KAULI ya Waziri Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, ya kukosoa mwenendo wa serikali na kuionya kuwa makini na nyongeza ya posho mpya za wabunge, imeichefua Ofisi ya Spika wa Bunge.
Ofisi ya Spika wa Bunge jana ilimshambulia vikali Sumaye juu ya shutuma hizo na kumwonya awe makini na mwangalifu juu ya kauli anazozitoa dhidi ya Serikali ya Rais Kikwete.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu kutoka mjini Dodoma, Naibu Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai, alisema tuhuma nyingi ambazo Sumaye alizielekeza kwa Bunge na serikali hazina msingi na amezitoa kama njia ya kuusaka urais.
“Mimi namheshimu sana Sumaye kutokana na nafasi yake, lakini namtaka awe makini na kauli zake. Mambo mengi aliyoyasema yana lengo la kujitafutia sifa kisiasa. Asitumie matatizo ya Serikali na Bunge kama mtaji wake kisiasa,” alisema Ndugai.
Ndugai alisema kauli ya Sumaye kupinga nyongeza ya posho mpya za vikao kwa wabunge ni ya kushangaza kwa kuwa ndiye mwasisi wa suala hilo.
“Sumaye amenishangaza sana, yeye alipokuwa waziri mkuu, ndiye aliyeasisi posho hizi (sitting allowance) anazopigia kelele leo. Lakini pia alikuwa akiziongeza kila mara kadiri ya mahitaji ya wabunge yalivyokuwa na mimi wakati huo nikiwa mbunge. Kwa hiyo ameshiriki kuzianzisha, ameshiriki kuziongeza, ameshiriki kuzipokea, leo anasema tusiongeze posho, aseme basi anataka ziwe kiasi gani?”
“Sumaye amechukua posho (sitting allowance), muda wake wote wa ubunge na kiasi cha wakati ule kilizingatia mazingira na hali ya uchumi. Mazingira ya sasa yamebadilika, aseme anataka wabunge wapokee kiasi gani,” alisema Ndugai.
Ndugai alidai Sumaye analipwa asilimia 80 ya mshahara wa waziri mkuu aliye madarakani, gharama za matibabu na nyingine nyingi kiasi ambacho ni kikubwa kuliko wastaafu wengi nchini lakini hajawahi kulalamika kutaka mshahara huo upunguzwe.
“Sumaye analipwa marupurupu makubwa kama waziri mkuu mstaafu kuliko wastaafu wa kada nyingine,” alisema Ndugai.
Kwa mujibu wa Ndugai, kauli ya Sumaye ni moja ya harakati zake za kutaka urais, hivyo alimtaka asitumie nafasi hiyo kuishambulia serikali iliyopo madarakani kama mtaji wake kisiasa.
“Tunajua kwamba kelele za Sumaye zinatokana na dhamira yake ya kutaka urais mwaka 2015 na kama ni hivyo basi, asubiri muda ufike au atangaze rasmi kuwania kiti hicho kuanzia sasa ili jamii ijue,” alisema Naibu Spika Ndugayi.
Kuhusu kulinganisha utendaji na mafanikio ya Serikali yao ya Awamu ya Tatu, chini ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa na ya sasa ya Rais Kikwete, Ndugai alisema Sumaye anakosea kuzilinganisha serikali hizo wakati wa sasa ambapo haijamaliza muda wake.
“Sipendi kuzungumzia hoja yake kuhusu serikali yao na hii ya Kikwete. Lakini atuambie, wao wamemaliza miaka kumi, Kikwete ana mwaka wa sita, bado ana safari ndefu, unalinganishaje utendaji wa serikali hizo mbili?” alihoji Ndugai.
Juzi wakati akihojiwa katika kipindi cha dakika 45, kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, Sumaye aliionya serikali kutoridhia posho mpya za wabunge kwani kilio cha nyongeza ya posho ni cha wengi, hali ambayo itasababisha uendeshaji wa serikali kuwa mgumu.
Sumaye alisema kwa kuwa tayari suala hilo limeonesha kukera umma wa Watanzania, si sahihi serikali kuendelea nalo.
“Mwanasiasa mzuri ni yule anayefanya jambo ambalo halikeri umma, lakini jambo hilo tayari limeonesha kuukera umma, hivyo si vizuri kuendelea nalo. Lakini jambo hili bado lina utata, tumeshuhudia Katibu wa Bunge na Spika wanatofautiana huku Ikulu ikiwa imekaa kimya, mambo haya yanachanganya umma, watu wanapaswa kujua kumetokea nini,” alisema Sumaye.
Hata hivyo, alisema suala la posho ni tatizo kubwa serikalini, kwani hivi sasa ofisi nyingi zimehamia hotelini kufanya mikutano ya aina mbalimbali kwa lengo la kupata posho.
Sumaye alisema alipokuwa waziri mkuu katika kipindi chake cha kwanza mwaka 1999 na 2000 alipambana na wabunge kuhusu suala hilo na aliwakatalia na Rais Mkapa alipotaka kumteua kwa mara ya pili kuendelea na wadhifa huo, alikataa, kwani alihofu wabunge wasingelipitisha jina lake kwa hasira.
Sumaye ambaye ni waziri mkuu pekee aliyeteuliwa kushika wadhifa huo katika vipindi viwili mfululizo, aliiomba serikali kuachana na jambo hilo kwani limeonekana kupingwa na umma.
Mbali ya posho mpya za wabunge, Sumaye pia alizungumzia madaraka ya urais ambapo alisema viongozi wengi Afrika wanapokuwa marais wanayachukulia madaraka hayo kama mali yao binafsi na familia zao, hivyo hutajirika baada ya muda mfupi.
Alipoulizwa endapo anakusudia kuwania urais mwaka 2015, Sumaye ambaye amepata kuwania kiti hicho mwaka 2005, alisema bado hajaamua kugombea nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment