Mgombea Ubunge Jimbo la Igunga kwa tiketi ya CCM, Dk Dalaly Kafumu (katikati) akiwa ameshikana mikono na wagombea wenzake Joseph Kashindye wa Chadema (kushoto) na Leopold Mahona wa CUF baada ya kumalizika kwa mdahalo wa pamoja uliofanyika kwenye ukumbi wa Sakao mjini Igunga juzi usiku
WAGOMBEA ubunge katika Jimbo la Igunga, Leopold Mahona wa CUF na Mwalimu Joseph Kashindye wa Chadema, jana walimkaba koo mgombea wa CCM, Dk Dalaly Kafumu katika mdahalo uliofanyika jana mjini hapa kuwa amehusika na mikataba mibovu ya madini.Walitoa maneno hayo kwenye mdahalo wa uchaguzi mdogo wa Igunga na Tanzania tunayoitaka ambao uliwahusisha wagombea hao watatu uliofanyika katika ukumbi wa Sakawa.
Mahona alimtuhumu Dk Kafumu kuwa ndiye aliyesaini mikataba mibovu ya madini inayoligharimu taifa hadi sasa akidai kwamba katika kila Sh100 ya Tanzania, nchi inapata Sh3.“Hakuna wilaya ambayo mtu anaweza kutembea na kuokota almasi, isipokuwa Igunga. Lakini sekta hiyo iko chini na chanzo ni huyu bwana, nani asiyejua kuwa ndiye aliyesaini mikataba mibovu ya madini?” alihoji Mahona.
“Mikataba ambayo katika kila Sh100, Serikali ya Tanzania na watu wake inaambulia Sh3!”alisema Mahona huku akishangiliwa na watu waliohudhuria madahalo huo.Akijibu hoja hiyo, Dk Kafumu alisema hakuwahi kuingia mikataba ya madini, bali alikuwa msimamizi wa sheria iliyotungwa bungeni.
“Mimi kazi yangu ni kusimamia sheria na si kusaini mikataba. Kazi ya kusaini mikataba inafanywa na waziri na sheria inatungwa bungeni kina Zitto (Kabwe, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Chadema) wanafahamu,” alisema Dk Kafumu.
Hata hivyo, baada ya majibu hayo mgombea wa Chadema Kashindye, alisimama na kitabu kinachoelezea utafiti wa madini nchini alichoeleza kuwa hakijulikani kwa wananchi wa kawaida na badala yake, kimeuzwa Ulaya kutafuta wawekezaji.
“Katika kitabu cha mgombea wa CCM kinaeleza kuwa Igunga kuna madini ya aina 11, kitabu hiki amekiuza na kukitangaza Ulaya kuvutia wawekezaji, woga wangu ni kuwa ule mpango wa kufukia wananchi katika Mgodi wa Bulyanhulu, unaweza kufanyika hapa Igunga,” alisema Kashindye.
Maswali kwa mgombea wa Chadema
Moja ya matukio yaliyopamba mjadala huo ni maswali ya papo kwa papo yaliyoelekezwa kwa wagombea na mengi yaliyoonekana kuwa magumu yalielekezwa kwa Kashindye.
Miongoni mwa maswali yaliyompa mgombea huyo wakati mgumu kujibu ni kueleza endapo chama hicho si chama cha fujo kutokana na matukio kadhaa yaliyotokea wakati wa kampeni ikiwamo kupigwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.
Akijibu swali hilo Kashindye alisema kwa kuwa kesi iko mahakamani ushahidi wa wazi kuhusu tuhuma hizo utafafanuliwa mahakamani na watu wote watajua ukweli.
Swali jingine lilihusu yeye kuwa mtumishi wa halmashauri na moja ya matatizo katika wilaya hiyo ni ubadhirifu wa mali za umma na elimu duni.
Alisema: “Mimi sikuwa mtumishi wa halmashauri ya wilaya kama ambavyo inapotoshwa hapa. Mimi ni Mkaguzi wa Elimu na bosi wangu ni Wizara ya Elimu na wala si halmashauri ya wilaya,” alisema.
Alitaja kazi ya mkaguzi wa elimu kuwa ni kuangalia matatizo katika shule mbalimbali na kutoa ushauri wa kitaalamu unaopaswa kutekelezwa na watendaji wa halmashauri iliyoko chini ya DC, mkurugenzi na ofisa elimu.
“Nilifanya kazi yangu na kukabidhi ushauri wangu lakini watendaji serikalini hawakuufanyia kazi, mkaguzi ni kama mtu wa maabara anayepima na kueleza ugonjwa lakini wa kuandika dawa ni daktari,” alisema.
Kuhusu alama ya vidole viwili kama alama ya fujo alisema alama hiyo huashiria ukombozi na imekuwa ikitumiwa na wananchi wanaotafuta ukombozi wanapokuwa wamechoshwa na Serikali zao.
“Nchi kama Libya, Tunisia, Misri wale siyo waasi, bali ni wananchi wanaopigania ukombozi wa nchi zao baada ya kuchoshwa na Serikali dhalimu na sisi Chadema, tunasema tutawakomboa wananchi wa Tanzania tukianzia na Igunga kwa njia ya kura,” alisema.
CUF yaahidi mabadiliko ndani ya siku 100
Kwa upande wake, Mahona aliahidi mabadiliko ndani ya siku 100 endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Alisema endapo atachaguliwa, atahakikisha ndani ya siku 600 anajenga Daraja la Mbutu na kuwafikishia neema wakazi wa Jimbo hilo.Alisema ataanzisha Saccos katika kila tarafa, atachimba visima vya maji katika kila kijiji na atahakikisha rasilimali ya madini inawanufaisha wakazi wa Igunga
CCM yajivunia Ilani ya Uchaguzi ya 2010
Dk Kafumu alisema endapo atachaguliwa atahakikisha anatekeleza ahadi zote zilizomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.Alisema katika ilani hiyo kuna ujenzi wa Daraja la Mbutu ambalo limekuwa likiisumbua Igunga, kukamilisha ujenzi wa zahanati na shule za kata.
Kuhusu maji, alisema atachimba bwawa kubwa litakalolingana na lile la Kata ya Mwanzugi katika kila kata ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wote wa Igunga. Aidha, alisema atahakikisha anatekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria.
Mtatiro aisukumia CCM zigo la vurugu
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro amekituhumu CCM kuwa ndicho chama kinachoanzisha vurugu katika uchaguzi mdogo wa Igunga licha ya viongozi wake kuhubiri amani.
Mtatiro alitoa kauli hiyo wakati viongozi wa vyama vya siasa walipokaribishwa jukwaani baada ya kumalizika kwa mdahalo wa wagombea.
Alikishambulia CCM na kujibu hoja za Mratibu wa Kampeni wa chama hicho, Mwigulu Nchemba.“Mwigulu ameongea amani ya kudumu huku akiwa ameandaa makambi ya vijana katika Wilaya ya Nzega, Uyui na Iramba mkoani Singida, vijana hao wanajiandaa kufanya nini?” alihoji Mtatiro.
Aliwataka wakazi wa Igunga kumchagua Mahona akidai kuwa ndiye kijana pekee aliyeonyesha kuwa anaweza kuwatumikia wakazi wake na kwamba ana mtaji wa kura zaidi ya 11,000.
Nchemba azomewa jukwaani
Kauli ya Mtatiro ilimfanya Nchemba kusimama na kuchukua kipaza sauti kwa lengo la kutaka kujibu hoja hizo lakini kundi la watu waliohudhuria mkutano lilipinga kitendo hicho.
Washiriki wa mdahalo huo hasa waliodaiwa kutoka vyama vya CUF na Chadema walisimama na kupinga mratibu huyo kupewa kipaza sauti kwa kile walichoeleza kuwa Mtatiro alikuwa mzungumzaji wa mwisho.
Huku Nchemba akiwa ameshika kipaza sauti mkononi, hali ilibadilika ukumbini hapo, kundi hilo lilipiga kelele na kuanza kusogea eneo lilikokuwa jukwaa kuu kupinga kitendo hicho.
“Hapana, hapana hii haikubaliki hatutaki azungumze huyo,” zilisika kauli kutoka kwa washiriki wa mdahalo huo.
Hali hiyo iliwafanya wanachama na wafuasi wa CCM waliomsindikiza mgombea huyo ukumbini kutoka wakiwa hawana furaha ya kutosha kama ilivyokuwa wa wafuasi wa vyama vya CUF na Chadema.
Zitto aahidi utumishi uliotukuka
Kwa upande wake, Zitto aliwaasa wakazi wa Igunga kuchagua mbunge atakayeweza kuwasemea kero zao ili zifanyiwe kazi.“Nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa wagombea wote, wameonyesha namna walivyojiandaa kuwatumikia wananchi,” alisema Zito na kuongeza:
“Kumbukeni kuwa uchaguzi huu si wa kuamua nani anajua kutukana, nani kavuliwa hijabu ni uchaguzi uliolenga kumpata Mbunge wa Igunga atakayeshughulika na matatizo ya watu.”
“Uchaguzi huu unaohusu kero za maji, ajira kwa vijana na hatima ya maendeleo ya watu wa Igunga na Chadema tumeshaonyesha mfano bungeni tupatieni mbunge wa 49 ili kutuongezea nguvu,” alisema.
Aliwahimiza wakazi wa Igunga kwenda kupiga kura kumchagua mbunge atakayeweza kuwasemea bungeni na si bora kiongozi.Alisema watu wanakumbuka katika Bunge la Tisa ambalo wabunge wa Chadema walikuwa 11, lakini kazi zao zilionekana na sasa wamefikia 48.
“Chadema hatuahidi maziwa na asali kwa wakazi wa Igunga, kazi zetu Watanzania mmeziona na mkatuongeza hadi kufikia 48 na sasa tunataka Igunga mtuongezee mtu wa 49 ili kutuongezea nguvu ya kufanya kazi.”
Kabla ya mdahalo
Mdahalo huo ulitanguliwa na vurugu za hapa na pale. Watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM na CUF walishambuliana kwa maneno.Hali hiyo ilimlazimu Polisi aliyekuwapo ukumbini kusimama na kutoa maelezo juu ya malengo ya mdahalo huo kwamba ni kuwapima wagombea wao na kutishia kwamba endapo hali ingeendelea kuwa hivyo kungeahirishwa.
“Mdahalo unawapa nafasi ninyi wakazi wa Igunga kupima wagombea, lakini kama hali itaendelea hivi tuna uwezo kusitisha,” alisema.
No comments:
Post a Comment