TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Sunday, June 26, 2011

Mbunge aliyezirai bungeni aruhusiwa hospitalini


Mwanakhamis Kassim Said (MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM))

MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM), Mwanakhamis Kassim Said, aliyeanguka bungeni juzi na kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu, amepata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Habari zilizopatikana mjini hapa na kuthibitishwa na Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, zilisema mbunge huyo aliruhusiwa jana asubuhi baada ya madaktari kujiridhisha kuwa afya yake ni mzuri.

"Mbunge ameruhusiwa kutoka hospitalini na afya yake inaendelea vizuri, "alisema Joel alipoulizwa na gazeti hili jana asubuhi katika viwaja vya Bunge mjini Dodoma.

Juzi mbunge huyo alianguka ghafla wakati wabunge walipokuwa wakiendelea na mjadala kuhusu bajeti ya Waziri Mkuu na kuzua tafrani ndani na nje ya ukumbi wa bunge.

Alianguka wakati Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, alipokuwa akitoa mchango wake katika mjadala huo uliokuwa ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mapumba.

Wabunge kadhaa wakiongozwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Sera na Uratibu), William Lukuvi, walikuwa wakihaha hapa na pale kutafuta msaada kwa ajili ya mbunge huyo aliyekuwa amepoteza fahamu kabla kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Wakati wabunge hao na wafanyakazi wengine wa Bunge wakiwa wanahangaikia huduma ya kwanza kwa mgonjwa huyo, vurugu kubwa iliibuka baina ya waandishi wa habari na askari polisi waliokuwa wakiwazuia kupiga picha.

Vurugu hizo zilisitishwa na Waziri Lukuvi ambaye aliingilia kati na kuwataka waandishi kuacha kulumbana na askari na kusisitiza kuwa wakiwa bungeni wanapaswa kutambua kuwa wko chini ya Sheria ya Bunge.

"Ni vema ndugu zangu waandishi mkawasikiliza hao askari. Msione mmepewa vitambulisho hivyo, mjue kuwa mkiwa humu ndani, mnaongozwa na sheria ya bunge, sheria zingine zote zinaanza kufanya kazi mkiwa nje ya fensi ya Bunge,"alisema Lukuvi.

No comments: