TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Friday, May 27, 2011

Mataka: Mkapa amenikera, ATANGAZA KUSTAAFU UKURUGENZI ATC, ALIACHA BILA YA HATA NDEGE HATA MOJA

Mataka: Mkapa amenikera

• Atangaza kustaafu ATC, aliacha bila ndege hata mojaMKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), David Mataka, ametangaza kustaafu, huku akimtupia lawama Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kwamba alimkwaza kwa kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi wa kashfa dhidi yake wakati akiwa Mkurungenzi wa Mfuko wa Mashirika ya Umma (PPF).

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam jana, Mataka alitumia muda mwingi kuelezea historia yake tangu serikali ya awamu ya kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, hadi serikali ya sasa chini ya Rais Jakaya Kikwete.

Alisema hajafukuzwa wala kuacha kazi ATC, bali ameamua kustaafu kwa mujibu wa sheria baada ya muda wake kufika. Mataka alizaliwa Mei 11, 1951 na Mei 11 mwaka huu alitimiza umri wa miaka 60.

Alisema anamshukuru Mungu kwamba amekuwa mkurugenzi katika mashirika mbalimbali katika vipindi vyote vinne vya serikali na alipata mafanikio makubwa isipokuwa ATC.

Alielezea kashfa alizopata kipindi cha Mkapa akiwa mkurugenzi wa PPF, Mataka alisema tuhuma dhidi yake zilikuwa za kupikwa, lakini alishangazwa na jinsi Mkapa alivyochukua uamuzi wa kumsimamisha.

“Kwa kweli Rais Mkapa alinikwaza sana, nilijisikia vibaya kama binadamu. Niliumia sana sana, lakini nikaona nikae kimya, tume iliundwa kunichunguza, PCCB ikanichunguza, Jeshi la Polisi nalo, lakini hawakubaini chochote, ndipo Rais Mkapa alipoamua kunirudisha tena kazini na kuamua kunisafisha,” alisema Mataka.

Alisema kashfa hizo zilitokana na yeye (Mataka) kuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza kwani Mwalimu Nyerere ndiye aliyemteua kuwa mkurugenzi Bima ambayo baadaye ilizaa PPF.

“Mwalimu Nyerere, Mungu ailaze roho yake Mahala Pema Peponi, Amina. Ndiye aliyenisomesha na baadaye kuniteua kuwa mkurugenzi wa Bima na baadaye kuzaliwa PPF. Nilifanya mambo mengi yenye mafanikio, ikiwa ni pamoja na kujenga majengo ya PPF Tower, PPF House na Kijiji cha Arusha.

Alitaja sababu ya pili ya kupakwa matope katika kashfa hiyo kuwa ni tabia yake ya kutojificha katika maisha yake kwani anapenda kuishi maisha ya raha na aliweza kununua magari yaliyotokana na mshahara wake wa sh milioni 3.5 ambao kwa wakati huo ulikuwa mkubwa sana.

“Mnajua mimi sipendi kujificha, nilikuwa na magari matatu aina ya Nissan Patrol, Toyota Grand Vitara na Benzi. Watu wakanizulia maneno na kashfa wakidai kuwa natumia fedha za miradi ya majengo ya PPF wakati sio kweli. Wakati huo mshahara wangu ulikuwa sh milioni 3.5, ulikuwa mkubwa sana na nilikuwa na uwezo wa kuishi vizuri na zilinisaidia sana kipindi nilichosimamishwa,” alisema Mataka.

Kwa mujibu wa Mataka, nafasi yake kwa sasa inashikiliwa na William Haji kama Kaimu Mkurugenzi hadi hapo Rais Jakaya Kikwete atakapofanya uteuzi mwingine.

Kuhusu hali ya kifedha ya Shirika la Ndege la Taifa la ATC, Mataka alisema, lina hali mbaya kwani anaondoka na kuliacha likiwa halina hata ndege moja inayofanya safari zake.

Alisema hali hiyo imetokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake hasa baada ya serikali kuacha kutoa ruzuku ya sh milioni 500 kila mwezi.

Mataka anasema moja ya mambo anayojivunia akiwa ATC ni kufanikiwa kuliondoa shirikia hilo kwenye ubia na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (S.A).

Alisema ubia huo ulisababisha utegemezi mkubwa wa S.A ambayo kutokana na utegemezi huo, iliamua kutumia nembo ya kwao badala ya ile ya ATC.

Mkurugenzi huyo mstaafu alisema anafurahishwa na hatua ya serikali kurejesha matumaini kwa ATC ya kutaka kulikwamua katika mazingira ya sasa ya kutokuwa na ndege hata moja.

No comments: