Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Yuda Thedeus Ruwai’chi
MAKANISA nchini yamesema hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyotoa juzi katika Baraza la Idd ni nzito na kwamba, kama angekuwa anatoa hotuba kama hizo, matatizo mengi ya nchi yangekuwa yamepata ufumbuzi.Katika baraza hilo pamoja na mambo mengine, Rais Kikwete akijibu risala ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania, (Bakwata) alizungumzia mambo muhimu kuhusu taifa ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kadhi, viongozi wa dini na biashara ya dawa za kulevya na udini katika siasa.
Jana, kwa nyakati tofauti wakizungumzia hotuba hiyo baadhi ya maaskofu akiwemo Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Yuda Thedeus Ruwai’chi, alimpongeza mkuu huyo wa nchi kwa hotuba hiyo nzito.
Ruwai'chi
Ruwai'chi ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Mwanza alisema: “Kauli kama za jana (juzi) zingekuwa zinatolewa mara kwa mara, masuala mengi ya nchi yangeshapata ufumbuzi, nimesoma hotuba hiyo kwenye magazeti, lakini nitafurahi sana nitakapopata hotuba yenyewe niisome kwa mtiririko wake”.
Mahakama ya Kadhi
Kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi, Askofu Ruwai’chi aliunga mkono kauli ya Rais Kikwete kuhusu waumini hao kuanzisha mahakama hiyo wenyewe na kusisitiza kuwa Waislamu ni watu wazima wasiotaka kubebwa na mtu yeyote ili kufanikisha mambo yao.
Askofu Ruwai'ch alifafanua: “Wakianzisha wenyewe Mahakama ya Kadhi hakuna anayewazuia..., kwa sababu ni dini isiyohitaji kubebwa, waanzishe chombo chao kisicho cha Serikali, wakiendeshe kwa fedha zao wenyewe”.
Hata hivyo, alisema, bado Serikali inaonekana kuwa na kigugumizi juu ya suala la mahakama hiyo, ndiyo maana kuna kauli zinazogongana.
Rais huyo wa Tec badala yake alisema, “Mara anasema suala lipo kwa Waziri Mkuu, mara waanzishe wenyewe..., wasijing’ate, wawaambie tu kuwa waanzishe mahakama yao kwa fedha zao na waiendeshe wenyewe”.
Utaifishaji wa shule
Akizungumzia madai ya kurejeshwa kwa shule zilizokuwa zikimilikiwa na taasisi za dini na baadaye kutaifishwa wakati wa Serikali ya awamu ya kwanza chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, Ruwai’chi alisema ingekuwa ni kulalamika, kanisa lingekuwa la kwanza kwa sababu mamia ya shule zake zilitaifishwa.
“Lakini kanisa tumetulia na tumejenga shule zetu nyingine ambazo zinatoa huduma kwa Watanzania bila ubaguzi wowote..., tujipange tuanzishe shule na tuziendeshe,” alisema Askofu Ruwai’chi.
Dawa za kulevya
Ruwai’chi alisema Serikali ichukue hatua za kuwakamata watu wanaojihusisha na biashara hiyo bila kujali kama ni viongozi wa dini wala siasa.
“Serikali itumie vyombo vyake kuhakikisha wote wanaojishughulisha na biashara hii wanakamatwa, siyo kuibua hoja ambayo itajificha nyuma yake na kuacha kushughulikia mambo muhimu yanayowakabili wananchi,” alisema Ruwai’chi.
Kuhusu udini katika siasa, Ruwai’chi alisema kwamba, suala hilo lilienezwa na baadhi ya wanasiasa katika uchaguzi uliopita na sasa limedakwa na baadhi ya viongozi wa dini na baadhi ya vituo vya redio.
Ruwai'ch alionya akisema: “Huku ni kucheza na moto, ni vyema Serikali ikahakikisha kuwa yeyote anayejaribu kuleta udini wa namna yoyote, anashughulikiwa mara moja, hili siyo suala la kucheza nalo hata kidogo”.
CCT nayo yakunwa
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Peter Kitula, alisema hotuba ya Rais Kikwete ni nzuri na imeweza kutoa ufafanuzi wa mambo mengi yaliyokuwa yakiikabili nchi.
Askofu Kitula ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la African Inland (AICT),Dayosisi ya Mara na Ukerewe alifafanua: “Hotuba ni nzuri, haikuegemea popote..., imetoa ufafanuzi kwa mambo mengi ya nchi na msimamo wa Serikali tumeuona”.
Kuhusu suala la Mahakama ya Kadhi, naye alisisitiza kwamba, inatakiwa ianzishwe na Waislamu wenyewe na uendeshwaji wake pia ufanywe na dini husika na isiwe na kufanya ujanja wa kuianzisha na baadaye Serikali ikajiingiza katika kuiendesha.
Akizungumzia kurejeshwa shule zilizotaifishwa, alisema jambo la kufanya ni Serikali kusaidia katika uendeshaji wa shule zote binafsi na siyo kuzirudisha ambazo zilitaifishwa.Kuhusu dawa za kulevya, alisema ni vyema Serikali ikachukua hatua kwa mujibu wa sheria ama kutaja majina ya wahusika hadharani badala ya kutoa maelezo ya jumla.
Mbatia
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amekitaka CCM kuwaomba radhi Watanzania kutokana na kile alichokiita kufanya ulaghai wa kisiasa kwa kuweka ahadi hewa katika uchaguzi wa mwaka 2005/2010.
Mbatia alifafanua kwamba, hatua ya CCM kuwageuka Waislamu kuhusu kuanzishwa Mahakama ya Kadhi ni fundisho kwa Watanzania kupima ahadi za vyama katika uchaguzi kama zinatekelezeka.
Alisema CCM katika baadhi ya ahadi zake za uchaguzi ilifanya ulaghai kwa Watanzania kwani hazitekelezeki.
Kwa mujibu wa Mbatia, umefika wakati sasa mambo ya kitaalamu yakaachwa kuingizwa siasa akitoa mfano wa mahakama hiyo ya Waislamu kwamba ni jambo la wataalamu wa sheria na si wanasiasa.
Mhadhiri UDOM aonya udini
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Wallace Mlaga, alisema kuwa suala la kueneza chuki za kidini ni vyema likashughulikiwa haraka iwezekanavyo.
“Huko mitaani kuna kanda, CD, VCD ambazo zinaeneza chuki za kidini zinasambazwa..., ni vyema Serikali ikachukua hatua haraka, hii ni hatari sana,” alisema Mlaga.
Lakini, kuhusu hotuba kwa ujumla wake, alisema Rais Kikwete aligusia mambo muhimu ya nchi.
“Hata kuthubutu kuyasema tu ni ujasiri mkubwa..., sasa kinachotakiwa ni utekelezaji,” alisema Mlaga.
Hotuba ya JK
Akihutubia Baraza la Idd ambalo ni sehemu ya maadhimisho ya SikuKuu ya Idd El Fitri mjini Dodoma juzi, pamoja na mambo mengine Rais Kikwete alisema Wakristo nchini hawahusiki na kuchelewa kwa mchakato wa kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi.
“Nilipokutana na Jukwaa la Maaskofu Julai 22, mwaka huu walisema ngoja ninukuu…… Kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini ni jambo zuri linalowahusu Waislamu. Kwa kuwa ni jambo la kidini waachiwe Waislamu wenyewe walifanye ndani ya Uislamu, pasipo kutumia hazina ya Serikali ambayo ni fedha ya walipa kodi wote nchini…," alifafanua Rais katika tukio hilo lililofanyika katika Msikiti wa Gaddafi mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment