TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Monday, June 20, 2011

Vikongwe wafunga ndoa ya kihistoria Rukwa

WAZEE wawili wakazi wa Mji wa Namanyere wilayani Nkasi, mkoani Rukwa, wameandika historia ya pekee ndani na nje ya nchi kwa kufunga ndoa wakiwa na umri mkubwa kuliko kawaida.

Wazee hao, Mathias Kisokota (94) na Uria Mwimanzi (80) walifunga ndoa hiyo ya kihistoria katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Antony, Parokia ya Namanyere wilayani Nkasi mkoani Rukwa.

Ibada ya ndoa hiyo iliyofungwa jana, iliongozwa na mapadri wawili ambao ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Katindi na Twamba Peter.Ndoa hiyo ilivuta hisia za watu wengi kiasi cha kufurika katika kanisa hilo kwa lengo kushuhudia wazee hao wakifunga ndoa.

Kabla ya Ibada hiyo kufanyika nyakati za saa tisa mchana, gumzo katika Mji wa Namanyere, Sumbawanga na Mpanda ilikuwa ni juu ya kufungwa kwa ndoa hiyo ambapo wakazi wa mjini humo walisikika wakieleza kuwa hii itakuwa historia kwa wazee kufunga ndoa wakiwa na umri mkubwa kiasi hicho.

Wazee hao ambao wamefunga pingu za maisha kwa kuamua kuwa mwili mmoja kama maandiko ya vitabu vya dini yanavyoeleza, wana watoto wapatao 10 na wajukuu zaidi ya 50 ambapo walianza kuishi pamoja miaka 35 iliyopita baada ya kufariki mke wa kwanza aitwaye Agnes Kasinsila.

Hata hivyo baada ya mzee Kasokota ambaye ni Mkatoliki kuanza maisha mapya Uria anayesali Kanisa la Moravian mpaka sasa, waliendelea kusali kama kawaida, lakini wakikosa baadhi ya huduma za kanisa.

Katika mahubiri yake kanisani hapo, Padri Twamba alisema kuwa hiyo ni changamoto ya uwokovu hasa kwa vijana kubadilika kitabia na kutenda matendo mema na ya kumpendeza mwenyezi Mungu hasa kipindi hiki ambacho Jimbo Katoliki Sumbawanga linajiandaa kusherekea Jubilee ya miaka 125 tangu kuanzishwa kwake.

"Hii ni changamoto ya uokovu hasa kwa vijana kubadilika kitabia na kutenda matendo mema ya kumpendeza Mungu..... ni faraja kwetu katika umri wa wazee hawa wameamua kufanga ndoa, tena kipindi ambacho tunajiandaa kusherekea Jubilee ya miaka 125 tangu kuanzishwa kwa jimbo
letu," alisema Padri Twamba.

Mjomba wa wazee hao ambaye ndiye msemaji wa familia hiyo, Filibert Lumbert alisema wazee hao pamoja na kwamba wameanza kupoteza baadhi ya kumbukumbu muhimu katika akili zao, lakini walisisitiza kila mara
kwamba lazima wafunge ndoa kanisani ili waweze kupata huduma zote muhimu za kanisa kama ilivyo kwa Wakristo wengine hususani Wakatoliki.

Huduma ambazo wamekuwa wakizikosa ni pamoja kupokea mwili wa Kristu (Sakramenti takatifu) na pia waliamini wakiendelea na maisha ya bila ndoa wanaweza kuzikwa nje ya makaburi ya Wakristo wakatoliki kitu ambacho si sahihi kwao.

Hata hivyo ndoa ya wazee hao ambayo ilifana sana, sherehe zake hazikuishia kanisani badala yake zilikwenda hadi ukumbini ambako watu waliwapongeza kwa kuamua kufanya tendo hilo muhimu katika
maisha ya wanadamu.

No comments: