chake.

Wakati Lembeli akitoa matamshi hayo, Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Umoja wa Vijana wa CCM, Hussein Bashe, kwa upande wake alieleza kusikitishwa na tafsiri ya dhana ya kujivua gamba inayowalenga wanasiasa watatu tu wakubwa ndani ya chama hicho.

Bashe aliyekuwapo Igunga wakati Rostam akitangaza uamuzi wake huo, alisema mtazamo huo unaowalenga wanasiasa hao watatu unalenga kukiua chama hicho badala ya kujijenga na kukiimarisha.

Kwa Lowassa na Chenge, kauli hiyo ya Bashe inaweza ikawa kipimo wanachoweza kukitumia kutafakari namna ya kukabiliana na shinikizo la kuwataka wajiuzulu nafasi zao za kisiasa.

Habari ambazo Blog hii imezipata kutoka kwa watu walio karibu na Lowassa zinaeleza kwamba mwanasiasa huyo alikuwa akikusudia kuchukua hatua tofauti na ile iliyotangazwa na Rostam ambaye amekuwa rafiki yake wa muda mrefu.

Vyanzo vya habari vya kuaminika, vimelihakikishia gazeti hili kwamba mkakati huo wa Lowassa ambao haukuweza kupatikana, umekuwa ukitokana na kuwapo kwa msukumo mkubwa kutoka kwa wanasiasa wengine walio ndani na nje ya chama hicho.

Habari zinaeleza kwamba Lowassa amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kumtaka ajitokeze hadharani na kueleza ukweli wote anaoujua kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwake.

Kwa mujibu wa habari hizo, viongozi wa serikali, CCM na kiimani ambao wamekuwa wakiwasiliana na Lowassa wamekuwa wakimtaka achukue hatua hizo kutokana na kuwapo kwa mgawanyiko mkubwa kuhusu tuhuma anazokabiliana nazo.

Ni wazi kwamba baada ya hatua ya jana ya Rostam kujitokeza hadharani na kuamua kujivua ubunge na ujumbe wa NEC, Lowassa anaweza akajikuta akiridhia ushawishi huo ambao amekuwa akikataa kuutekeleza kwa muda mrefu.

Wakati hali ikiwa hivyo, kwa upande wa Chenge habari zinaeleza kwamba ingawa hajaeleza bayana uamuzi ambao anakusudia kuuchukua bado alikuwa akitafakari majaliwa yake ya kisiasa kwa siku zijazo.

Chenge ambaye amekuwa nje ya nchi, anaelezwa kwamba amesikika mara kadhaa akipinga hatua zozote za kumshinikiza kujiuzulu nafasi za uongozi wa kisiasa anazoshikilia.

Mtu mmoja aliye karibu na Chenge ambaye amepata kuwa mwanasheria mkuu wa serikali, amelieleza Tanzania Daima kwamba iwapo atalazimika au kulazimishwa kujiuzulu ujumbe wa NEC, basi upo uwezekano mkubwa wa yeye pia kujivua ubunge kama alivyofanya Rostam.

No comments: