TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, June 30, 2011

Wanafunzi Udom warejeshwa, wengine waachwa



CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimetangaza kuwarejesha wanafunzi wa mwaka wa tatu waliokuwa wamesimamishwa masomo, huku wanafunzi 15 wakiwekwa kando hadi hapo watakapoarifiwa.
Wanafunzi hao wa chuo cha sanaa na sayansi za jamii walisimamishwa masomo tangu Juni 14 mwaka huu, baada ya kugoma na kuandamana kwa madai mbalimbali.

Wananfunzi hao waliandamana kushinikiza kujiuzulu kwa viongozi waandamizi wa Serikali akiwamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kwa madai kwamba wamewadanganya kuhusu malipo yao ya masomo kwa vitendo.
Taarifa iliyotolewa na Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Idris Kikula kupitia tangazo lake katika tovuti ya chuo hicho, imewataka wanafunzi hao kuripoti chuoni hapo kesho, huku litikaja siku ya mwisho ya kujisajili kuwa ni keshokutwa Julai 3 saa 4:00 asubuhi.

“Wanafunzi wote wa mwaka wa tatu Chuo Cha Sanaa na Sayansi za Jamii, waliosimamishwa masomo, wanajulishwa kwamba, wanatakiwa kuripoti chuoni siku ya Jumamosi (kesho),tarehe 2, Julai saa 4:00 asubuhi," ilieleza taarifa hiyo ya makamu mkuu wa chuo.

Udom imetangaza kuwa mitihani kwa wanafunzi hao itaanza Jumatatu ya Julai 4, 2011, huku ikielekeza eneo la kufanyia usajili kwa wanafunzi hao kuwa lililotengwa katika uwanja wa mpira wa miguu mita 200 kutoka Ofisi za Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka mjini Dodoma (Duwasa).

Imefafanua kwamba kila mwanafunzi anatakiwa kuripoti chuoni hapo akiwa na nakala halisi ya vithibitisho vya malipo ya ada na gharama nyingine, ikionya kuwa atakayeshindwa kutekeleza masharti hayo hatapokelewa.

Wengine wawekwa kando
Hata hivyo, taarifa hiyo imetaja majina ya wanafunzi 15 ambao hawatarejea chuoni hapo huku wengine ambao hawatapokelewa kuwa ni wale ambao wanadaiwa ada, gharama za malazi, mitihani na gharama nyingine.
Taarifa hiyo ya Profesa Kikula ilisema kuwa wanafunzi hao ambao hawatarejea watapewa taarifa zao binafsi na mamlaka husika.

"...isipokuwa wanafunzi wafuatao: (A) Wale ambao wanadaiwa ada, gharama za malazi, mitihani na gharama nyingine. (B) Hawa 15 waliotajwa hapa chini ambao watapewa taarifa zao binafsi na mamlaka husika,” ilifafanua taarifa hiyo.Imewataja wanafunzi hao kuwa ni pamoja na Tindo Salum, Tairo Edwin, Ngaiza Paschal, Messo Baraka, Melchiory Very na Emmanuel Vicent.

Wengine ni pamoja na, Boniface Alfrey, Mushi Alex, Msangi Geofrey, Julius Samora Mnyonga, Baradyana Romano, Goodness Moses, Seleman Bakari Katanga, Ally Hassan na Shaaban Mustafa.

Juni 14 chuo hicho kiliwafukuza zaidi ya wanafunzi 9,000 wa kwa madai ya kuhamasisha mgomo usio halali na kwamba uongozi wa chuo uliwataka wanafunzi hao kuondoka kabla ya saa 8:00 mchana.
Hata hivyo, baada ya amri hiyo, Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), walionekana wakiwa wanarandaranda katika maeneo ya chuo hicho hali ambayo ilichangia wanafunzi hao kuharakisha kuondoka chuoni hapo wakihofia kukumbana na kipigo.

No comments: