Katibu mkuu wa CCM, Wilson Mukama (mwenye miwani) akitoka kuangalia nyumba ya Katibu wa chama hicho kata ya Nyandekwa Jimbo la Igunga, Hamis Makala iliyochomwa moto usiku wa kuamkia juzi na watu wasiojulikana
MATUKIO ya hujuma yanazidi kulitikisa Jimbo la Igunga safari hii watu wasiojulikana wamechoma moto nyumba ya Katibu wa CCM, Kata ya Nyandekwa usiku wa kuamkia juzi.Tukio hilo linahusishwa na wafuasi wa Chadema kutokana na ujumbe wa maandishi uliokutwa umechomekwa katika nyumba hiyo ukisomeka: “Chadema sisi ni wajanja”.Katibu huyo, Hamis Makala alimweleza Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama aliyemtembelea jana kumpa pole kuwa, kwa muda mrefu amekuwa akiwindwa na wafuasi hao wa Chadema.
Alidai kuwa sababu ya kuwindwa na wafuasi hao inatokana na kukasirishwa na kampeni anazozifanya katika kata hiyo zinazoifanya CCM ikubalike kwa wananchi na kukiacha Chadema kikikosa watu kinapokwenda kufanya mikutano ya hadhara. Nyumba iliyoteketezwa kwa moto ilikuwa ikitumiwa na katibu huyo kwa shughuli za jiko na kuhifadhia kuku.
“Niliposhtuka na kutoka nje nilikuta moto mkubwa unawaka nikapiga yowe kuomba msaada. Lakini majirani walishindwa kuuzima kwa kuwa ulikuwa umesambaa… kuku 15 kati ya 21 waliokuwamo ndani wamekufa,” alisema.
Alisema baada ya kushindwa kuuzima moto huo na nyumba hiyo kuteketea, aliamua kulala na asubuhi majirani walipofika tena kumjulia hali ndipo walipogundua karatasi ikiwa na ujumbe wa Chadema kuhusika.
Alidai kuwa mbali na ujumbe huo, upo mwingine wa maandishi ambao ulipenyezwa katika Ofisi ya CCM ya kata hiyo unaosisitiza kuwa Chadema hawahitaji bendera za CCM katika kata hiyo. Alisema kuwa karatasi zote hizo mbili zimechukuliwa na polisi.
Mukama alaani
Akizungumzia tukio hilo, Mukama amesema alisema ni lazima lilaaniwe na kila Mtanzania mpenda amani wakiwamo wananchi wa Igunga na akavitaka vyombo vya dola kuhakikisha vinawasaka na kuwakamata waliohusika.
“Ni lazima lilaaniwe kwa sababu halitoi taswira na maana halisi ya kuwa na vyama vingi ambavyo vinapaswa kushindana kwa ubora na sera… hatushindani kwa vitisho, uhuni na hata kumwagiana tindikali,” alisema.
Alisema ameshangazwa na mwenendo wa Chadema kuendesha siasa za chuki hususan katika Jimbo la Igunga na kutoa mfano wa Kenya ambako vyama vingi ni vya kikabila lakini hakuna matukio ya aina hiyo.
Alitumia fursa hiyo kupiga kampeni akisema matukio yanayotokea Igunga hivi sasa yanawasaidia Watanzania kukielewa Chadema ni chama cha aina gani na kuwataka Wana-Igunga kukiadhibu hicho kwa kukinyima kura Oktoba 2 ,mwaka huu.
“Demokrasia haiwezi kuanishwa kwa matukio ya kihuni na wale wanaotaka kuipa demokrasia taswira ya hovyo ni lazima waadhibiwe. Njia pekee ya kuwaadhibu watu wa aina hiyo ni kuwanyima kura,” alisema.
Katibu Mkuu huyo alimpa kiongozi huyo msaada wa Sh100,000 ili azitumie kuirejesha nyumba hiyo katika hali iliyokuwapo kabla ya tukio.
CUF waungana na CCM
Mwenyekiti wa CUF Kata ya Nyandekwa, Emmanuel Ezekiel ambaye alifika eneo la tukio mata tu baada ya Mkama na msafara wake kufika, alisema tukio hilo ni la kihuni na linapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote.
“Unajua kwenye mji unaweza kuwa na watoto watatu wa baba mmoja, mama mmoja lakini akatokea mmoja akawa kichaa msipomdhibiti atawaharibia ule mji,” alisema Ezekiel bila kufafanua kauli yake hiyo.
Mwenyekiti huyo alitahadharisha kuwa kampeni katika Jimbo hilo la Igunga ni za mwezi mmoja tu lakini, kama zisipofanyika kwa ustaarabu zinaweza kuzaa uhasama utakaodumu kwa miaka mingi.
Polisi wanena
Mkuu wa kitengo cha ufuatiliaji na tathmini kutoka makao makuu ya Polisi, Naibu Kamishna, Isaya Mngullu alisema polisi wanaendelea na upelelezi.
“Ni kweli hilo tukio lipo linadaiwa kutokea usiku wa kuamkia jana (juzi) na sisi tumeanzisha upelelezi, nipeni muda tukusanye taarifa halafu nitawaita (waandishi) niwapeni taarifa kamili,” alisema Mngullu.
Chadema waruka
Lakini Kamanda wa Operesheni za Kampeni wa Chadema, Benson Kijaila jana alikanusha chama chake kuhusika na tukio hilo na kukigeuzia kibao CCM kuwa wao ndicho kilichoshiriki katika tukio hilo.
“Matukio haya wanayapanga wao wenyewe halafu wanasingizia vijana wetu… kama ni kuchoma hiyo nyumba wameichoma wenyewe ni mpango wao huo,” alisema.
Kamanda huyo alisema hata tuhuma za tindikali zinazoelekezwa kwa Chadema ni mipango iliyosukwa na CCM na kwamba kama ni watu wenye tindikali, basi CCM ndiyo walionazo.
Tukio hilo la juzi la kuchomwa moto nyumba ya kada huyo wa CCM ni mwendelezo wa matukio ya kihalifu yanayotokea Igunga na wakati wote, matukio hayo yamehusishwa na wafuasi wa Chadema.
Mwanzoni mwa wiki hii, wabunge wawili na kada mmoja wa chama hicho walishtakiwa mahakamani kwa makosa manne likiwamo la kumdhalilisha na kumwibia Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario.
Septemba 9 mwaka huu, kijana mmoja anayedaiwa ni mwanachama wa CCM, Mussa Tesha (25) alimwagiwa tindikali usoni na watu anaodai kuwatambua kuwa ni wanachama wa Chadema.
No comments:
Post a Comment