TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, July 7, 2011

DPP aomba ushahidi wa Dk Slaa dhidi ya Chenge


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa

MKURUGENZI wa Mashtaka Nchini (DPP), Eliezer Feleshi, amemtaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, kuwasilisha nyaraka zenye ushahidi dhidi ya watuhumiwa wa rada serikalini ili ziweze kufanyiwa kazi.Feleshi aliliambia gazeti hili jana kuwa ofisi yake inayo sehemu ya ushahidi wa suala hilo, lakini hautoshi kumtia Chenge hatiani kama atafikishwa mahakamani."Kama Chadema wanao (ushahidi), kama alivyoeleza Dk Slaa, walete tutaulinganisha na ushahidi tulionao ili tuone kama unatosha kuitetea kesi hiyo mahakamani," alisema Feleshi.

Kwa mujibu wa Feleshi kuna uwezekano wa nyaraka alizonazo Dk Slaa kuwa na ushahidi unaotofautiana na ushahidi uliopo serikalini hivyo kuwasilisha nyaraka hizo, kutasaidia kufanikisha jambo hilo.

“Sheria zetu zina utaratibu mzuri wa kupokea ushahidi. Sheria ya Mwenendo wa Kesi na Makosa ya Jinai, kifungu cha Saba na ile ya kupambana na rushwa, kifungu cha 39, zinaeleza bayana kuwa mtu mwenye ushahidi anaweza kuuwasilisha kwenye vyombo vinavyohusika,” alisema Feleshi.

Feleshi alitoa kauli hiyo jana alipotakiwa na gazeti hili kuzungumzia kauli ya Dk Slaa aliyoitoa juzi kuwa Serikali ina ushahidi dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi wa rada ila imeamua kuwalinda.

“Waupeleke serikalini ushahidi huo kama wanao ili ukalinganishwe, inawezekana ukawa tofauti na uliopo, hivyo kufanikisha kuwachukuliwa hatua watuhumiwa, hakuna mtu anayefurahia suala hilo,” alisema Feleshi.

Hata hivyo, Feleshi alibainisha kuwa ushahidi pekee hauwezi kumtia mtu hatiani isipokuwa ushahidi unaoweza kuithibitishia mahakama kuwa mshtakiwa ametenda kosa.

Alisema ni vema Chadema na watu wengine wanaodai kuwa wana ushahidi wa kutosha kuhusu ushiriki wa Chenge kwenye ufisadi wa rada wauwasilisha serikalini ili ufanyiwe kazi badala ya kulalamika nje ya utaratibu.

Kauli ya Mwanasheria Mkuu
Kauli hiyo ya DPP imeungwa mkono na Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Fredrick Werema, aliyesema kuwa nyaraka alizo nazo Dk Slaa kuhusu watuhumiwa wa rada zipo pia ofisini kwake, lakini hazina ushahidi wa kutosha kumtia Chenge hatiani.

Hata hivyo akinukuu Katiba ya nchi, Mwanasheria huyo Mkuu wa Serikali alisema ofisi yake siyo ya mwendesha mashtaka, hivyo haina mamlaka kuwashtaki watuhumiwa.

“Kuna mtu anayehusika na kazi hiyo, mimi siyo prosecutor (mwendesha mashtaka). Lakini uchunguzi ulifanyika na kuonekana kuwa ushahidi hautoshi kumtia Chenge hatiani,” alisema Werema na kuongeza:

“Ungekuwa karibu tungeangalia Katiba na tungesoma Ibara ya 59 Sehemu ya Kwanza, Tano hadi 60. Yupo mtu wa kufanya kazi hiyo ya uchunguzi.”

Ibara ya 59 ya Katiba, Sehemu ya Tatu inaeleza kazi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa ni kuishauri serikali juu ya mambo ya sheria na kwamba, yeye ndiye atakayeshughulikia mambo yote yahusuyo sheria yatakayopelekwa kwake au kazi atakazoagizwa na Rais na nyingine zinazokabidhiwa kwake kwa mujibu wa katiba.

Katiba imeeleza kuwa mwenye mamlaka ya kuendesha mashtaka ni Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na anafanya kazi hiyo akiwa huru bila kuingiliwa na mtu ama mamlaka yoyote.

Katiba inamtaja Mkurugenzi wa Mashtaka na Makosa ya Jinai katika Ibara ya 59(b), Sehemu ya Nne kuwa katika kazi zake hataingiliwa na mtu yeyote wala mamlaka yoyote na atafanya kazi kwa kuzingiatia nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma.Kazi zake ni kufungua, kuendesha na kusimamia mashtaka yote nchini.

Juzi ikiwa ni siku moja baada ya Serikali kumkingia kifua Mbunge wa Bariadi Mashariki (CCM), Andrew Chenge, ili asishtakiwe kwa rushwa katika mchakato wa ununuzi ya rada, Chadema imeweka hadharani kurasa 11 za ushahidi inaodai kuwa unaweza kumtia hatiani Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani kama atashtakiwa.

Ushahidi huo uliotolewa na Dk Slaa, ni ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Shirika la Upelelezi la Makosa Makubwa ya Jinai la Nchini Uingereza (SFO).

Dk Slaa aliwaambia waandishi wa habari kuwa amefikia hatua hiyo baada ya kusikitishwa na majibu ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, kuhusu suala hilo alipokuwa akijibu hoja za wabunge.

Kwa mujibu wa Dk Slaa, ukurasa wa tano wa ripoti hiyo, unaeleza jinsi Chenge alivyoshinikiza utekelezwaji wa mkataba huo na jinsi alivyofaidika kwa malipo ya kitita cha Dolaza Marekani 1.5 milioni kupitia akaunti ya Benki ya Barclays iliyoko katika kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza.

"Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kati ya mwaka 1995 na 2006. Katika kipindi hicho, BAE na SPS walikuwa wakifanya majadiliano ya ununuzi wa rada kwa ajili ya Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam na Chenge alihusika moja kwa moja katika mchakato huo hasa kushinikiza ununuzi huo," alisema Dk Slaa akinukuu waraka huo alioutoa pia kwa waandishi wa habari.

Aliendelea,"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilitakiwa kutoa maoni na kuthibitisha malipo hayo na bila Chenge kukubali, kusingeweza kufanyika chochote."

Kwa mujibu wa Dk Slaa, kauli ya Waziri Chikawe kuwa Serikali haina ushahidi unaowataja watuhumiwa wa kashfa ya rada moja kwa moja na kutaka mwenye ushahidi wauwasilishe kwake, ni hatari kwa kuwa inaonyesha kuwa haina dhamira ya kweli ya kushughulikia rushwa na ufisadi huo.

Alisema ripoti hiyo ya SFO, ambayo anaamini Serikali inayo, ni ushahidi tosha unaoweza kumtia hatiani Chenge ambaye pia angeweza kusaidia kutaja wahusika wengine katika sakata hilo.

Kauli ya Dk Hoseah
Katika katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hosea, alisema taratibu za kuwasilisha ushahidi ofisini kwake ziko wazi, hivyo kumtaka Dk Slaa kuuwasilisha kwake ili akaufanyie kazi.

Dk Hosea alisema Ofisi yake inafanya kazi saa 24, lakini inahitaji ushahidi na ndio sababu Kifungu cha 39 cha Sheria ya kupambana na rushwa Takukuru kinamtaka mtu yeyote mwenye ushahidi juu ya masuala ya rushwa kuwasilisha hapo.

Kuhusu hatua ambazo ofisi yake inafanya kuhusu tuhuma za rada ambazo juzi Dk Slaa alidai ana ushahidi, alisema swali hilo aulizwe waziri (Chikawe).

“Kwanini usimuulize waziri , yeye ndiye aliyetoa kauli hiyo (Statement) muulize huyo ndiye anaweza kuwa na majibu kuhusiana na hilo,” alisema Dk Hosea.

Alisema wao ni watendaji na si wanasiasa na kwamba, ofisi yake inafanya kazi kwa kufuata kanuni, taratibu na sheria zilizopo.

Alisema kama kunamtu mwenye ushahidi auwasilishe kwao nao wataufanyia kazi mara moja kwa sababu hiyo ndiyo kazi yao.

No comments: