TANGAZA BIASHARA YAKO HAPA NA UONE FAIDA YAKE

Kwa Habari au Tangazo lolote la Biashara tuwasiliane kwa Simu 0713 - 581741 au 0755 - 863097.Email: robadio8@gmail.com

Monday, August 8, 2011

Chadema yafanya 'maamuzi' magumu

Madiwani wa Chadema wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Kuanzia kushoto Estomih Mallah wa Kata ya Kimandolu, John Bayo wa Kata ya Elerai, Ruben Ngowi wa Kata ya Themi, Rehema Mohamed wa Viti Maalum na Charles Mpanda wa Kata ya kaloleni, wakijadiliana jambo kabla ya kuingia katika kikao cha Kamati Kuu ya Chama hicho ili kuhojiwa, mjini Dodoma jana

KAMATI Kuu (CC) ya Chadema jana imetangaza kuwatimua uanachama madiwani watano wa chama hicho katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, akiwamo Naibu Meya, Estomih Mallah kwa tuhuma za kudharau uamuzi wa chama hicho na kumaliza tambo za muda mrefu za wawakilishi hao wa wananchi.

Madiwani hao wamekuwa kwenye mvutano na uongozi wa juu wa Chadema wakipinga uamuzi wa CC ya chama hicho uliowataka kuomba radhi baada ya kuingia muafaka huo bila ridhaa ya uongozi huo wa juu katika mgogoro huo.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana alitangaza uamuzi huo aliouita 'maamuzi magumu' baada ya kusema juhudi nyingine za kutafuta suluhu zimekwama.

Mbowe aliwataja madiwani hao kwamba ni pamoja na Mallah wa Kata ya Kimandolu, John Bayo (Elerai), Reuben Ngoi wa Kata ya Themi, Charles Mpanda wa Kaloleni na Diwani wa Viti Maalumu, Rehema Mohamed. Alisema kwamba kutokana na kufukuzwa uanachama, kisheria wanasiasa hao wamepoteza pia nafasi zao za udiwani. Diwani mwingine, Cyprian Tarimo wa Kata ya Sekei hakuhukumiwa kwa kuwa hakufika Dodoma kujitetea kutokana na kuwa na udhuru.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mbowe alisema Kamati Kuu ya Chadema ndiyo iliyofikia uamuzi huo mgumu lakini kwa shingo upande: "Kwa masikitiko makubwa Kamati Kuu ya Chadema kutokana na mamlaka kikatiba, imewafukuza uanachama madiwani watano kwa kukataa kutekeleza uamuzi halali wa chama.”

Hata hivyo, wakizungumza katika Hoteli ya Durban waliyokuwa wamefikia mjini hapa jana, madiwani hao walisema kwamba wanapinga uamuzi huo na kuahidi kukata rufani katika Baraza Kuu la chama hicho.

“Tulikuja Dodoma tukijua tunakuja kufukuzwa lakini, tuliamini huenda busara zingetumika na kutambua kuwa uamuzi wetu wa kuingia katika muafaka ulikuwa ni sahihi kwa manufaa ya Mji wa Arusha,” alisema Mallah ambaye ni Mwenyekiti wa madiwani na kuongeza kwamba wanatarajia kukutana na wananchi waliowachagua na kueleza kilichotokea hapa Dodoma.

Awali, Mbowe alisema Kamati Kuu ilipokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa Julai 17, mwaka huu iliyowataka madiwani hao baada ya kusaini muafaka huo kujiuzulu. Alisema madiwani hao pia waliagizwa kuomba radhi kwa makosa waliyokuwa wamefanya kutokana na mwafaka uliofikiwa baina yao na madiwani wa CCM na TLP bila ridhaa ya chama.

“Kamati Kuu imezingatia kuwa kati ya madiwani kumi na moja waliopewa maelekezo na kamati kuu, watano ndiyo walitekeleza na kuomba na radhi na madiwani sita waligoma,"

Alisema baada ya kutafakari kwa kina taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Kamati Kuu na kuwapa nafasi ya kujieleza mbele yake, madiwani hao walikataa kutekeleza uamuzi huo.

“Kamati Kuu imezingatia kuwa kitendo cha madiwani hao kukataa kutekeleza maagizo yake halali ni utovu mkubwa wa nidhamu na ni kuvunja maadili na kanuni za chama," alisema Mbowe.

Pinda, Mbowe walizungumza
Kamati Kuu ya Chadema pia ilipokea taarifa ya mazungumzo baina ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mbowe kuhusiana na kumaliza mgogoro huo na kueleza kwamba wamekubaliana kuunda kwa kamati ya kitaifa ya kushughulikia mgogoro huo wa Umeya.

Mbowe alisema mazungumzo ambayo yalifanyika juzi nyumbani kwa Waziri Mkuu, yalihudhuriwa pia Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa: “Kamati hii itakuwa na wajumbe kutoka CCM na Chadema, itaundwa haraka iwezekanavyo ndani ya mwezi mmoja na mwenyekiti anatarajiwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa.”

Mwenyekiti huyo wa Chadema alisema kamati hiyo pia itawajumuisha makatibu wakuu wa vyama vya CCM na Chadema ambao ndiyo watakaoteua wajumbe.Hata hivyo, alisema kwa sasa madiwani wote wa Chadema hawataruhusiwa kuingia katika vikao vya Baraza la Madiwani wala kumtambua Meya wa Arusha, Gaudence Lymo hadi hapo muafaka utakapopatikana.

Kwenda Arusha
Katika kile kinachoonekana ni kusafisha hali ya hewa, ujumbe mzito wa Kamati Kuu ya chama hicho, ukiongozwa na Mbowe, Dk Slaa, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na wajumbe wengine utafanya mkutano mkubwa wa hadhara keshokutwa jijini Arusha.Mbali na mkutano huo wa hadhara wajumbe hao, watakuwa na mikutano katika kata nne ambazo madiwani wao wametimuliwa.

Mgogoro wa umeya Arusha ni sehemu ya majeraha ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambao chama hicho cha upinzani kilipata nguvu zaidi katika nafasi za urais na ubunge, ikilinganishwa na vyama vingine vya upinzani nchini.

Kutokana na Chadema kukataa matokeo ya umeya Arusha kutokana kura iliyopigwa na Mary Chatanda ambaye chama hicho kilisema kwamba hakustahili kwa kuwa ni Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, kuliibua ghasia zilizosababisha mauaji baada ya chama hicho kufanya maandamano hayo kwa nguvu.

Katika kushughulikia mgogoro huo wa madiwani, Chadema pia kiliunda kamati maalumu ya uchunguzi chini ya kada wake, Mabere Marando na matokeo yalionyesha kuwa ingawa waliingia muafaka huo bila ridhaa ya chama makao makuu, hapakuwa na ushahidi wowote kuthibitisha kama madiwani hao sita walihongwa.

Hatima ya Shibuda bado
Taarifa zilisema hatima ya Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda bado haijafahamika kwani taratibu za kumhoji zimekuwa zikiendelea chini ya jopo maalumu linaloongozwa na Profesa Abdallah Safari ambaye alipewa jukumu hilo na kikao cha CC iliyoketi mwezi uliopita.

Tayari CC ilisema jopo hilo halimchunguzi Shibuda kuhusiana na kauli zake kuhusu msimamo wake wa posho alioutoa bungeni akipinga msimamo wa kambi ya upinzani, bali ni kuhusu mwenendo mbovu wa maadili baada ya kuzungumza mambo mbalimbali nje ya vikao na kwamba, suala la posho bungeni liko chini ya mamlaka za nidhamu za kambi hiyo kwa pamoja na wabunge wa chama hicho.

No comments: