TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Saturday, May 28, 2011

SIMBA YASEMA MTATUTAMBUA CASABLANCA



WACHEZAJI WA SIMBA WAKIFANYA MAZOEZI JANA KUJIANDAA NA MECHI DHIDI WYDAD CASABLANCA MJINI CAIRO.

SIMBA ya Tanzania imeitamkia Wydad Casablanca neno moja tu; "Mtatumbua.'Wekundu hao wanaoonekana kujiamini kupita kiasi wana kazi moja tu leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Petrosport jijini hapa, kuifunga Wydad ya Morocco, saa 1.00 usiku katika mechi ya mtoano kuwania kufuzu hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mechi hiyo, ambayo kwa muda wa hapa itaanza saa 12.00 jioni sawa na saa 1.00 usiku kwa saa za Tanzania, imegubikwa na mambo mengi huku kila timu ikiwa imejizatiti kulinda heshima yake na kupata ushindi.

Simba ambayo iliwasili jijini hapa mapema juzi Alhamisi imekuwa gumzo katika mitaa mbalimbali kutokana na mambo mengi, kwanza maumbo madogo ya wachezaji wake, rangi nyeusi pamoja na mashabiki wa Zamalek ambao wanakumbuka kipigo cha mwaka 2003.

Wachezaji wakiongozwa na kipa mahiri Juma Kaseja pamoja na viongozi wote wa juu wa Simba na Kocha Mkuu Mosses Basena, wameonyesha kujiamini kuanzia mazoezini mpaka kambini huku wakibadilishana mbinu tofauti na kushauriana.
Silaha zote za Simba ziko kamili kwa mchezo huo huku viongozi wakionekana kufanya jitihada za kila namna kuhakikisha usalama wa wachezaji na kwamba hakuna adui yeyote anayeingia kambini au kusumbua wachezaji kisaikolojia ingawa mashushushu wa Waydad wameonekana wakifuatilia nyendo za Simba tangu juzi Alhamisi jioni.

Wydad, ambao kikosi chao kilitarajiwa kuwasili Cairo jana Ijumaa asubuhi na kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Petrosport, imeripotiwa kuwa wametuma mashushushu wao mapema mjini hapa kufanya mipango mbalimbali mara tu baada ya CAF kutangaza kwamba watakutana na Simba.

Si hapa, mitandao mbalimbali ya Morocco pamoja ule wa klabu hiyo imeripoti kwa lugha ya Kiarabu kwamba viongozi wake Wydad walikuwa wakifuatilia ilichokuwa ikifanya Simba usiku na mchana kabla haijatoka Dar es Salaam mpaka inatua Misri, jambo ambalo linaashiria wanaihofia.


MAZOEZI
Uwanja ilipofanyia mazoezi na ambako mechi itachezwa umejengwa kisasa miaka mitatu iliyopita. Basena juzi Alhamisi alitumia saa tatu kuwapa mazoezi ya nguvu wachezaji wake ambayo yalianza saa 11:45 jioni hadi saa 1:45 usiku na wachezaji bado wakaonekana na ari kubwa ingawa baadhi walilalamikia hali ya hewa ya Cairo ni nzito hivyo kuwajaza vifua.

Basena alikuwa na kazi moja uwanjani, kuwatengeneza washambuliaji kupiga mipira langoni, lakini bado baadhi ya wachezaji walipoteza nafasi nyingi. Walioongoza kupoteza mashuti ni Mussa Hassan `Mgosi', Mohamed Banka, Hillary Echessa huku Aziz Gilla na Shija Mkina waking'ara.

Basena aliwasisitiza wachezaji wake kukaba kwa nguvu na kutowaruhusu Wydad kuingia kwenye eneo la hatari. Kocha huyo aliridhika na kasi na viwango vya wachezaji wake na kusema; "Ni kipindi kifupi, lakini kwa hali ninayoiona kwa wachezaji inanipa moyo sana, tunaweza. Matumaini ya ushindi ni makubwa, sasa hapa kinachosubiriwa ni filimbi ya mwisho."
Nahodha wa Simba, Nico Nyagawa sambamba na Amir Maftah, Juma Kaseja wamesisitiza kuwa watafanya vitendo uwanjani kuhakikisha Simba inapata ushindi kwa kuwa wanaelewa umuhimu wa mchezo huo kwao na Taifa la Tanzania.

Jana usiku, Balozi wa Tanzania hapa, Shauri Haji, alikutana na wachezaji wa Simba na kuwatakia kila kheri katika mchezo huo.

KIKOSI
Kwa mujibu wa mazoezi Simba inaweza kuanza hivi; Juma Kaseja, Salum Kanoni, Amir Maftah, Kelvin Yondan, Juma Nyosso, Jerry Santo, Haruna Shamte, Mohamed Banka, Emmanuel Okwi, Hilary Echessa na Shija Mkina.

HISTORIA
Simba kila inapopita kuanzia itue jijini hapa imekuwa ikijadiliwa. Shughuli zilisimama kila mahali walipopita wachezaji wa Simba, kwenye Uwanja wa Ndege, baadhi ya watu walikuwa wakiuliza "Hii timu gani...timu gani weusi hivi?" Ni maswali yaliyokuwa yametawala vichwa vya baadhi ya watu ambao uchunguzi ulionyesha ni mashabiki wa Al Ahly na Zamalek.

"Aah Simba iliyoitoa Zamalek.." alisikika mmoja wa mashabiki alipopatiwa jibu na mmoja wa maofisa wa ubalozi aliyekuwa akimuuliza kwa Kiarabu. Katika duka moja la kuuza vifaa vya simu, mmoja alihoji kama ilivyokuwa Uwanja wa Ndege wa Cairo, kuwa "Ni Simba iliyoitoa Zamalek?"

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki walikuwa wakishangaa Simba na Wydad kucheza Misri na wengine hawafahamu kwanini mechi hiyo ipo hapa leo Jumamosi.

Simba iliitoa Zamalek na kuingia hatua ya makundi mwaka 2003 ilipoifunga timu hiyo bao 1-0 jijini Dar es Salaam kabla ya kufungwa 1-0 mjini na mikwaju ya penalti kutumika kuamua mshindi.

Juma Kaseja, mchezaji pekee aliyeko Simba, aliyecheza mechi hiyo, aliokoa penalti moja katika mchezo ambao Simba iliitoa timu hiyo kwa penalti 3-2 na kuivua ubingwa.

UWANJA
Viongozi wa Simba walisema jana kuwa wamepata jibu la aina ya uwanja wa kujenga, kwani itajenga unaofanana na Petrosport wa hapa katika mipango yake.
Viongozi wa Simba waliukagua uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 12,750 na kuridhika na kiwango na kuchukua ramani yake.

No comments: