TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Tuesday, March 6, 2012

MAGUFULI ACHARUKA


Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli akipongezana na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (kushoto) baada ya kufungua rasmi kituo cha mabasi madogo ya abiria cha Mbezi Mwisho, Barabara ya Morogoro, Dar es Salaam kitakachohudumia mabasi zaidi ya 80. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki na Meya wa Ilala, Yusuf Mwenda (kushoto kwa Waziri). (Picha kwa hisani ya Habari Leo).


WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ameipa siku tano Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam kuondoa wafanyabiashara na mabango yote yaliyojengwa kwenye barabara za pembeni ikiwa ni hatua ya kukabiliana na msongamano.
Amesema hata ikiwa bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) au Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imesimikwa eneo la barabara, ing’olewe mara moja kwa kuwa katika suala la utekelezaji wa sheria, kila mtu anahusika.
Aidha, amesema Serikali ipo katika utekelezaji wa miradi ya barabara kwa fedha za ndani na za wahisani ambapo madaraja ya juu ya waenda kwa miguu kama la Manzese yatajengwa katika vituo vikuu vitano kati ya 29 jijini humo.

Magufuli alisema jana kuwa katika ujenzi wa barabara unaoendelea nchini, ni kosa la kisheria kwa barabara kuu kuwekwa matuta na kuwataka wenye magari wanaoona kuna umuhimu wa matuta wakayapitishe magari yao kwenye matuta ya viazi.

“Serikali imekuwa ikijenga barabara kwa kiwango cha lami kila siku, lengo ni kuharakisha maendeleo na kupunguza msongamano wa magari, lakini kuna watu wanadai matuta kwenye barabara kuu. “Sheria namba 13 ya mwaka 2007 inakataza hilo. Tanroads hakuna kuweka matuta kwenye barabara hizo, kama ni muhimu wakapitishe magari yao katika matuta ya viazi,” alisema Magufuli.

Hii ni mara ya pili kwa Magufuli kutoa kauli ya namna hiyo baada ya ile aliyowataka wakazi wa Kigamboni wanaogomea ongezeko la nauli kwa vivuko vyao kuacha kuvitumia vivuko na badala yake wapige mbizi.

Magufuli alikuwa akizungumza jana katika ufunguzi wa kituo kipya cha daladala cha Mbezi Mwisho, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, kilichojengwa na Kampuni ya Skol Building kwa gharama ya Sh bilioni 1.4 hadi sasa, huku choo hakijakamilika.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanroads, Patrick Mfugale, ujenzi wa choo na uzio ungekamilika katika kipindi cha mwezi mmoja, lakini jana Magufuli aliagiza choo kikamilike
wiki moja ijayo.

Pia alipiga marufuku biashara katika kituo hicho na kuagiza daladala zisitozwe ushuru wowote kuingia hapo.

Akizungumza katika hadhara hiyo, Magufuli alisema jitihada nyingi za ujenzi wa miundombinu zikiwamo barabara zinazofanywa na Serikali, zimerudishwa nyuma na baadhi ya watendaji na viongozi kwa kufumbia macho uvunjifu wa sheria wa kuwaacha wafanyabiashara holela na ujenzi wa ofisi na maegesho ya malori kando ya barabara.

“Sheria ni msumeno, tunavyosema kuwa Serikali ijenge barabara ni lazima sisi wenyewe kuzingatia sheria, viongozi wa manispaa zote hili tatizo lipo, lakini Dar es Salaam inaongoza kwa kuvunja sheria za Mfuko wa Barabara, barabara za pembeni Ubungo sasa ni maegesho ya malori,” alisema Magufuli na kuongeza: “Meneja wa Tanroads, (huku akimgeukia Mkurugenzi), nakupa siku tano, wale wote waliovamia maeneo hayo kwa kutumia kifungu namba 26 cha sheria kinachosema msimamizi wa barabara zote ni Tanroads, waondoke mara moja, hata kama ni bendera ya CCM au Chadema, ivunje kama iko eneo la barabara”.

Waziri aliitaka Tanroads isitangulize siasa katika suala la utendaji wa sheria kwa kueleza kuwa ikiwa hatua hiyo haitachukuliwa, hata malaika wakiletwa nchini, watakwama kwenye msongamano.

Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, kutumia mamlaka yake kwa kushirikiana na Polisi kuwachukulia hatua papo hapo ya kuwatoza faini ya Sh milioni moja watakaokamatwa wakikiuka agizo hilo.

Kuhusu vituo na barabara za juu, Magufuli alisema tayari Serikali imesaini zaidi ya Sh bilioni 240 kutoka Benki ya Dunia kwa ujenzi wa barabara hizo kwa mradi wa mabasi ya kasi.

Baadhi ya vituo vitakavyohusika alivitaja kuwa ni Kimara, Magomeni, Fire, Kariakoo na kivukoni na Magomeni-Moroccona wakandarasi wako tayari.

Alisema ujenzi huo utahusisha vivuko vya waenda kwa miguu kama daraja la Manzese ambapo mpaka sasa vituo 29 vimeainishwa vikiwamo vikuu vitano na Sh bilioni 48.9 zitatumika.

Akizungumzia mafanikio ya barabara tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961, Magufuli alisema kulikuwa na barabara za lami za umbali wa kilometa 1,300 na wakati wa maadhimisho ya miaka 50 zimefikia kilometa 6,500 na zilizo kwenye ujenzi wa kiwango cha lami sasa ni kilometa 11,154.

“Hizi zitakamilika kati ya miaka minne au mitano ijayo, hizi zikipelekwa Rwanda, nchi nzima itakuwa ya lami, hii inadhihirisha kuwa Serikali yenu inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, iko kazini,” alisema Magufuli.

Akizungumzia ombi la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mkuu wa Mkoa Sadiki walioyatoa kwa nyakati tofauti katika hafla hiyo ya kutaka baadhi ya barabara za pembezoni kupandishwa
hadhi, Magufuli alisema suala hilo atalifikisha katika kikao cha wizara hivi karibuni ili zitakazostahili kwa mujibu wa sheria zipandishwe.

Kuhusu kituo hicho, kabla ya ufunguzi, Magufuli aliagiza Tanroads iendelee kukisimamia kwa kuhakikisha kuwa hakuna biashara itakayofanyika na daladala zote zikitumie bila ushuru.

Mara baada ya ufunguzi huo daladala zilianza kazi; ya kwanza kuingia ni inayofanya safari za Ubungo-Mlandizi yenye namba T343 AUZ.

Watendaji wafukuzwe
Akizungumzia changamoto kubwa kwa barabara, Magufuli alisema ni matumizi yasiyo sahihi ya fedha za Mfuko wa Barabara na kumtaka Mwenyekiti wa Mfuko huo, Dk. James Wanyancha, kumpelekea orodha ya watendaji wa manispaa waliotumia fedha hizo vibaya ili aipeleke orodha hiyo kwa Rais wafukuzwe kazi.

“Kazi ya Mfuko wa Wanyancha, za barabara zilitengwa Sh bilioni 316 mwaka huu wa fedha, niwashukuru wabunge walifanya kazi nzuri katika marekebisho ya sheria sasa ongezeko la fedha za mafuta ya taa zinaingia humo, awamu zote nne zikiisha, tutapata ongezeko la Sh bilioni 90, hizi zitatumika katika Manispaa,” alisema na kuongeza: “Ila baadhi ya Manispaa hazitumii hizi fedha vizuri, zinapelekwa kwenye posho za vikao vya madiwani, Mwenyekiti wa Mfuko hakikisha fedha hizi hazitumiki vinginevyo, tusaidiane wabunge, madiwani hizi pesa zifanye yaliyokusudiwa, mniletee orodha ya wakurugenzi wote waliozitumia vibaya, nipeleke kwa Rais awafute kazi”.

Mkandarasi Msimamizi wa Ujenzi huo, Andrew Msacky, alisema mpaka mwisho wa mwezi huu, ujenzi wa uzio na choo utakuwa umekamilika, lakini kwa sasa vyoo vya dharura vitaendelea kutumika ili kuruhusu kiendelee kutumika.

Awali Sadiki alishukuru kwa ufunguzi wa kituo hicho kilichokuwa kikisubiri ujenzi wa choo ili kifunguliwe rasmi na kueleza kuwa kitasaidia kupunguza msongamano eneo la Mbezi Mwisho katika barabara kuu ya Morogoro.

“Moja ya sababu za kuchelewa ni mvutano uliokuwapo wa nani atajenga choo kati ya Manispaa na Tanroads, tunashukuru suluhu ilipatikana kuwa Tanroads ijenge, tunaomba kituo kisiwe cha biashara na daladala zisitozwe ushuru,” alisema Sadiki.

Mkuu huyo alitumia fursa hiyo kuwataka wakazi wa Dar es Salaam kuwa wazalendo kwa ulinzi wa mali za jamii hasa mifuniko ya majitaka barabarani na alama za barabara ambazo zimekuwa zikiibwa na kugeuzwa vyuma chakavu.

Katika hilo Magufuli alimtaka kuvamia maeneo ya kuyeyusha vyuma na kukamata wahusika.
Kituo hicho kilichoanza kujengwa mwaka 2009, kina uwezo wa kuingiza daladala 80, mabasi ya mikoani 10 na magari madogo yasiyozidi tani tano kwa wakati mmoja.

No comments: