Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo
WAKATI Bunge limeunda Kamati Teule ya kuchunguza sakata la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, upepo unaonekana kumgeukia Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, baada ya wasomi na wanasiasa kumbebesha mzigo wa tatizo hilo.
Mwenyekiti wa Jukwa la Katiba, Deus Kibamba, amesema kitendo cha kutofautiana kwa viongozi katika kauli zao kuhusu kosa alilofanya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Jairo kinaonyesha Serikaliimegawanyika.Alisema alichofanya Luhanjo kinaifanya Serikali ipoteze uwajibikaji wa pamoja ambao kimsingi katika suala zima la mgawanyo wa madaraka kila mtu amekuwa akitumia vibaya nafasi aliyonayo.
“Waziri Mkuu alituambia kuwa angekuwa ndiye mwenye mamlaka ya mwisho angemfukuza kazi na alisisitiza kuwa anasubiri Rais arudi, lakini ghafla anajitokeza Katibu Mkuu Kiongozi, Luhanjo n kutangaza hatua za kumchukulia mtumishi wa Serikali ziko hivi. Huko ni kumdhalilisha Waziri Mkuu,” alisema Kibamba.Alisema hatua zote alizochukua Luhanjo zilionekana kumdhalilisha Waziri Mkuu na pia kitendo cha kutofautiana kwao kinaonyesha dhahiri Serikali haina mshikamano.
“Hii ni hatari kwa taifa, Serikali inaundwa na CCM chama ambacho tayari kimegawanyika na sasa inaonekana nayo imegawanyika,” alisema Kibamba.
Shellukindo
Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, William Shelukindo, amesema Phillimone Luhanjo ameshindwa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete.
Shelukindo ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Rais Ikulu (cheo ambacho sasa kinaitwa Katibu Mkuu Kiongozi) katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais Ali Hassan Mwinyi, alisema Luhanjo ameonyesha utovu wa nidhamu na ameidhalilisha Ikulu kutangaza kumrejesha Jairo bila kupitia bungeni.
"Kwa kitendo cha kutangaza kupitia vyombo vya habari kumrejesha kazini Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini David Jairo badala ya kufikisha bungeni suala lake, amemdhalilisha Rais na Ikulu," alisema.
Akizungumza na Blog hii katika Mahojiano maalum, Shelukindo ambaye pia ni Mbunge wa zamani wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, alisema kuliruka Bunge ni kuchonganisha mihimili miwili yaani Serikali na Bunge.
"Sipendi kuzungumza hivi sasa kwa sababu nimeamua kukaa kimya, lakini kwa kuwa naheshimiana na vyombo vya habari na mmetaka nizungumzie suala hili, nasema Luhanjo amemdhalilisha Rais Jakaya Kikwete na alitaka kumchonganisha na mhimili muhimu wa Bunge," alisema Shellukindo.
Alisema Luhanjo amefanya makosa na kumfanya aonekane kwamba hajasoma katiba ya nchi, kwani inaeleza wazi kwamba bunge lina jukumu la kusimamia shughuli za Serikali kwani ni muhimili.
Katiba ya nchi
Shellukindo alisema ibara ya 63 kifungu kidogo cha kwanza ya katiba inasema bunge ni pamoja na Rais kwa sababu wote tumekwenda kwenye uchaguzi kuomba ridhaa ya wananchi ya kuongoza Serikali na ndiyo maana hata mawaziri wanatokana na wabunge.
Mwanasiasa huyo alisema ibara hiyohiyo ya 63 kifungu cha pili kinaeleza kuwa Bunge lina jukumu la kusimamia mihimili hii ya Serikali, hivyo kwa kuwa suala la Jairo kwa lilianza bungeni ripoti yake ilistahili kupelekwa bungeni na isomwe huko na siyo vinginevyo.
Shellukindo alisema kitendo alichofanya Luhanjo kutoa taarifa ya kumrejesha Jairo kupitia vyombo vya habari pia kimemdhalilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Alisema kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi serikalini, baada ya kupelekewa majibu ya uchunguzi juu ya Jairo, Luhanjo alistahili kuwasiliana na Rais Kikwete kutaka ushauri na Rais angewasiliana na Pinda ili aandae taratibu za kutangazwa bungeni na siyo kutangaza kupitia vyombo vya habari.
"Tatizo hapa Luhanjo aliharakisha mno kutangaza suala hili kupitia kwenye vyombo vya habari tena kwa mbwembwe kana kwamba alikuwa na dukuduku moyoni mwake la kuwaonyesha ubabe wabunge," alisema Shellukindo.
Kamati Teule
Spika wa Bunge, Anne Makinda juzi alitangaza majina ya wabunge watano, wanaounda Kamati Teule kuchunguza utaratibu uliotumiwa na Wizara ya Nishati na Madini, kukusanya fedha kutoka katika taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kupitisha wa bajeti.
Alisema kamati hiyo itakayofanya kazi kwa wiki zisizozidi nane pia itachunguza iwapo hatua ya Katibu Mkuu Kiongozi, Luhanjo, kutangaza matokeo ya uchunguzi dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo uliingilia haki na madaraka ya Bunge.
Hii ni kamati teule ya pili kuundwa wakati wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, lakini kwa wizara hiyohiyo ya Nishati na Madini ambayo hivi sasa inaongozwa na Waziri William Ngeleja.
Maadili ya watumishi
Kuhusu maadili ya utumishi kwa kipindi hiki akilinganisha na alipokuwa Ikulu, Shellukindo alisema nidhamu ya watumishi imeshuka na hili linaiweka pabaya Serikali ikiwamo kuvuja kwa baadhi ya siri za Serikali.
Alisema nidhamu katika utumishi imeshuka hivi sasa ikilinganishwa na wakati wa utawala wa awamu ya kwanza na ya pili, kwani watumishi walikuwa na uzalendo na nchi yao na ilikuwa ni jambo lisilowezekana kuona siri ya Serikali imevuja.
Alilipongeza bunge kwa kuunda kamati ya kuchunguza sakata hilo na kuwataka watumishi nchini kufanya kazi kwa nidhamu ili kusukuma mbele maendeleo ya nchi kwa kujivika uzalendo kwani utaalamu wao unahitajika kwa kiasi kikubwa.
Luhanjo
Jumanne wiki hii Ikulu ilitangaza kumrejesha kazini Jairo baada ya uchunguzi wa tuhuma dhidi yake za kutenga mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kuhonga wabunge ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo.
Luhanjo alitangaza uamuzi huo katika mkutano wake na waandishi uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam akisema Jairo hana hatia na siku iliyofuata akatakiwa kurejea kazini.Hata hivyo, wabunge walichachamaa na kutaka kuundwa kwa kamati teule ya Bunge.
Hata hivyo, Rais Kikwete alitengua uamuzi huo na kumrejesha Jairo likizo kupitisha uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge.
Kaiza
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Fordia, Buberwa Kaiza aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa Serikali imepoteza uwezo wa kudhibiti viongozi wake.“Katika hili Serikali imepoteza uwezo wa kudhibiti watendaji wake, lakini pia kuratibu shughuli zake, kila mtendaji anatumia nafasi aliyonayo kama mali yake binafsi,” alisema Kaiza.
Alisema zipo athari nyingi ambazo hutokana na vitendo hivyo, watu hupoteza imani na Serikali yao kwa kuidharau na kwamba, migogoro ya wazi huweza kuongezeka.
Jaji Mkwawa
Kwa upande wake Jaji Mstaafu, John Mkwawa alisema kugongana kwa utendaji wa mihimili hiyo miwili ni jambo la kawaida na kuwataka wananchi kuzoea.
Jaji Mkwawa alisema kuwa hali hiyo ni ya kawaida hasa kwa nchi ambazo zina mfumo wa vyama vingi.
"Uamuzi huo ni wa kidemokrasia, lakini kikubwa ni hiyo Kamati Teule ya bunge kufanya kazi yake kwa umakini, haya ni mambo ambayo Watanzania wanatakiwa kuyakubali," alisema Jaji Mkwawa.
Alisisitiza kwamba Luhanjo naye ametumia madaraka yake kutokana na uamuzi alichukua huku akisisitiza kuwa hata uundwaji wa tume nao ni jambo ambalo lipo wazi.
"Tusiogope na kulipa jambo hili tafsiri mbaya wakati mwingine tukubali kuwa migogoro huwa ipo, ila lengo ni kufikia katika hatua nzuri," alisema Mkwawa.
Imeandikwa na Burhani Yakub, Geofrey Nyang'oro na Fidelis Butahe.
No comments:
Post a Comment