TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Wednesday, June 22, 2011

Mbowe alichachafya Bunge, Atoa miezi sita mashangingi yauzwe, posho zifutwe



KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ametaka yafanyike mabadiliko ya sera na sheria ili kuwezesha kuondolewa kwa posho kwa wabunge na watumishi wa umma na ununuzi wa magari ya kifahari ili fedha hizo ziwanufaishe Watanzania wote.

Akizungumza bungeni jana wakati akichangia hoja ya Bajeti ya Serikali, Mbowe alisema; "Tunachotaka Chadema sio kuwafutia wabunge posho, bali ni kufanya mabadiliko ya msingi katika sera zinazohusu posho," alisema Mbowe na kusisitiza:

“Tunapofanya uamuzi tukiangalia maslahi ya wabunge 350, tutakuwa tunakosea. Posho hawapokei wabunge pekee, kuna taasisi nyingi za umma na serikali ambako wanalipana zaidi ya shilingi milioni moja kama posho. Hatuwezi kujenga taifa kwa kulipana posho kubwa namna hii.

"Wabunge hapa tunakazania kulipana posho kwa sababu ya umaskini, lakini tunaishi kitajiri. Ni kweli ‘sitting allowance’ (posho za vikao) za wabunge sio nyingi, lakini posho na semina siyo suluhisho. Tukitaka tuangalie pia mishahara na si kung'ang'ania posho.".

Kwa mujibu wa Mbowe, posho, semina, ununuzi wa magari ya kifahari kwa viongozi wa serikali na wabunge na kusafiri kwa ndege kwenye madaraja ya juu vinachangia kuongeza umaskini wa nchi.

Mbowe alisisitiza kuwa vitu hivyo vinapaswa kufutwa haraka na fedha hizo zipelekwe kwenye maeneo ambayo yatakuwa ni ya manufaa kwa Watanzania walio wengi.Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai na mwenyekiti wa Chadema ameitaka serikali ifanye uamuzi wa haraka wa kuyapiga mnada mashangingi yote yaliyonunuliwa na serikali kwa ajili ya vigogo serikalini.

"Hii ni nchi ya ajabu sana, watumishi wa umma tunajichana na magari mapya na kusafiri kwa ‘first class’ (daraja la kwanza) katika ndege, tunatumia dola za Marekani 6,000 kutoka Tanzania kwenda Washington DC (Marekani) badala ya dola 1,000 kwenye ‘economy class’ (daraja la kawaida lisilo la gharama kubwa) kutegemeana na msimu!

“Tuna raha gani katika nchi maskini kama hii? Tujiulize, tukiondoka kwenye nafasi hizi tunaweza kuendelea kuponda raha hizi?" alihoji Mbowe na kuendelea:

"Rais anatembelea landcruiser, makamu wake ana la kwake, Waziri Mkuu naye analo, wabunge tumepewa Landcruiser, mkuu wa mkoa ana landcruiser, DC naye analo na hata wakurugenzi wote wa halmashauri wanatembelea landcruiser!

“Hivi tuna hadhi gani hasa sisi hata tunaponda raha kiasi hicho? alihoji Mbowe na kuongeza kuwa ili kutatua tatizo hilo ni kwa serikali kuamua kuuza magari hayo na fedha zake zitumike kuwanasua Watanzania na uduni wa maisha duni unaowakumba wengi.

“Magari hayo tuyapige mnada ndani ya miezi sita ili fedha zikanunue ambulance (magari ya kubebea wagonjwa )na kufanya shughuli zingine za maendeleo halafu viongozi hao wakopeshwe fedha wakanunue magari yao. Kama ni lazima kuendelea na magari hayo, basi wawe ni viongozi wakuu tu wa nchi."

Kwa mujibu wa Mbowe, ni jambo lisilokubalika kwa viongozi wa nchi kutumia magari hayo ya anasa huku nchi ikiendeshwa kwa misaada kutoka kwa wahisani ambao wenyewe, hawaishi maisha hayo ya kifahari.Mbowe alisema wakiwa viongozi, wabunge na viongozi wengine wa serikali wanatakiwa kujifunza kufanya maamuzi magumu ya kuacha kujilipa posho za vikao na kutumia magari hayo ya kifahari kwani kinyume chake hawalitendei haki taifa.


Alisema kama tatizo ni udogo wa mishahara, anaamini sio kwa wabunge tu bali ni kwa watumishi wote wa umma, hivyo kundi hilo dogo kujilipa posho huku asimilia kubwa wakiishi kwa kutegema mishahara, siyo uzalendo.

Pia, alisema msimamo wa chama chakeni kufutwa kwa posho za vikao vya watumishi wa umma na si wabunge pekee kwani wabunge ni kada ndogo tu inayofaidika na posho hizo, tofauti na baadhi ya watu wanavyotaka kupotosha ukweli kuwa chama hicho kinataka kuwafutia wabunge posho.


"Mheshimiwa spika, hivi karibuni kumekuwa na mvutano mkali sana humu bungeni kuhusu suala la posho. Na mimi nikiwa mwenyekiti wa chama na kiongozi wa kambi ya upinzani, ninaona leo nitumie muda wangu kulifafanua hili ili wabunge tutumie busara zetu kupima," alisema Mbowe na kuongeza:

"Kama viongozi tunaojadili mustakabali wa nchi, tunapaswa kujifunza kufanya uamuzi mgumu na tuwe ‘victim’ (waathirika) wa kwanza na kama tutashindwa kufanya hivyo, tutakuwa hatulitendei haki taifa hili.


"Nasema tunachotaka sisi si kuwafutia wabunge posho, ni kufanya mabadiliko ya msingi katika sera zinazohusu posho. "Tuna halsmahauri 133 za wilaya na ukienda unaambiwa viongozi wapo kwenye semina ya Ukimwi. Mimi nasema leo kwamba, kama mpaka leo kuna kiongozi asiyejua madhara ya ukimwi hata akahitaji semina, hatufai," alieleza Mbowe.

Alisema kuwa baadhi ya vitu vingine vinavyokuwa vya matumizi mabaya ya fedha za umma serikalini ni utengenezaji wa kofia, fulana na mikoba kwa ajili ya semina na wajumbe.Kauli hiyo ya Mbowe iliyotolewa mwishoni mwa mjadala wa bajeti ya serikali ya mwaka 2011/2012, inaonekana kama msumari wa mwisho katika suala hilo lililoanza kujadiliwa tangu mwanzo wa kikao hiki cha nne cha bunge la bajeti.

Mbali na hoja hiyo ya posho, juzi Mbunge wa Chadema (Viti Maalumu), Esther Matiko aliibua hoja mpya baada ya kulitaka bunge lisitishe malipo ya nauli kwa wabunge ili kuipunguzia serikali mzigo.

Akichangia katika mjadala wa hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2011/2012 uliokuwa ukiendelea bungeni, Matiko alisema wabunge wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuisaidia serikali katika kupunguza matumizi yake.

Mbali na wabunge hao kupinga, serikali kupitia Waziri Mkuu Mizengo Pinda Alhamisi ilitoa msimamo wake ikisema suala la posho za wabunge lipo kwa mujibu wa sheria na kuziondoa pia zinahitaji utaratibu wa kubadilisha sheria hiyo.

No comments: