TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Thursday, June 23, 2011

Posho: Bunge sarakasi tupu


Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu

Ulikuwa mpambano wa Lissu, Zitto na Mnyika
Serikali, wabunge wake wafanya kazi ya ziada

Pendekezo la kusamehe kodi kwa posho za watumishi wa umma limelipua Bunge kiasi cha kuzua malumbano makali kati ya kambi ya upinzani na ule wa chama tawala ukitetea serikali katika pendekezo hilo.

Mpambano huo ulikuwa kama timu mbili za mpira, upande mmoja ukiwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) na upande wa pili mawaziri na wabunge wa chama tawala.

Katika malumbano hayo, wabunge walijikuta wakirushiana vijembe, kuzomea huku wengine wakiwasha vipaza sauti bila kufuata utaratibu, hali iliyomfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuwa katika wakati mgumu kudhibiti hali ya mambo.

Hali hiyo ilisababishwa na Lissu aliyewasilisha mapendekezo ya kubadili muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2011/12 kwa kufuta kifungu kilichokuwa kinapendekeza posho zote wanazopewa watumishi wa serikali zisitozwe kodi, kwa kuwa ni kinyume cha mkakati wa serikali wa kuachana na matumzi makubwa yasiyokuwa ya msingi kama ilivyoanishwa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano.

Lissu alifafanua kuwa kuendelea kuwasamehe kodi ya mapato watumishi hao, ni sawa na kuzidi kuwaongezea walichonacho, na si kuwaangalia wale wa kipato cha chini kwa sababu watumishi wa chini hakuna anayelipwa posho inayofikia Sh. 100,000 ambacho ndicho kima cha kuanza kukatwa kodi kisheria.

Pandekezo la Lissu lilipingwa na wabunge kadhaa, akiwamo Jenista Muhagama (Peramiho- CCM), George Simbachaweni (Kibakwe-CCM), Nimrod Mkono (Musoma Vijijini - CCM), Peter Serukamba (Kigoma Mjini – CCM), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, wote wakipinga mapendekezo hayo.

Tofauti na wenzake, Lukuvi alisema kuwa mawazo ya Lissu ni chanya kulingana na mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa serikali, lakini ni vema kukawa na utaratibu mpana wa kuchambua makundi mbalimbali katika jamii na si kuibuka tu na msimamo wa kukurupuka kama ambavyo inapendekezwa na Lissu kwa sababu madhara yake yanaweza kuwa mabaya zaidi kwa watumishi wengine.

Moto wa mabishano ulizidi kuwaka baada ya Mkono kusema kwamba mapendezo ya Lissu yangewaumiza madiwani ambao wanalipwa posho lakini hawana mishahara.

Kutokana na kauli ya Mkono, mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alisimama na kueleza kuwa kinachozungumzwa na baadhi ya wabunge kuwa msamaha huo wa kodi utawasadia watu wa kipato cha chini, wakiwamo walimu, madiwani, askari polisi na kada nyingine za chini, si za kweli kwa sababu katika kundi hilo hakuna anayelipwa posho ya Sh. 100,000.

Zitto alisema kuwa msamaha huo utawasaidia na kuwanufaisha zaidi wakubwa serikalini, wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu na hata wabunge ambao tayari wana mapato makubwa wakilinganishwa na watumishi wengine.

Akijibu hoja hizo, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, alisema kwamba haoni sababu ya malumbano bungeni kwa sababu fedha yenyewe inayotokana na msamaha huo ni ndogo mno.

Alisema isije kuwa wanaowasilisha marekebisho hayo wanasukumwa tu na hoja ya posho, lakini kimsingi hakuna hasara kubwa kwa serikali kwa kutoa msamaha huo.

Lissu alipopewa fursa ya kujibu hoja wa wabunge alimweleza Mkono kama kipofu wa sheria kwa sababu suala la madiwani alilichomeka tu kwenye mjadala huo kwa kuokota maneno.

Lissu alihoji kwamba ni diwani gani analipwa posho ya wajibu, posho ya nyumba, posho ya matibabu na nyingine kama si wakubwa serikali na wabunge ambao tayari wana mishahara mikubwa ya mamilioni.

Kauli ya Lissu kuwa wabunge wanalipwa mshahara wa Sh. milioni 3.5 ililipua zaidi wabunge na wengi waliwasha vipaza sauti na kutaka kutoa taarifa, hata hivyo Spika Makinda wakati huo akiwa ni mwenyekiti wa kamati ya Bunge zima kupitisha vifungu vya sheria, aliwakatalia na kuwataka waache vurugu na kujirusha bungeni.

Lissu alihitimisha hoja yake kwa kusema kuwa kimsingi hakuna ufanisi wowote utakaopatikana kwa kukataa kulipa kodi kwa kuwa wanaolengwa ni wakubwa ambao tayari wana mapato makubwa.

Naye Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Khamisi Kigwangallah, aliomba mwongozo wa Spika juu ya kauli ya Lissu kwamba wabunge wanalipwa mshahara wa Sh. milioni 3.5 wakati anavyojua yeye na kwa mujibu wa salary slip yake mshahara wa wabunge ni Sh. milioni 2.3.

Hata hivyo, Makinda alisema kuwa mshahara wa mbunge ni Sh. milioni 2.3 pamoja na kodi.

Mpambano wa jana jioni kwa ujumla mali na Lissu na Zitto, pia uliwahusisha mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, ambaye aliwasilisha mapendekezo kadhaa ya kubadili muswada huo, lakini kama ilivyo kwa mapendekezo kadhaa ya Lissu yalikataliwa kwa wingi wa wabunge wa CCM.

No comments: