TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE
Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com
Friday, April 20, 2012
Tume Ya Katiba: Tamko La Kituo Cha Haki Za Kibinadamu
Dr. Helen Kijo-Bisimba Mkurugenzi mtendaji- LHRC
Ndugu wanahabari na wananchi kwa ujumla,
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tumefuatilia kwa makini sana mchakato wa Katiba mpya kuanzia ulipoanza mpaka hapa ulipofikia.
Sote tunafahamu kwamba hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kuteuliwa na kuapishwa kwa wajumbe wa tume ya kukusanya maoni juu ya mchakato mzima wa Katiba mpya na namna ambavyo wananchi wangependa iwe.
Tunependa kupompongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali kupitia wizara ya Katiba na Sheria kwa hatua iliyofikiwa mpaka sasa kwenye mchakato mzima.
Tunatoa pongezi kwa uteuzi wajumbe wengi waliobobea katika fani mbalimbali za Sheria, Siasa na Masuala ya kijamii. Tumefurahi kuona kuwa Mheshimiwa Rais amemteua kuwa mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Sinde Warioba ambae tulishaona kazi yake nzuri hususan pale alipoongoza vizuri tume ya Rais iliyohusu masuala ya Rushwa. Tuna imani kuwa ataongoza tume hii kufanya kazi nzuri.
Wajumbe wa Tume hii ni 32 (akiwemo mwenyekiti na makamu) waliapishwa tarehe 13/04/2012.
Wajumbe hao ni kama ifuatavyo;
Mwenyekiti wa Tume ambaye ni Jaji Sinde Warioba na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Agustino Ramadhani.Wajumbe wa tume toka Tanzania Bara ni Prof. Mwesiga L. Baregu, Nd. Riziki Shahari Mngwali, Dr. Edmund Adrian Sengodo Mvungi, Nd. Richard Shadrack Lyimo, Nd. John J. Nkolo, Alhaj Said El- Maamry, Nd. Jesca Sydney Mkuchu, Prof. Palamagamba J. Kabudi, Nd. Humphrey Polepole, Nd. Yahya Msulwa, Nd. Esther P. Mkwizu, Nd. Maria Malingumu Kashonda, Mhe. Al-Shaymaa J. Kwegyir (Mb), Nd. Mwantumu Jasmine Malale Na Nd. Joseph Butiku. 2
Wajumbe wengine 15 ni kutoka Tanzania Zanzibar. Wajumbe hao ni Dkt. Salim Ahmed Salim, Nd. Fatma Said Ali, Nd. Omar Sheha Mussa, Mhe. Raya Suleiman Hamad, Nd. Awadh Ali Said, Nd. Ussi Khamis Haji, Nd. Salma Maoulidi, Nd. Nassor Khamis Mohammed, Nd. Simai Mohamed Said, Nd. Muhammed Yussuf Mshamba, Nd. Kibibi Mwinyi Hassan, Nd. Suleiman Omar Ali, Nd. Salama Kombo Ahmed, Nd. Abubakar Mohammed Ali na Nd. Ally Abdullah Ally Saleh.
Mapungufu tunayoyaona;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunaona mapungufu makubwa mawili kwa tume hii
i) Kuwemo kwa mbunge na mjumbe wa baraza la wawakilishi
ii) Uwakilishi finyu wa kijinsia na makundi mengine mfano vijana
Wawakilishi kuwa wajumbe
Kituo hakikubaliani kabisa na uteuzi wa wakilishi wa wananchi (Mbunge na Mjumbe wa Baraza la wawakilishi). Wajumbe hawa ni Mhe. Al-Shaymaa J. Kwegyir (Mb) Tanzania Bara na Raya Suleiman Hamada mwakilishi Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Sababu kubwa za kutokukubaliana na uteuzi wa wajumbe hawa ni kuwa kwanza, hawa watashiriki kama wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (constituent assembly) kwa hiyo kuna ‘mgongano ulio dhahiri wa kimaslahi’. (kwa mujibu wa vifungu cha 6 na 22 (1) (a) na (b) vya sheria Namba 8 ya Mabadiliko ya Katiba, 2011)
Pili wananchi wanaowawakilisha watanyimwa haki yao ya kuwakilishwa kwa kipindi chote cha miezi 18 mpaka ishirini ambacho tume itafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Tatu, kuna majina mengi ambayo mheshimiwa Rais alipelekewa yenye sifa za kutosha angeweza kuwateua. Kulimbikiza kazi nyingi kwa watu wale wale si afya kwa demokrasia.
Uwakilishi finyu wa kijinsia na makundi mengine
Katika tume hii tumeona kuna uwakilishi finyu sana wa makundi kwa mfano wanawake wako 10 kati ya 32, yaani sawa na asilimia 27% tu! Tungetegemea asilimia 50% kwa 50% kwani Tanzania imesaini na kuridhia mkataba wa nyongeza wa maendeleo ya kijinsia kusini mwa Afrika yaani SADC Gender Protocol. Pia 3
Tanzania ina asilimia ya 51 ya idadi ya wanawake ambao miongoni mwao wengi wana utaalamu na sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume.
WITO
I) Tunapenda kutoa wito kwa serikali kuwa mchakato wa Katiba ni wa muhimu sana hautakiwi kuchukuliwa kwa wepesi. Mchakato huu unajenga mustakabali wa Taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Hivyo katika maamuzi yote yanayochukuliwa, kuwe na jicho la HAKI ZA BINADAMU na utawala wa sheria.
II) Pia tunapenda kutoa wito kwa WANANCHI wote wa Tanzania, mijini na vijijini, wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara, TUSHIRIKI kwenye mchakato huu. Tunawasihi kuwa Tume ya Katiba itakapokuja kwenye maeneo yetu tuhudhurie mikutano yote na kutoa maoni yetu juu ya Katiba Mpya.
Wananchi katika makundi au mtu mmojamoja anaweza kupeleka maoni ya maandishi kwenye tume mara anuani itakapojulishwa kwa wananchi.
III) Mwisho tunatoa wito kwa tume kuhakikisha watu wote wanatoa maoni yao bila ubaguzi. Makundi yote ya jamii yafikiwe (Wanawake, wanaume, watu wenye ulemavu na watoto wenye umri wa kutoa maoni).
Asanteni kwa kunisikiliza,
Dr. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi mtendaji- LHRC
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment