TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, July 28, 2011

BUNGE HILI NI LA KITOTO, SAHIHI YA PINDA YAFOJIWA

WAZIRI MKUU Mh:Mizengo Kayanza Peter Pinda

VITUKO vya wabunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vimezidi kuongezekana; sasa baadhi ya wabunge wanadaiwa kugushi sahihi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa malengo ambayo bado hayajafahamika.

Kitendo cha kugushi sahihi ya Waziri Mkuu ndani ya ukumbi huo kunawaathiri zaidi wabunge wa upinzani, hasa wa Chadema ambao wamekuwa wakipelekewa ‘meseji’ za kuwadanganywa kuwa wanaitwa na Waziri Mkuu.

Juzi jioni kabla ya kikao cha Bunge kuahirishwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alilazimika kuomba mwongozo wa Mwenyekiti kukemea kitendo hicho alichokiita kuwa ni cha kihuni.

Lukuvi alisimama mara tu baada ya Bunge kumaliza kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ambayo yalikuwa yalijadiliwa kwa siku mbili mfululizo.

“Naomba mwongozo wako kwamba, humu ndani imejitokeza tabia ambayo naona imezoeleka kidogo. “Kuna watu wanawaandikia wenzao meseji za kuwasumbua kwamba wanaitwa na mtu fulani halafu wanaweka sahihi na wakati mwingine haitokei,” alisema Lukuvi na kuongeza:

“ Nimeisikia hayo wiki iliyopita, lakini leo Mheshimiwa Joseph Selasini (Chadema) ameitwa kwa meseji inayodaiwa kuwa imesainiwa na Waziri Mkuu na hii nyingine ameitwa Mheshimiwa Leticia Nyerere (Chadema) kwamba anaitwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu wakazungumze maneno ya maana, lakini Waziri Mkuu hana habari na wamegushi sahihi yake,’’ alisema Lukuvi.

Waziri huyo wa Sera, Uratibu na Bunge alitaka mwongozo wa Mwenyekiti kama jambo hilo linaweza kufanywa na Wabunge, ndani ya Bunge kwa wabunge kugushi taarifa ambazo alisema nyingine na zinatisha.

Mwenyekiti wa Bunge George Simbachawene alikiri kuwepo kwa tabia hiyo ndani ya ukumbi wa bunge ambayo imekuwa ikifanywa na baadhi yao na kamba inaonekana kuota mizizi.

“Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, ni kweli kuna mtu amefanya hivyo na karatasi aliyoiandika ipo hapa, Kwa kweli siyo nzuri haionyeshi kama tupo serious (makini) na kazi,” alisema Simbachawene na kuisoma:

“Amemwandikia hivi, Mheshimiwa Joseph Selasini Mbunge, samahani nakuomba mara moja tuje tujadili suala moja muhimu ambalo ningependa kujua kutoka kwako. Ahsante. Mizengo Peter Pinda na sahihi”.

Simbachawene alisema Selasini alipokwenda kwa Waziri Mkuu alishindwa kusaidiwa kwa kuwa wakati huo Waziri Mkuu alikuwa makini kusikiliza hotuba ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika katika majumuisho yake.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo alisema uongozi wa Bunge utafanya kila liwezekanalo kubaini ni nani mwenye tabia hiyo na kwamba ili kukomesha vitendo hivyo.

No comments: