TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Wednesday, September 7, 2011

Dk. Slaa aandaa makombora mazito kumlipua Mkapa, JK


WAKATI pazia la kampeni za uchaguzi katika jimbo la Igunga, mkoani Tabora linafunguliwa leo, homa ya uchaguzi huo imepamba moto kwa wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF), kutunishiana misuli kwa kutaka kutwangana makonde.

Maneno makali na lugha chafu, zilisikika kutoka kwa wafuasi wa vyama hivyo wakati wakiwasindikiza wagombea wao walipokuwa wakirejesha fomu za kuomba kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kugombea kiti hicho.

Jeshi la Polisi wilayani hapa, lililazimika kufanya mazungumzo na wagombea wa vyama vyote pamoja na viongozi wao kusisitiza umuhimu wa kufanya kampeni za amani na utulivu.

Wagombea katika uchaguzi huo unaovuta hisia za Watanzania wengi na vyama vyao kwenye mabano ni Dk. Peter Kafumu (CCM), Joseph Kashindye (CHADEMA), Leopold Mahona (CUF), Hassan Ramadhan, (Chausta), Hemed Ramadhan (UPDP), John Maguma (SAU), Stevin Makingi (AFP) na Saidi Makeni (DP).

Katika hekaheka za kurejesha fomu hizo kabla ya muda uliowekwa kisheria wa saa 10 jioni kumalizika, misafara ya wafuasi wa vyama hivyo iliingiliana na kusababisha tafrani kubwa.

Hata hivyo wakati wafuasi wa CCM wakikwaruzana na wenzao wa CHADEMA na CUF, mgombea wao, Dk. Peter Kafumu, alirejesha fomu yake mapema kimyakimya.

CHADEMA inayopewa nafasi kubwa kushinda kiti hicho kilichoachwa wazi na Rostam Aziz (CCM), ilikuwa ikiongoza maandamano kuanzia ofisi zake za wilaya kuelekea katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi, lakini ghafla msafara wa maandamano yake uliopambwa na bendera, pikipiki, baskeli na magari, uliingiliwa na kukatizwa na wafuasi wa CUF, hali iliyosababisha wafuasi wa vyama hivyo kuanza kutunishiana misuli na kutaka kupigana.

Mgombea wa CHADEMA, Kashindye, aliwasilisha fomu yake kwa msimamizi wa uchaguzi saa saba mchana, wakati huo mgombea wa CUF, Leopold Mahona, naye akisubiri nje na wafuasi wake ili kuingia kukabidhi fomu yake.

Baada ya kukabidhi fumo yake, Kashindye alisema yuko tayari katika mapambano ya kusaka kura na kuwapa matumaini wananchi wa Igunga kwamba endapo watampa ridhaa, atafanya mambo makubwa kwa kutoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu, miundombinu, kilimo na mambo mengine ya miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake Mahona, alisema chama chake kinajiaandaa kusaka kura kwa wananchi na kuwaelimisha jinsi gani kimeandaa kuboresha maisha ya wananchi wa Igunga.

Lakini wakati huohuo, viongozi wa vyama hivyo kwa nyakati tofauti walikuwa wakiendelea kurushiana maneno ambapo kila mmoja alimshtumu mwenzake kuhusika katika kuwachochea wafuasi wake wafanye vurugu.

Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa CHADEMA, Waitara Mwikabwe, alisema CUF iliingilia msafara wao, jambo alilodai kwamba lingeweza kusababisha kutoweka kwa amani katika shughuli hizo.

Aliwaasa wafuasi wa CHADEMA kuwa wastaarabu katika mchakato huo, akisema wao wamekuja Igunga kuchukua kiti hicho.

Kwa upande wake, Katibu wa Vijana wa CUF, Mohamed Babu, aliishutumu CHADEMA kuwa ilivamia maandamano yao.

“Sisi tumetumia hekima kubwa sana kwa kuwastahi hawa mabwana, tungeamua tungezichapa kwanza ndipo tupeane heshima lakini kwa kuzingatia busara tumeacha.”

CCM kwa upande wake, ilitumia staili ya aina yake ambapo mgombea wake alifika katika ofisi za msimamizi saa tano asubuhi akiwa amesindikizwa na viongozi wa chama wilaya, mkoa na taifa, ikiwa kimya.

Sababu ya kufanya hivyo, ilitajwa kuwa ni kutokana na kuomboleza msiba wa mtoto Peter Zakaria, aliyepoteza maisha kwa ajali ya gari aina ya fuso wakati wa maandamano ya kumsindikiza Dk. Kafumu kuchukua fomu.

Dk. Kafumu alijinasibu kuwa kipaumbele chake kitakuwa upatikaji wa maji kwa kuchimba mabwawa, kuboresha miundombinu hasa daraja la Mbutu, kuboresha elimu ya sekondari na kilimo cha pamba.

Mratibu wa kampeni wa CCM, Mwigulu Nchema, alisema chama hicho kinategemea ushindi mkubwa wa kishindo, huku akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye uzinduzi wa kampeni za kumnadi mgombea wao Septemba 10.

Kampeni za uchaguzi huo zinatarajiwa kuanza rasmi leo huku muda wa kuwawekea pingamizi wagombea ukimalizika leo saa 10 jioni. Msimamizi wa Uchaguzi, Protace Magayane, alisema wagombea nane walioteuliwa kuwania kiti hicho.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, atazindua kampeni za mgombea wao kesho, wakati kesho kutwa Rais mstaafu Benjamini Mkapa, akitarajiwa kuzindua kampeni za CCM na CUF itazindua kampeni zake Septemba 13.

Akizungumza na gazeti hili, Dk. Slaa alisema wameandaa makombora zaidi ya 100 kuisambaratisha CCM na serikali yake ambayo alirejea wito wake wa mara kwa mara kuwa imeshindwa kuongoza na kusababisha maisha kuwa magumu kwa Watanzania.

Alisema amefurahi kwamba kampeni za CCM zinafunguliwa na Mkapa kwani CHADEMA imemwandalia makombora yake ya ufisadi alioufanya wakati akiwa Rais kabla ya Rais Jakaya Kikwete kurithi kiti chake.

No comments: