Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge akichangia mjadala wa makadirio, mapato na matumizi ya wizara ya ujenzi kwa mwaka wa fedha 2011/2012
WAKATI Kamati Kuu ya CCM (CC), ikitaka makada wake wenye tuhuma mbalimbali za ufisadi kuwajibika wenyewe kwa kujiuzulu nyadhifa zao zote ifikapo kikao kijacho cha Halmashauri yake Kuu (Nec) Septemba, mwaka huu Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge amevunja ukimya akiwataka wananchi wa jimbo lake kupuuza kile alichokiita maneno dhidi yake.
Chenge ambaye amekuwa akinyooshwewa vidole kuhusu tuhuma hizo amekuwa kimya kwa muda mrefu hata alipofuatwa kutoa maoni yake baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz mnamo Julai 13, mwaka huu. MwanaCCM mwingine aliyetakiwa kutoa maoni yake juu ya hilo alikuwa ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ambaye aliahidi kuchukua hatua muda mwafaka ukifika.
Chenge ambaye aliwahi kuliambia gazeti hili: "Sijui kama mimi ni gamba," jana alitumia sehemu ya dakika zake 15 za kuchangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kuwatoa hofu wapigakura wake.
Mwanasheria huyo Mkuu (AG) mstaafu ambaye amekuwa akitajwa katika tuhuma za rada ambayo Serikali iliinunua kutoka Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza, alitumia muda huo kubeza maneno dhidi yake: "Naomba wananchi wa jimbo langu msisikilize maneno dhidi yangu, naomba tushirikiane."
Aliwashukuru wananchi wa jimbo lake kwa kuzidi kumuunga mkono na kuwataka waendeleze ushirikiano wao ili kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo.
Mbali ya kauli hiyo ya bungeni jana, Chenge aliwahi pia kuziita tuhuma hizo za rada kama, "makandokando dhidi yake," ambayo hayana mantiki wakati alipofanya mkutano na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya Courtyard alipokuwa akitangaza azma ya kuwania uspika wa Bunge la Kumi.
Tuhuma za rada dhidi ya Chenge zilishika kasi zaidi mwaka 2008 baada ya uchunguzi wa Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO) kutangaza kwamba imekuta kiasi cha Dola za Marekani 1.2 milioni (zaidi ya Sh1.2bilioni), kwenye akaunti yake alizokuwa amezificha kisiwani Jersey, lakini aliziita, "ni vijisenti tu."
Kutokana na tuhuma hizo, Chenge alilazimika kujiuzulu wadhifa wa Waziri wa Miundombinu.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah alisema uchunguzi dhidi ya fedha hizo umekamilika na jalada lilikuwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP) kwa hatua zaidi. Hata hivyo, DPP Eliezer Feleshi alikaririwa akikanusha kupokea faili hilo.
Chenge akichangia mjadala wa hotuba hiyo jana, alieleza mafanikio kadhaa katika sekta hiyo kwa kumpongeza Waziri Dk John Magufuli, Naibu wake, Dk Harrison Mwakyembe na watendaji wa wizara hiyo kwa kazi kubwa.
Aliwaponda wapinzani wanaosema kuwa Serikali haijafanya kitu katika ujenzi wa barabara nchini... “Hawa wanaosema Serikali haijafanyakitu hawatembei nchi hii. Ukweli ni kuwa kazi kubwa imefanywa katika sekta ya ujenzi.”
Alitoa mifano ya utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya barabara ambayo inaunganisha kanda zote, ikiwamo ya kuunganisha Tanzania na nchi jirani.Hata hivyo, alitaka maelezo ya wizara hiyo juu ya ukimya kuhusu upembezi yakinifu wa mradi wa barabara iliyokuwa inapaswa kujengwa kwa lami kutoka Kolandoto, Mwamuzi kupitia Lalago.
Pia aliomba kuboreshwa kwa barabara inayotoka Karatu Oldian, Mago’ola kupitia mwamuzi hadi Shinyanga ambayo ni muhimu kwa kuwa inaiunganisha Arusha na Mkoa wa Shinyanga.
Hotuba ya Magufuli yavutia
Awali, Dk Magufuli alitoa hutuba ya wizara yake ambayo iliwavutia wabunge wengi huku ikibainisha mipango ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara kadhaa na kuanza usanifu wa miradi mingine, ikiwamo ya kutoka Mto wa Mbu, Wilaya ya Monduli hadi Makutano mkoani Mara, iliyokuwa inapigwa vita na wanaharakati.
Katika hutuba hiyo, Waziri Magufuli aliitaja miradi mbalimbali ya barabara ambayo itaanza kutekelezwa mwaka 2011/12 lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwapo ongezeko la barabara za lami zinazounganisha mikoa nchini.
Alisema Serikali katika mwaka wa fedha 2011/12, imepanga kujenga nyumba 47 za viongozi na ghofofa moja katika mikoa 12 nchini.
Alisema nyumba 28 na ghorofa moja litajengwa Dar es Salaam, mbili mkoani Dodoma na kuongeza: “Tunataka nyumba hizi 28 zijengwe Dodoma ili kwenda na azma ya kuhamia Dodoma makazi ya Serikali.”
Maoni ya Kamati ya Bunge
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Anne Kilango Malecela aliiomba wizara hiyo kuacha kuendelea kujenga nyumba za Serikali Dar es Salaam na badala yake zijengwe Dodoma ili kutimiza azma ya kuhamia makao makuu.
Pia kamati hiyo ilishauri kuundwa kwa Wizara ya Dar es Salaam au mamlaka maalumu ya kusimamia jiji hilo ili kuondoa kero mbalimbali zinazolikabili.Alisema jiji la Dar es Salaam linapaswa kupewa mtazamo wa kipekee kwani msongamano kwa siku moja tu husababisha harasa ya Sh4bilioni.
Wenyeviti wa CCM kupambana na gamba
Baadhi ya wenyeviti wa CCM wa mikoa wamepania kushinikiza kutenguliwa kwa uamuzi wa CC kuhusiana na mkakati huo wa kuwataka makada wake kujivua gamba.
Mmoja wa wenyeviti hao alisema jana kwamba wanasubiri kwa hamu mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) akisema hawako tayari kuona chama kikisambaratika.
“Subirini halmashauri kuu mtasikia, haya wanayoyataka hayana maslahi kwa chama ni makundi ya urais mwaka 2015.” alisema.
No comments:
Post a Comment