Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee
VIGOGO wa CCM wakiwamo Marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa wamelipuliwa bungeni jana wakituhumiwa kuhodhi maeneo makubwa ya ardhi mkoani Morogoro huku wakishindwa kuyaendeleza.
Katika orodha hiyo ya waliolipuliwa wamo pia Mawaziri Wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na John Malecela, Katibu Mkuu wa CCM mstaafu, Philip Mangula, aliyekuwa Naibu wake (Tanzania Bara), Hassan Ngwilizi na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Nawab Mulla.
Tuhuma hizo zilitolewa bungeni Mjini Dodoma na Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee wakati akisoma bajeti mbadala ya upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka 2011/12.
Mdee alisema hali hiyo inawanyima fursa wananchi wa kawaida kumiliki maeneo kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kuongeza kwamba vigogo hao kwa kutumia nafasi zao waliwanyang’anya wananchi ardhi hiyo na kujimilikisha wenyewe lakini kwa sehemu kubwa wameshindwa kuyaendeleza.
“Mheshimiwa Spika, matatizo ya ardhi kwa wakubwa kunyang’anya wanyonge yameikumba pia Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero (Morogoro), ambako mgogoro huu unakumba shamba namba 299 iliyokuwa NARCO Ranches lenye ukubwa wa hekta 49,981,” alisema na kuongeza:
“Taarifa za kiuchunguzi zinaonyesha kuwa maeneo yaliyokuwa yamepangwa kugawiwa kwa wanavijiji wa Kijiji cha Wami, yamegawiwa wanavijiji wafuatao,’’ alisema na kuanza kuwataja vigogo hao kwa majina mmoja baada ya mwingine.
Akitoa orodha hiyo, Mdee alisema Mangula anamiliki hekta 2,000, Mwinyi hekta 2,000 na Mkapa hekta 1,000 ambaye hata hivyo, ndiye pekee aliyeweza kuliendeleza shamba lake.
Katika orodha yake, Mdee alimtaja pia Sumaye kwamba anamiliki hekta 500, Malecela hekta 100 na Ngwilizi ambaye anamiliki hekta 100 huku akisisitiza orodha hiyo ni ndefu.
Mdee aliitaka Serikali itoe maelezo ya ni vigezo vipi vilitumika kuwagawia ardhi viongozi hao huku wakiwanyima ardhi wananchi wa maeneo husika.
Akizungumzia maeneo mbalimbali yaliyoporwa ardhi na kupewa wawekezaji, msemaji huyo alitaja Shamba la Mpunga la Mbarali ambalo alisema kuwa amepewa Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo kwa bei ya kutupa.
“Hata kule Mbeya Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo, Nawab Mulla amemilikishwa eneo hilo huku wananchi zaidi ya 30,000 wakigeuka kuwa wapangaji katika eneo hilo kwa kukodi ili waweze kulima na kujipatia kipato,’’ alisema na kuongeza:
“Wakati shamba la Mbarali akipewa mwenyekiti kwa bei ya kutupa, Shamba la Kapunga lilikabidhiwa kwa Kampuni ya Export Co. Ltd kwa bei ya kutupa ya Sh2.3 bilioni huku mmiliki akiwa ni Jeetu Patel, hii ni hatari kwa mustabali wa nchi yetu.’’
Alisema hali hiyo ikiachwa inaweza kusababisha umwagaji wa damu kwa Watanzania wasiokuwa na hatia kwa kuwa baadhi ya wajanja kwa kutumia nafasi zao wanamiliki maeneo makubwa bila ya kuwa na huruma kwa wengine.
Kodi za pango
Waziri kivuli huyo aliishutumu Serikali kwa kutumia vibaya fedha za walipa kodi kwa kushindwa kulipia kodi za pango katika maeneo mbalimbali, huku Bunge likipitisha kila wakati bajeti ya kulipia fedha hizo, akahoji ni wapi na mfuko gani zinakopelekwa?
Alisema hadi Machi mwaka huu, Serikali na taasisi zake ilikuwa inadaiwa jumla ya Sh1.543 bilioni baada ya kupunguza malimbikizo kwa kiasi cha Sh115 milioni sawa na asilimia nane tu ya madeni yote licha ya kuwa kila mwaka zinatengwa fedha za kulilipa shirika la nyumba.
Rutabanzibwa naye alipuliwa
Katika hatua nyingine, baadhi ya wabunge jana walimlipua Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa wakisema amekuwa kikwazo na chanzo cha migogoro mikubwa ndani ya wizara hiyo.
Wakichangia katika hotuba hiyo, walisema tangu katibu huyo alipopewa jukumu katika wizara hiyo kila siku imekuwa ni migogoro.
Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu alisema katibu huyo amesababisha migogoro mikubwa katika eneo la Kurasini ambako kila wakati amekuwa akitoa maelekezo bila hata ya yeye kufika.
Mtemvu alisema kitendo cha Rutabanzibwa kuamua kutumia nafasi yake kwa makusudi na kuagiza mambo bila hata ya kufika katika eneo husika, ni tatizo kwani hajui hali halisi iliyopo.
“Nataka nikwambie Mheshimiwa Waziri kuwa Katibu wako ni tatizo kubwa tena atakuponza huyo maana kila siku anafanya kazi ya kuagiza bila ya kujua kitu chochote kinachoendelea hafai huyu, lazima mumwangalie,’’ alisema Mtemvu.
Kwa upande wake, Danstan Kitandula (Mkinga-CCM), alisema maagizo ya katibu huyo kuhusu masuala ya ardhi yamevuka mipaka kwani anafanya mambo ambayo mengine ni hatari kwa mustakabali wa nchi.
Kitandula alisema katibu huyo alifika wakati wa kupingana na maagizo yaliyotolewa na Katibu Mkuu Tamisemi ya kutaka kusitisha utoaji wa ardhi katika eneo la vijiji, ambavyo viko mpakani mwa Tanzania na Kenya, lakini yeye wa maslahi yake aliandika barua ya nguvu ili mwekezaji apewe.
Mbunge huyo alisema kumekuwa na hali ya kutofautiana kwa viongozi wa juu wa Serikali, ambao wanatoa mawazo ya kupingana kila wakati jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa nchi.
“Mheshimiwa Spika, mimi siungi mkono hotuba hii, kwa kuwa hata wananchi wa Mkinga wamenituma nisiunge mkono, tatizo kubwa hapa ni huyu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kila kitu anakifanya kwa ubabe bila hata ya kushirikisha mawazo ya wenzake,’’ alisema Kitandula.
Mbunge huyo alisema katika eneo ambalo Katibu huyo alilazimisha apewe mwekezaji ambalo ni zaidi ya hekta 25,000, kulikuwa na mwananchi mzawa alitaka kupewa hekta 3,000 lakini alinyimwa lakini alipofika mwekezaji mwenye asili ya Kitaliano alipewa eneo hilo bila masharti.
No comments:
Post a Comment