TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, July 15, 2011

HII NI SIRI YA JAKAYA NA ROSTAM


UAMUZI wa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kuachia nyadhifa zake ndani ya chama tawala, CCM mapema wiki hii unaonekana kuwa siri nzito kati yake na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete. Hadi jana, si chama hicho (CCM), Ofisi ya Bunge, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa au Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) iliyokuwa tayari kutoa taarifa rasmi za uamuzi huo.

Kila upande uliieleza Mwananchi kuwa haukuwa umepata taarifa rasmi au hata kuiona barua ya Rostam, kiasi cha kuiacha barua ile kuwa siri baina ya washirika hao wawili kisiasa na wafuasi wa uliokuwa mtandao uliomwingiza madarakani Kikwete mwaka 2005.

Hadi tunakwenda mitamboni, viongozi waandamizi wa CCM walielekea kukosa majibu ya msingi kuhusu ilipo barua ya kujiuzulu kwa Rostam.

Wakati Rostam akiliambia gazeti hili juzi kuwa amewasilisha barua yake kwa mwenyekiti Kikwete, makamu mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Pius Msekwa, Katibu Mkuu, Wilson Mkama na Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye jana walisisitiza kuwa hawana taarifa rasmi za uamuzi huo wa kujiuzulu kwa Rostam na kuacha nafasi zake za Ubunge na Ujumbe wa Nec.

Mbali na viongozi hao wa chama, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa na ofisa mmoja mwandamizi wa Tume ya Taifa Uchaguzi (Nec) ambaye hakutaka kutajwa gazetini, walisema pia taarifa za Rostam kujiuzulu ubunge hawajazipata rasmi.


Kauli ya Msekwa
Jana, Msekwa aliliambia gazeti hili kuwa chama hakina taarifa rasmi, lakini pia hawana cha kufanya kama kweli amejiuzulu kwa kuwa huo ni uamuzi wake.

“Sasa sisi tuchukue hatua gani? Mtu amechukua uamuzi wake, tufanye nini? Hebu na wewe nisaidie tufanyeje,” alihoji Msekwa. Katika hali ya kushangaza, Msekwa alisisitiza kuwa chama kimeshatoa tamko rasmi kwa hiyo hakuna haja ya viongozi wake kuendelea kuulizwa.

Ingawa Msekwa hakufafanua tamko gani lililowahi kutolewa na CCM kuhusu kujiuzulu kwa Rostam, juzi Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama alisema, "Sisi bado hatujapata taarifa rasmi kutoka kwake( Rostam)."

“Kwani wewe jana hukusikia tamko letu?" Alihoji Msekwa, na alipoulizwa tamko gani, hakusema chochote zaidi ya kusisitiza "Mwongo... mwongo, mwongo." kisha akakata simu.

Mukama awa mbogo
Wakati Msekwa akitoa kauli hiyo, Katibu Mkuu wa CCM Wilson Mukama, aligeuka mbogo baada ya kumfokea mwandishi baada kujitambulisha na kueleza swali lake.“Tulishatoa msimamo wa chama jana (juzi),” alisema Mukama kwa jazba na kisha kukata simu.

Nape: Sina hakika kama JK anayo barua ya Rostam
Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana kuwa hadi mchana jana, hakuwa na taarifa za uwepo wa barua ya Rostam kwenye chama.Awali, Nape alieleza kuwa jana hakuwa makao makuu ya CCM, lakini hakuwa anajua kama kuna barua hiyo.

Alipoelezwa kwamba, Rostam mwenyewe amesema kuwa barua yake iko kwa mwenyekiti (Rais Jakaya Kikwete), alisema, "Hilo ndio naliskia kutoka kwako. Mimi sijui kama kamkabidhi mwenyekiti."

Kingunge: No Comment
Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale- Mwiru, alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema, "No Comment" (Sina cha kusema).Alisema hayo alipotafutwa na gazeti hili atoa maoni yake kuhusu uamuzi wa kada huyo wa siku nyingi wa CCM kujiuzulu nyadhifa zake zote.

Tendwa: Nami sijui
Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tenbdwa alisema kama kweli Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz amejiuzulu nafasi yake itajazwa baada ya siku 90 na hadi jana hakuwa na taarifa rasmi.Kwa mujibu wa Tendwa, hadi jana alikuwa hajapata taarifa kamili za kujiuzulu kwa mbunge huyo.

Akizungumza na Mwananchi jana, Tendwa alisema, “Kujiuzulu kwa Rostam kunasikika katika vyombo vya habari, lakini bado hajakamilisha taratibu zinazotakiwa.“Hizi taarifa zinasomwa kwenye magazeti, bado hajakamilisha taratibu zinazotakiwa, kwa mfano kukiandikia chama chake barua juu ya uamuzi wake wa kujiuzulu,” alisema Tendwa.

Tendwa aliongeza, “Mbunge huyo atakapokiandikia chama chake barua, ama yeye mwenyewe au chama husika kitaandika barua kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kumpa taarifa hizo.”
Alifafanua kwamba, baada ya spika kupokea barua hiyo atatakiwa kutangaza bungeni kuwa nafasi yaJimbo hilo liko wazi.

“Jimbo litakapokuwa wazi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inapaswa kutangaza uchaguzi baada ya siku 90,” alifafanua Tendwa.

Nayo NEC
Akizungumza na Blog hii kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, ofisa mmoja wa tume hiyo, alisema bado hawajapata taarifa rasmi ya kujiuzulu kwa mbunge huyo wa Igunga."Bado hatuna taarifa rasmi ya kujiuzulu kwake na wala haijafikishwa kwetu sisi,’’ alisema ofisa huyo wa Nec, tume yenye dhamana ya kusimamia uchaguzi nchini.

Alifafanua kwamba, suala la kujiuzulu kwa Rostam hatua hiyo haihusu Nec, bali chama (CCM) na Bunge, kwani wao hupelekewa taarifa.Kwa mujibu wa ofisa huyo, wajibu wao ni kujaza nafasi zilio achwa wazi na viongozi.

Aidha, ofisa wa tume hiyo alisema kuwa tume yake ina wajibu wa kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa wabunge katika Jamhuri ya Mungano wa Tanzania

Spika wa Bunge
Juzi, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema ofisi yake haina taarifa rasmi na kwamba itawasiliana na wabunge baada ya kupata taarifa hiyo

Makinda alisema hayo alipokuwa akitoa mwongozo kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (Chadema) aliyetaka kujua endapo kiti cha ubunge katika jimbo la Igunga kipo wazi."Sijapata taarifa rasmi, lakini mara nitakapozipata nitawaeleza utaratibu," alisema Makinda.

Rostam: Barua yangu iko kwa JK
Jana gazeti hili lilipomtafuta Rostam aeleze kwa nini ameamua kumpa barua yake Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete badalaya katibu Mkuu Wilson Mukama hakupatikana baada ya simu yake ya mkononi kutoita kabisa.

Lakini baadhi ya washirika wake wa karibu walilishauri gazeti hili kumtumia ujumbe kupitia simu hiyo ingawa hata baada ya kuupata, aliendelea kukaa kimya.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Salva Rweyemamu hakupatikana jana kutwa nzima na simu yake ilikuw ainaita muda wote bila kupokelewa, lakini majira ya saa 11: 00 jioni simu hiyo ilipokelewa na mtu alyejitambulisha kuwa msaidizi wake ambaye alilieleza gazeti hlii kuwa: "Salva yuko busy".

Mwandishi Msaidizi wa Rais, Premi Kibanga hakupatikana muda wote kuzungumzia suala hilo jana kutokana na simu yake ya mkononi kuita muda mwingi bila kupokelewa

Maalim Seif amzungumzia Rostam
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, alisema uamuzi wa kujiuzulu uliofanywa Rostam ni wa busara kutokana na hali ya siasa ilivyo sasa nchini.

Hata hivyo, Maalim Seif alikiri hadi jana binafsi, hakuwa amepata sababu kamili ya mbunge huyo aliyedumu katika jimbo lake kwa miaka 18 kuchukua uamuzi huo.

"Rostam amefanya uamuzi wa busara na nadhani hii itakuwa imetosheleza shauku iliyokuwa imetawala miongoni mwa wananchi wengi waliotaka kujua dhana nzima ya kujiua gamba," alisema Maalim Seif.

Alifanua kwamba huenda uamuzi huo umekuja baada ya mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kuzungumza wakati wa mkutano mkuu wa chama dhana ya uwajibikaji na kujivua gamba kwa viongozi wote wanaotuhumiwa ni mafisadi.

HABARI HII NIKWA HISSANI YA GAZETI LA MWANANCHI NA BLOG HII

No comments: